Wapendekeza sheria moja ya uvuvi EAC

TANZANIA, Uganda na Kenya zimejaliwa na Mwenyezi Mungu kuwa na maliasili muhimu ya Ziwa Victoria zinazotumiwa na nchi hizo ingawa bonde la ziwa hilo pia linazihusisha pia karibu nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

Ziwa hilo lenye ukubwa wa kilomita za mraba 68,800 ni la kwanza kwa ukubwa barani Afrika na la pili kwa ukubwa duniani baada ya Ziwa Superior lililopo Marekani ya Kaskazini. Ziwa Victoria lipo futi 3,726 kutoka usawa wa bahari. Maji yake yanamiminika kwenye Mto Nile na kuelekea katika Bahari ya Mediteranea kwa umbali wa maili 4,000.

Mgawanyo wa kimataifa umeihalalisha Tanzania kumiliki asilimia 51 ya ziwa hilo, Uganda asilimia 43 na Kenya asilimia sita ya ukubwa wa Ziwa Victoria linalobeba rasilimali za samaki na maji baridi. Ziwa hilo ni miongoni mwa vyanzo vikuu vya maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa takribani nchi zote za EAC. Kwa takwimu za mwaka 2004 kupitia filamu ya Darwin’s Nightmare, kulikuwa na boti 51,712 na wavuvi 153,066 katika ziwa hilo.

Takwimu pia zinaonesha kwamba uzalishaji wa sangara kwa ajili ya soko la nje katika miaka ya 1990 ulifikia tani 500,000 kwa mwaka, lakini kiwango kimekuwa kikizidi kupungua mwaka hadi mwaka. Hata kiwango cha samaki wengine kwa ajili ya matumizi ya wananchi wengine wanaolizunguka kimekuwa pia kikipungua mwaka hadi mwaka.

Ni dhahiri ziwa hilo linaweza kuendelea kuwa tegemeo muhimu la kiuchumi na kijamii kwa raia wa nchi hizo ikiwa zitaamua kutumia sheria moja ya uvuvi wa samaki na matumizi ya maji yake. Hii ni kutokana na ukweli kwamba rasilimali za samaki na maji zinasambaa katika ziwa hilo pasipo kutambua mipaka iliyowekwa ya nchi za Tanzania, Kenya na Uganda.

Inaaminika kwamba kwa kuwa na sheria moja ya matumizi ya rasilimali za ziwa na kuisimamia ipasavyo itaepusha migogoro isiyo ya lazima, hasa baina ya jumuiya za wavuvi katika nchi hizo. Shirika la Muungano wa Wavuvi (FUO) mkoani Mwanza, Tanzania, linaamini kwamba kutumia sheria moja kutawezesha nchi hizo kunufaika zaidi na rasilimali za ziwa hilo na kwa usawa kuliko ilivyo sasa.

Mwenyekiti Mtendaji wa FUO, Juvenal Matagili, anasema hatua ya Tanzania kuweka kiwango (standard) cha nyavu zenye matundu yenye ukubwa wa inchi saba kuvua samaki huku na Uganda na Kenya zikitumia kiwango chao cha chini kikiwa nchi tano hakitoi uwiano wa mavuno sawa ya samaki katika ziwa hilo. “Wanaotumia nyavu zenye matundu ya inchi tano wanavua samaki wadogo na wengi ikilinganishwa na wanaotumia nyavu zenye matundu ya inchi saba.

Hivyo ingependeza kuwa na sheria na sera moja katika ziwa na sheria hiyo ikasimamiwa ipasavyo katika kila eneo,” anasema Matagili ambaye ni mvuvi mstaafu. Matagili anaamini kwamba tofauti hiyo ikiendelea itazidi kushusha mavuno ya samaki kwa upande wa Tanzania na kuwawia vigumu wavuvi wa nchi hiyo kupata samaki wenye ukubwa wa nchi saba kwa kuwa matumizi ya nyavu zenye matundu yenye ukubwa wa nchi tano zinavua wale ambao hawajafikia ukubwa huo.

Hivi karibuni viongozi wa kisiasa kutoka nchi za Uganda na Kenya walipendekeza kuanzisha mikakati ya kurekebisha sheria za usimamizi wa rasilimali za ziwa hilo kuepusha mgogoro baina ya nchi hizo. Kwa mujibu kituo cha redio cha Voice of America (VOA) kiliripoti kwamba katika mkutano wa pamoja uliofanyika Busia, Kenya, Waziri Msaidizi wa Masuala ya Jumuiya (EAC) kutoka Uganda, John Maganda, alikiri kuwepo kwa mgogoro kuhusu uvuvi na matumizi ya maji ya ziwa hilo.

“Ziwa Victoria ni mali ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, tunapata samaki, tunalitumia kwa usafiri kutoka Jinja, Uganda hadi Kisumu, Kenya na mpaka Mwanza, Tanzania hivyo lazima tuepushe migogoro iliyopo au inayoweza kujitokeza,” Maganda alinukuliwa akisema katika mkutano huo. Mbunge wa Funyula, nchini Kenya, Paul Otwoma, aliunga mkono suala la nchi za EAC kuwa na sheria moja ya matumizi ya rasilimali za ziwa hilo.

“Samaki hawajui mipaka... Wanazaliwa huku, wanaenda kule, sheria lazima ziwe na usawa kwetu sote (akimaanisha Kenya, Uganda na Tanzania) na kuwezesha leseni moja kutumika kwa wavuvi wote bila kuzingatia nchi wanakotoka,” anasema Otwoma.

Wadau pia wanaona haja kwa serikali za nchi za EAC kuwa na mikakati ya pamoja ya kukabili vitendo vya uvuvi haramu ukiwamo ule wa kutumia sumu katika Ziwa Victoria ili kuepusha uharibifu wa mazalia ya samaki, uchafuzi wa maji yake na athari za kiuchumi na afya kwa watu.

Mwenyekiti Mtendaji wa FUO, Matagili, anashauri nchi za EAC kuangalia uwezekano wa kununua ndege ndogo au helikopta kwa ajili ya kufanya doria dhidi ya vitendo vya uvuvi haramu katika ziwa hilo badala ya kuendelea kutumia boti ambazo yeye anaona hazikidhi mahitaji hayo.

“Kutokana na kasi yake, matumizi ya ndege yatawezesha kudhibiti uvuvi haramu tofauti na boti zinazotumika sasa ambazo haziwezi kwenda hadi katikati ya ziwa,” anasema. Pia, anashauri serikali ya Tanzania kufikiria mpango wa kuhamisha watu katika baadhi ya visiwa ili kurejesha uoto wa asili unaochochea mazalia ya samaki ndani ya ziwa hilo.

Anataja baadhi ya visiwa ambavyo watu wanaishi na kuendelea kuharibu mazingira rafiki kwa mazalia ya samaki upande wa mkoa wa Mwanza kuwa ni pamoja na Chitandele, Lyakanyasi, Nyazune, Bihira, Ikullu, Mfulubizi, Zilagula, Yuzu, Gembale, Nyamango, Chemagati, Chembaya na Lubalagazi.

“Visiwa hivyo vilikuwa vinachangia hifadhi na mazalia ya samaki kutokana na uoto wa asili lakini kwa sasa mazingira yake yameharibiwa na watu waliojenga makazi kwa ajili ya shughuli za uvuvi,” anasema Matagili na kuongeza: “Kutokana na hali hiyo, samaki sasa hawawezi kuzaana kwenye kingo za visiwa hivyo kwa sababu miti iliyokuwa inasaidia kupatikana kwa vivuli na vipepeo ambao ni chakula cha samaki vimetoweka.”

Anashauri hili pia lifanyike katika nchi zingine za Afrika Mashariki zitazogundua visiwa vya aina hiyo. Kwa upande wake, Mratibu wa Mradi wa Hifadhi ya Mazingira katika Bonde la Ziwa Victoria (LVEMP), Omary Myanza anahamasisha uanzishaji wa mabwawa ya samaki kando ya ziwa hilo kwa wingi kuliko ilivyo sasa ili kupunguza nguvu kubwa ya uvuvi usio endelevu na kuwapa samaki muda wa kuzaliana na kuongezeka.

Nayo Bodi ya Maji Bonde la Ziwa Victoria (LVBWB) inasisitiza kuwa Tathmini ya Athari ya Mazingira (EIA) kabla ya ujenzi wa mabwawa hayo ni muhimu ili kuepusha uchafuzi na uharibifu wa mazingira ya ziwa hillo.

Aidha, LVBWB inahimiza wadau kuzingatia matumizi ya maji kisheria ili kuepusha migogoro ya maji na kuhatarisha maisha ya watu, wanyama, mimea na viumbe hai wengine wanaotegemea maji ya ziwa hilo.

Matumizi sahihi ya maji kwa upande wa Tanzania ni yanayozingatia Sheria ya Usimamizi wa Rasilimali za Maji Namba 11 ya Mwaka 2009 iliyoweka mfumo madhubuti wa kulinda, kuendeleza na kusimamia rasilimali hiyo katika sekta za kijamii na kiuchumi.

Vipaumbele katika matumizi ya maji vimebainishwa katika sheria hiyo kuwa ni; Mosi, matumizi ya nyumbani, pili, hifadhi ya mazingira na tatu, shughuli nyingine za kijamii kulingana na upatikanaji wa rasilimali hiyo.

Sheria hiyo inatambua matumizi ya maji yasiyohitaji na yanayohitaji vibali kutoka bodi ya maji ya bonde husika. Inatamka wazi kuwa mtu yeyote mwenye uwezo wa kufikia maji anayo haki ya kuyatumia bila kibali alimradi asiyachukue kwa bomba, mifereji au njia yoyote inayohitaji miundombinu. Pia, mtu anaweza kuchimba/ kujenga kisima kifupi na kutumia maji kwa matumizi ya nyumbani bila kibali alimradi kisima hicho kisizidi urefu wa mita 15.

Kadhalika, mtu anaweza kuvuna maji ya mvua na kuyatumia nyumbani au kuyasafirisha kwa ajili ya kuyatumia bila kibali ilimradi miundombinu iliyojengwa haizidi uwezo wa kutunza lita 20,000.

Kwa upande mwingine, sheria inatamka kwamba mtu au taasisi yoyote hairuhusiwi kuchukua maji kwa njia yoyote ile (mifereji, mashine ya kusukuma maji, mabwawa) kutoka chanzo chochote kwa matumizi yoyote bila kuwa na kibali kutoka bodi ya bonde husika.

Aidha, mtu yeyote anayetaka kuchepusha, kukinga, kuhifadhi, kuchukua na kutumia maji kutoka chanzo cha maji juu au chini ya ardhi, au kujenga miundombinu yoyote lazima aombe kibali cha kutumia maji.

“Hakuna taasisi yoyote yenye mamlaka ya kutoa kibali cha matumizi ya maji, kwa mujibu wa Sheria ya Usimamizi wa Rasilimali za Maji, isipokuwa Bodi za Maji za Mabonde husika,” kinatamka Kifungu cha 43(3) cha sharia hiyo.

Kwa mujibu wa sheria hiyo, mtu akikutwa anatafiti maji bila leseni kutoka Bodi ya Maji ya Bonde husika atatozwa faini isiyopungua Sh milioni moja au kifungo cha miezi mitano jela, au adhabu hizo kwa pamoja.

“Pia, ukikutwa unachimba kisima cha maji bila leseni kutoka mamlaka husika utatozwa faini isiyopungua shilingi milioni tano au kifungo cha mwaka gerezani, au adhabu zote kwa pamoja,” anasema Mtaalamu wa Maji kutoka LVBWB, Renatus Shinhu.

Mwelimishaji jamii kuhusu maji, Godfrey Mkungu anasema sheria za maji zimetungwa kwa kuzingatia umuhimu wa rasilimali hiyo kwa viumbe hai. “Bila maji hakuna uhai. Maji ni muhimu kwa maendeleo ya kiuchumi na kijamii. Kiwango cha maendeleo ya jamii yoyote duniani kinategemea uwepo wa maji ya kutosha na yenye ubora.

“Katika hali yake ya asili, maji ni sehemu ya mazingira ambapo wingi na ubora wake ndiyo husaidia katika kuamua jinsi yatakavyotumika,” anasema Mkungu. Majukumu ya LVBWB ni kusimamia na kuratibu matumizi bora ya maji, kutoa vibali vya kutumia maji na kutupa maji taka, kukusanya ada za matumizi na kutatua migogoro ya rasilimali hiyo.

Pia kudhibiti, kuchukua hatua dhidi ya wachafuzi wa maji na vyanzo vyake, kuhifadhi na kulinda vyanzo vya maji, kuangalia ubora, usafi wa maji na yatafiti ardhini. Mbali ya uvuvi, ufugaji wa samaki kwenye mabwawa na matumizi ya nyumbani, shughuli nyingine za kiuchumi na kijamii zinazohitaji maji ya Ziwa Victoria ni mifugo, kilimo cha umwagiliaji, viwanda, migodi ya madini, biashara, utalii, ufuaji umeme, usafiri na usafirishaji.

Kwa hiyo, nchi za EAC zina jukumu la kuhakikisha ziwa hilo linadumu katika ikolojia imara inayokidhi mahitaji ya jamii kwa chakula, kipato, maji safi, ajira, mazingira bora yasiyo na magonjwa na kuhifadhi viumbe hai, kama inavyosisitizwa kwenye dira ya LVEMP