Mvua mwaka huu kuwaletea wakulima Chamwino neema?

MSIMU wa mvua umekaribia kuanza. Wakulima wilayani Chamwino mkoani Dodoma wameanza kuberega mashamba yao. Wengine wamepanda licha ya kuwa mvua za mwanzoni mwa Desemba siyo nzuri.

“Lakini hatuna uhakika kama mvua zitarudi mapema kwani zikichelewa zile mbegu zilizopandwa zitapotea,” anasema Ofisa Kilimo wa Wilaya ya Chamwino, Aithan Chaula. Wasiwasi alio nao Chaula unaakisi hali halisi ya uzalishaji mdogo mashambani uliozikabili kaya mbalimbali katika msimu wa kilimo uliopita.

Ukame na mvua zisizotabirika unaochochewa na mabadiliko ya tabia nchi na hivyo kuwa sababu ya uzalishaji mdogo unaochangia umasikini kutokana na ukosefu wa kipato na chakula.

Mathalani, katika vijiji vya Chamwino, Buigiri, Chinagali II na Mwegamile katika Tarafa ya Chilonwa ambavyo gazeti hili lilitembelea na kuzungumza na wakulima, wafugaji pamoja na wadau wengine wa kilimo, ilidhihirika namna ambavyo kaya kadhaa zinakabiliwa na umasikini.

Ofisa Kilimo wa Wilaya ya Chamwino, Chaula anaeleza walivyojipanga kuhakikisha wakulima wanatumia mvua zinazotarajiwa kunyesha hivi karibuni kwa kupanda mazao yanayostawi katika maeneo yao. Anasema pia wamejipanga kuhakikisha wakulima wanapanda katika maeneo yaliyotifuliwa ili kuongeza uzalishaji.

Mtaalamu huyu wa kilimo anasema utifuaji mashamba hufanya maji yasitembee shambani na kwenda kusababisha maporomoko. “Watu wengi hawalimi mpaka chini wanalima kwa kuparua mvua inaponyesha maji yanapita na kuacha udongo ukiwa mkavu,” anasema Chaula akiainisha jinsi ambavyo halmashauri imejipanga kusimamia uzalishaji katika kilimo.

Anaongeza: “Sasa tunajipanga kuhakikisha wakulima wote wanalima kwa kufuata kanuni ili waweze kupata mazao ya kutosha na kuondoa changamoto ya upungufu wa chakula.”

Anazungumzia hali ya upatikanaji wa huduma za kitaalamu kwa kukiri kuwa kumekuwapo malalamiko ya ukosefu wa maofisa ugani katika baadhi ya maeneo. Wilaya ya Chamwino ina vijiji 107.

Anafafanua kuwa maofisa ugani waliopo ni 87. Katika makao makuu ya wilaya wapo 15 na waliobaki wako kwenye kata na vijiji. “Kati ya hao 72 kuna wachache wako masomoni na ukiangalia tuna vijiji 107 ndiyo maana kuna maeneo kuna malalamiko kuwa hakuna maofisa ugani. Lakini sasa tunajipanga kuhakikisha maofisa ugani waliopo wanawafikia wananchi,” anasema.

Chaula anaweka mambo kadhaa yanayosaidia uzalishaji katika kilimo na kukiri kuwa miongoni mwake ni maofisa ugani kufuatilia wakulima. Hata hivyo, anasema ili wakulima waweze kuzalisha kwa wingi, ofisa kilimo anasisitiza pia wao kubadilika na kuacha kilimo cha mazoea kinachowakosesha mavuno. Miongoni mwa mabadiliko ambayo halmashauri inafuatilia kwa karibu ili kuongeza uzalishaji, ni wakulima kupanda mazao yanayolingana na hali ya hewa.

Kulingana na Mwongozo wa Uzalishaji Mazao kulingana na Kanda za kilimo za kiikolojia wa mwaka 2017, mazao ya chakula ya kipaumbele katika Wilaya ya Chamwino ni mtama na njugu mawe na ya biashara ni zabibu na ufuta. Mazao mengine yanayoweza kulimwa ni alizeti, karanga mpunga na viazi vitamu.

Mwongozo huo umezingatia ikolojia ya wilaya hii yenye mwinukowa meta 500 -1,400, mvua milimita 400 – 800 na udongo mwekundu na kichanga. Mambo mengine ambayo mtaalamu huyu wa kilimo anasema yanasaidia kuongeza uzalishaji ni matumizi ya trekta na utifuaji wa mashamba pamoja maofisa ugani kufuatilia wakulima.

Anasema wilaya hiyo sasa ina trekta 92 kubwa zinazofanya kazi. Vilevile zipo trekta ndogo 73 na majembe ya kukokotwa na wanyamakazi. Mkulima wa kijiji cha Mloda wilayani Chamwino, Juliana Madeje anasisitiza kuwa ipo haya ya ufuatiliwa kwa maofisa ugani ili waweze kufika kwa wakulima hususani mashambani.

“Kama serikali inahamasisha kilimo cha kisasa, wataalamu waje mashambani watuelekeze kwa vitendo itasaidia kuhamasisha kilimo,” anasema. Hata hivyo, kwa kuzingatia namna ambavyo mvua imeathiri baadhi ya wakulima na kujikuta wakizalisha kidogo, Ofisa Maendeleo ya Jamii Wilaya ya Chamwino, Rachel Lugeye anasema wanahamasisha shughuli za ujasiriamali ili wananchi wajifunze kuongeza vipato vyao kwenye kaya.

“Wananchi wachangamkie fursa ya kujiunga kwenye kikundi licha ya kilimo, wanatakiwa kuwa wajasiriamali ili wajiongezee kipato,” anasema ofisa maendeleo. Wakati halmashauri ya Chamwino ikiweka bayana mikakati yake ya kuongeza uzalishaji katika kilimo, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk Binilith Mahenge anasisitiza wakulima kupewa mwongozo wa mazao ya kulima.

Anasema wakulima hawawezi kuachwa waamue wenyewe mazao ya kulima. Anasisitiza suala la takwinu za wakulima na mazao wanayolima akisema kuanzia sasa, zitachukuliwa kwa kila kata, kijiji na kitongoji kwa lengo la kuhakikisha wanalima mazao yanayostawi katika maeneo yao.

Akiwa kwenye kikao hicho ambacho viongozi na watendaji hao walikuwa wakizungumzia mkakati wa mpango wa kuondoa umasikini mkoa wa Dodoma, Dk Mahenge anaeleza hali halisi ya mvua inayopatikana mkoani humo.

Kikao hicho cha hivi karibuni, kilikutanisha wakuu wa wilaya za mkoa wa Dodoma, wakurugenzi wa halmashauri, wataalamu wa kilimo na wenyeviti wa halmashauri kujadili mikakati ya kuondokana na umasikini. Kwa mujibu wa mkuu wa mkoa, mkoa wa Dodoma hupata mvua chache (milimita 400 mpaka milimita 600 kwa mwaka na hunyesha kwa wastani wa siku 60 kwa msimu wote kuanzia mwishoni mwa Novemba/ Desemba mpaka Machi.

Anasema yapo maeneo machache sana ambayo hupata mvua mpaka milimita 800. “Lakini bado hayaondoi sifa kubwa ya Dodoma ya kupata mvua ndogo kwa mwaka,” anasema Mahenge. “Wakulima wetu wakilima mazao yanayohitaji mvua zaidi, mazao yao yatakauka na hali hiyo hutokea mara kwa mara. Tumewahi kujiuliza kwa nini na sisi kama viongozi kwa kuwatumia wataalamu wetu tunachukua hatua gani?” alihoji mkuu wa mkoa.

Anaelezea: Dodoma naambiwa kuna ukame mpaka mtama unakauka. Lakini wataalamu wanasema Dodoma mtama utakauka pale utakapopandwa kwa kuchelewa. “Uzoefu uliopo ni kwamba wakulima wanapanda mahindi mara ya kwanza yanakauka, mara ya pili yanakauka na hata mara ya tatu kipindi hicho ni mwisho wa Februari na mwanzo wa Machi,” anasema.

Anasema baada ya wakulima kuona hali hiyo, ndipo huchukua mbegu za mtama na kupanda na kipindi hicho huwa imebaki mvua ya mwezi Machi tu ambayo kitaalamu hutumika kwa ajili ya uzalishaji na siyo ukuaji wa mimea. Mkuu wa mkoa anasema: “Uzoefu ni kwamba wakulima wameachwa walime kadri wanavyoona wao… hivyo nasema hatuwezi kuwaacha wakulima waamue wenyewe mazao ya kulima hata kama tunajua hawatalima mazao yanayofaa ambayo yatawapa manufaa,” anasema.

Dk Mahenge anasema mambo ya msingi ambayo wanakubaliana ni kuimarisha usimamizi na utoaji wa huduma za ugani kwa wakulima na wakulima kutumia huduma wanazopewa na maofisa ugani na kusimamia mazao stahiki ya hali ya Dodoma. Ofisa Kilimo wa mkoa wa Dodoma, Benard Abraham anasema wanajipanga kuhakikisha malengo yote yanatekelezeka.