George Weah akabiliwa na changamoto kibao Liberia

MWANASOKA wa zamani, George Weah amechaguliwa kuongoza Taifa la Liberia. Lakini je, atamudu changamoto nyingi zinazoikabili Taifa hilo? Hili ndilo swali watu wengi wanajiuliza.

Katika sehemu ambayo Jiji la Monrovia linaonekana vizuri ni mabaki ya iliyokuwa hoteli ya nyota tano – DUCOR. Hapo kuna sanamu ya rangi ya njano na nyeusi ya Joseph J Roberts, rais wa kwanza wa nchi hiyo, ikitazama jiji hilo.

Mwasisi wa taifa hilo angekuwa mwenye furaha kwa kile kilichotokea Liberia hivi karibuni – hatua kubwa kuelekea katika kubadilishana madaraka ya nchi kutoka kwa rais aliyechaguliwa kwenda kwa mwingine kwa amani.

Nje ya Tume ya Uchaguzi ya Liberia, umati ulikusanyika kushangilia kutangazwa kwamba George Opong Weah ameshinda uchaguzi wa marudio. Kijana mdogo aliyekuwa tumbo wazi, alionekana akitokwa na machozi.

Alikuwa kielelezo cha yale yaliyotokea. Msaidizi wa Rais huyo mteule alisema alimwaga chozi baada ya kusikia taarifa hizo za ushindi. Hakika kila mmoja anashangazwa na ushindi huu.

Lakini ushindi huu wa kishindo ungeweza hata kuwashangaza wafuasi wa mwanasoka huyo bora wa zamani wa Fifa duniani. Sasa, Weah anakabiliwa na mpambano wake mkali zaidi.

Anaweza kuwa mahiri wa kufunga mabao uwanjani, lakini amekuwa seneta kwa miaka mitatu tu. Licha ya hilo, hajafanya siasa na kupimwa kama mwanasiasa. Labda kama angeruhusiwa kuwania urais wa Chama cha Soka cha Liberia wakati alipotaka kiti hicho mwaka 2004, kingekuwa kitu cha kumfanyia tathimini uwezo wake wa kiuongozi.

Na sasa ndiye ataiongoza Liberia, nchi ambayo ilijikuta katika vita ya wenyewe kwa wenyewe kwa miaka 17, ikianzishwa na Charles Taylor miaka 28 iliyopita, siku ya mkesha wa Sikukuu ya Krismasi mwaka 1989.

Baadaye Taylor alikuwa rais, kabla ya kulazimishwa kuachia ngazi kutokana na shinikizo la kimataifa kwa sababu ya uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binadamu alioufanya kwa nchi jirani ya Sierra Leone.

Kwa sasa anatumikia kifungo cha miaka 50 katika jela moja nchini Uingereza, baada ya kuhukumiwa kwa makosa hayo. Kwa hiyo inashangaza kuona kwamba Makamu wa Rais wa Weah, atakuwa Jewel Howard Taylor, mke wa zamani wa mbabe huyo wa vita aliyeko kifungoni.

Lakini wakati uteuzi wake ukionekana una utata, wafuasi wa seneta huyo wanasema anazo sifa na yuko vizuri kitaaluma na anao uzoefu kwa jukumu hilo jipya. Kwa hakika, George Weah amefanya mbinu nyingi za kisiasa kufika alipofika leo.

Siyo tu na mkewe Taylor, lakini pia na mbabe wa zamani wa vita, Prince Johnson ambaye alimuua kwa mapanga rais mwingine, Samuel Kayan Doe. Kuridhisha matakwa ya hao, itakuwa jambo muhimu kwa rais mpya.

Zaidi, baada ya kupata asilimia 38 ya kura katika raundi ya kwanza, alihitaji kufanya ‘dili’ ili kujitengeneza ushindi – na siyo mpinzani wake – chaguo kwa wagombea wengine 18 ambao hawakuweza kuingia katika marudio.

Hata mgombea mwenza wa Charles Brumskine ambaye alikuwa wa tatu na aliyekimbilia mahakamani kuzuia uchaguzi wa marudio, alimuunga mkono Weah, akienda kinyume cha msimamo wa kiongozi wake.

Haijawa wazi nani atateuliwa kwa nafasi ipi, lakini vyanzo vya habari vya kuaminika zinaeleza kuwa walioshirikiana naye wana nafasi kubwa zaidi ya kuula. Sababu nyingine ya ushindi wa Weah inaweza kuwa ni kwa sababu ya mtu aliyeshindana naye.

Kwa miaka 12, Joseph Boakai amekuwa Makamu wa Rais wa Liberia. Na kwa muongo mmoja, Boakai mwenye umri wa miaka 73, alikuwa mtumishi wa umma. Yeye na wafuasi wake waliuelezea uzoefu wake kuwa rasilimali kubwa.

Wanaompinga walieleza kuwa umri ulikuwa ni kikwazo kwake. Kama hiyo ilikuwa sababu au la, kamwe haiko wazi. Hata hivyo, yeye na Rais Ellen Johnson- Sirleaf wamesimamia kipindi cha utulivu wa nchi hiyo baada ya miongo kadhaa ya vita na machafuko makubwa.

Lakini Weah anachukua urais wa Liberia katika nchi ambayo rushwa inaaminika ni kubwa mno, umaskini umetamalaki na uchumi wake ni dhaifu. Kubadili hali ya uchumi wa nchi yenye maliasili kubwa zikiwamo uzalishaji mkubwa wa mpira, vyuma na uwezekano wa kuwapo mafuta, ni jambo la msingi.

Na kwa hayo, kutoa ajira hasa kwa vijana ambao ni sehemu kubwa ya idadi ya watu wa Liberia. Hili litahitaji sera zenye kufikirika vyema na misaada ya kigeni. Mkuu wa waangalizi wa kimataifa kutoka Jumuiya ya Nchi za Afrika Magharibi, Ecowas, aliiomba dunia iisaidie Liberia.

Rais wa zamani wa Ghana, John Mahama aliitaka “jumuiya ya kimataifa kuisaidia nchi hiyo na misaada zaidi.” Liberia imekuwa nchi ya mfano katika Bara la Afrika. Ikiwa jamhuri huru, imetoa rais wa kwanza mwanamke wa kuchaguliwa, mshindi wa tuzo ya binafsi ya mwanasoka duniani, na sasa rais wa kwanza mwanasoka wa zamani.

Kijana aliyekuwa akitoa chozi anahitaji kazi ili kufuta machozi yake. Sanamu ndefu ya Rais Roberts inaendelea kuitazamwa, Waliberia watajiuliza wenyewe kama furaha waliyokuwa nayo kwa ushindi wa Weah ilistahili.