Tumbaku inavyotishia maendeleo kiuchumi na kijamii

SAMUELI Mshomi amelazimika kuacha shughuli zake pamoja na familia na kuongozana na ndugu yake, Maine Mshomi ambaye yupo jijini Dar es Salaam akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Ocean Road.

Samuel ambaye anaendesha shughuli za kilimo na biashara, kwa zaidi ya miezi mitano hawezi kuzalisha chochote kwani muda wake wote ameutumia kuzunguka na mgonjwa wakisaka matibabu katika hospitali mbalimbali nchini.

Wakazi hawa wa wilayani Kiteto katika Mkoa wa Manyara, baada ya kuzungukia hospitali tofauti, Aprili mwaka huu walifika katika hospitali ya Ocean Road alikolazwa akipatiwa matibabu ya saratani ya koo.

Akiwa katika hospitali hiyo ambayo ni maalumu kwa wagonjwa wa saratani za aina mbalimbali, katika mahojiano na timu ya waandishi wa habari waliofika hapo, Maine ambaye ni mkazi wa kijiji cha Lugine anasimulia kuwa baada ya kuhisi maumivu, alikwenda katika hospitali mbalimbali.

Miongoni mwake ni hospitali ya Mvumi iliyopo mkoani Dodoma pamoja na KCMC ya mkoani Kilimanjaro kabla ya kwenda Ocean Road ambako alipimwa na kugundulika kuwa ana saratani ya koo.

Ingawa hajaambiwa na madaktari chanzo cha ugonjwa, anakiri maelezo ya daktari yameonesha moja kwa moja matumizi ya tumbaku ndiyo yamechangia. Maine anasema amekuwa akijigharimia matibabu na huduma mbalimbali na wakati akizungumza na waandishi, Agosti mwaka huu, alikuwa ametumia si chini ya Sh milioni 1.7.

Kwa upande wake Samueli (anayemuuguza Maine) mkazi wa kijiji cha Songambele, wilayani Kiteto, anasema analazimika kutumia sh 5,000 kila siku kwa ajili ya chakula hali ambayo imeathiri pia familia yake aliyoiacha kijijini.

“Tangu mwezi wa tatu (Machi) nimeshindwa kufanya shughuli zangu za kilimo na biashara zangu ndogo ndogo,” anasema Samueli akisisitiza kuwa kwa namna ambavyo ndugu yao alikuwa akivuta sigara/tumbaku na maelezo ya daktari, ni dhahiri ugonjwa wake umetokana na kuathiriwa na bidhaa hiyo. Maine anakiri kuwa alikuwa akivuta misokoto ya tumbaku kati ya minne na mitano kwa siku.

Alipokuwa akienda katika maeneo yenye mkusanyiko wa watu, alikuwa akinunua sigara dukani na kuendelea kuvuta. Sasa tumbaku/sigara siyo tu kwamba zimeathiri afya ya baba huyu mwenye umri wa miaka 55 aliyeanza kuvuta tangu akiwa kijana; bali pia ugonjwa umegeuka mzigo kwa familia na hata taifa kwa ujumla kutokana na gharama zinazoingiwa.

Kwa ngazi ya familia, Samueli anakiri tumbaku inaleta umasikini kutokana na familia kusimamisha uzalishaji na wakati huo huo fedha kuingizwa kwenye gharama za matibabu ya saratani hiyo ya koo.

Mkurugenzi wa Huduma za Kuzuia saratani wa Ocean Road, Dk Chrispin Kahesa anaeleza kuwa saratani za njia ya kinywa na chakula zinaongezeka. Anatoa mfano kwa wanaume kuwa saratani inayoongoza ni ya ngozi ikifuatiwa na njia ya chakula.

Anasema idadi inaongezeka na inaendana moja kwa moja na matumizi ya tumbaku. “Ila idadi tunayoiona hospitali ni ndogo labda wengine wanafariki dunia bila kutambulika hasa wakiwa kwenye maeneo wanayoishi, hasa ukizingatia wananchi wengi wanaoshiriki katika kilimo cha tumbaku wametoka katika maeneo ambayo yako chini kiuchumi, wakati mwingine hawapati fursa ya kufika katika maeneo ya tiba,” anasema Dk Kahesa.

Anatoa mfano: Ukienda Katavi kuna matatizo mengine ya kiafya ambayo yanaendana kabisa na matumizi ya tumbaku kama vile upungufu wa nguvu za kiume. Kwa hiyo hata saratani inaweza ikawepo sana lakini hawagunduliki kwa sababu hawafiki hospitalini au wanaweza kuwa wamefariki kwa magonjwa mengine.

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), Dk Mohamed Janabi anathibitisha tumbaku kuwa na athari kiuchumi akieleza kuwa gharama za vipimo na matibabu ya moyo ni kubwa hususani inapolazimu kumwekea mgonjwa chuma.

Kwa mujibu wa Dk Janabi, kumwekea mgonjwa chuma kimoja si chini ya Sh milioni tatu. “Ukiwekewa vyuma viwili au vitatu na ukiwa ni ugonjwa uliosambaa, utasababisha mzigo mkubwa sana kwa serikali, kwa jamii na mtu binafsi.”

Dk Janabi anasema wanaovuta sigara kwa muda mrefu na kwa kiwango kikubwa; takribani pakiti moja mpaka nne kwa siku, wanajijengea hisia kichwani kwamba wakiwa kwenye msongo wa aina yoyote, wakivuta watatulia.

“Akivuta sigara inamtuliza kidogo, ukitazama kwa haraka faida yake unaipata kwa muda mfupi lakini kwa muda mrefu mishipa ikiharibika moyo utaanza kutofanya kazi vizuri tutalazimika kukuwekea stendi (chuma) au kwenda kwenye bypass ambayo ni upasuaji mkubwa zaidi wa kupandikiza mishipa ya damu kutoka mkononi au miguuni,” anasema Dk Janabi.

Anasema athari za tumbaku/ sigara ni kwenye mishipa ya damu ya mwili mzima ikihusisha ubongo, figo, utumbo. Anasisitiza: Athari za sigara siyo kwamba ipo kwenye moyo tu, ni ya mwili mzima.

Kwa ujumla, kila kiungo kwenye mwili wetu kinakuwa affected (kimeathirika) kama tunavyosikia siku hizi magonjwa kama vile saratani ya mapafu ambayo sababu yake kubwa ni uvutaji, figo kuharibika, magonjwa ya akili na ule moshi unaingia kwenye mapafu.”

Kwa mujibu wa Dk Janabi, kitaalamu, ili moyo upige vizuri ni lazima mishipa ya damu ifanye kazi vizuri na kama moyo haupigi vizuri lazima kunakuwepo mishipa ambayo haifanyi kazi vizuri.

Mtaalamu huyu anafafanua zaidi kuwa kila moyo ukipiga mara moja unapaswa utoe mililita 70 za damu na ukipiga mara 70 ni sawa na mililita 4,900 ambazo ni sawa na lita tano za damu ambayo ndiyo binadamu anapaswa kuwa nayo.

Moyo unapokuwa haupigi unavyotakiwa (mfano badala ya kupiga mara 70 unapiga mara 30 au 40 ), maana yake ni kwamba damu inayotoka ni chache na ikiwa chache ndipo mgonjwa anaweza kuonekana miguu imevimba, hajisikii vizuri.

Baada ya hapo, anatakiwa kwenda kwenye kipimo kikubwa ambacho gharama yake ni Sh milioni mbili kuchunguza mishipa kujua ni upi uliobana kwa sababu moyo una mishipa mingi.

“Kwa mfano tunakuta mshipa wa kushoto umebana kwa asilimia 70 tunachofanya ni kuchukua hatua, unamwekea stendi ili damu iweze kutiririka vizuri zaidi hali yake inarudi kawaida na hapa ndipo tunamsisitiza aache vitu vilivyopelekea huko,” anasema.

Pamoja na kusisitiza udhibiti wa matumizi ya tumbaku, Dk Janabi anashauri Watanzania kujenga utamaduni wa kupima afya ili kugundua matatizo mapema na kupata matibabu.

Anatoa mfano kwamba, kama mshipa mkubwa umebana kwa asilimia 90 au 100, mgonjwa ana saa moja na nusu tu kabla hajafikishwa hospitalini, akichelewa mara nyingi matokeo yake ni kifo.

Dk Janabi anasema vita dhidi ya tumbaku inapaswa ishike kasi ikizingatiwa kuwa licha ya magonjwa yasiyoambukizwa, bado Tanzania iko katika mapambano yale ya kuambukiza hususani Malaria, Typhoid, kipindupindu.

“Sasa wakati tukiwa kwenye kupigana na haya ya kuambukiza, sasa yamekuja magonjwa ya kutoambukiza (NCD). Wenzetu Ulaya na Marekani walikuwa na bahati, kwanza yalikuja magonjwa ya kuambukiza wakaweza kushughulika nayo yakaisha,” anasema .

Shirikisho la Vyama vya Magonjwa yasiyoambukizwa Tanzania (TANCDA) katika kuhamasisha jamii kuchukua hadhari dhidi ya magonjwa hayo, linakiri kuwa magonjwa haya yana athari kwenye uchumi na watu .

Katika kampeni yake ya mwaka huu kupinga magonjwa yasiyoyaambukiza, shirikisho kupitia kwa Dk Tatizo Waane linasema watu wengi wamekuwa hawatilii maanani magonjwa yasiyoambukiza licha ya kwamba yana athari kubwa kiafya na kiuchumi kwa watu na taifa.

Ili kuhakikisha kuwa tumbaku na mazao yake yanadhibitiwa isiendelee kuchangia ongezeko la magonjwa yasiyoambukiza hususani moyo na saratani, Chama cha Kudhibiti Tumbaku Tanzania (TTCF) kinahimiza mkakati wa kilimo mbadala wa tumbaku.

Chama hicho kupitia kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Kudhibiti Tumbaku nchini, Lutgard Kagaruki kinasimamia kaulimbiu ya Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) siku ya kutotumia tumbaku duniani, Mei 31 mwaka huu inayosema ‘Tumbaku tishio la maendeleo’.

Kagaruki anasisitiza umuhimu wa wakulima kuwezeshwa kulima mazao mengine yenye soko na faida kwa afya ya binadamu badala ya tumbaku. Anasema wakati hapa nchini uzalishaji wa tumbaku unaongezeka, kwa upande wa Kenya na Uganda kilimo hicho kinashuka kutokana na wakulima kujikita katika kulima mazao mbadala.

Hata hivyo, mkurugenzi huyo wa TTCF anasema kinachosikitisha ni kuona kampuni zikija nchini na kufungua ofisi na kueneza kilimo cha tumbaku. Lakini anasisitiza kwamba hakuna nchi duniani iliyoendelea kupitia biashara ya tumbaku.

Ingawa vita dhidi ya tumbaku inatajwa kuwa ni ngumu kwa kuwa inapingana na kampuni zenye utajiri mkubwa zinazoiendesha, Kagaruki anaamini kuwa wakulima wakipata mazao mengine yenye soko, wataacha wenyewe kilimo cha tumbaku. Chama hicho kinasisitiza jamii kuendelea kuelimishwa juu ya madhara na athari za tumbaku kwa maendeleo ya watu kiuchumi, kijamii na kimazingira.