Tanzania kuvuna ilichopanda Michezo ya Madola 2018

TANZANIA ina medali 21 tangu imeanza kushiriki Michezo ya Jumuiya ya Madola mwaka 1966, ikiwa ni miaka 52 tangu iliposhiriki kwa mara ya kwanza.

Mchezo wa riadha ndiyo unaongoza kwa Tanzania kutwaa medali nyingi baada ya kukomba jumla ya medali 15 za aina tofauti tofauti, huku ndondi ikitwaa medali sita kutoka katika michezo hiyo.

MAANDALIZI YA MICHEZO

Tayari maandalizi ya ushiriki wa Michezo ya Jumuiya ya Madola kwa mwaka huu yameanza, lakini timu za Tanzania ukiondoa ile ya mpira wa meza, bado hazijaanza kambi ya kudumu.

Michezo ya mwaka huu itafanyika Gold Coast, Australia kuanzia Aprili 4 hadi 15 na Tanzania inatarajia kupeleka timu za riadha, ngumi, kuogelea na mpira wa meza. Timu ya mpira wa meza iko kambini nchini China, ambako inajifua kwa ajili ya maandalizi ya michezo hiyo inayofanyika kila baada ya miaka minne.

Hata hivyo, nchi nyingine zimeanza maandalizi muda mrefu mara baada ya kumalizika kwa michezo iliyopita iliyofanyika Glasgow, Scotland mwaka 2014. Kiujumla maandalizi ya timu zetu kwa ajili ya Michezo ya Jumuiya ya Madola 2018, siyo mazuri na hatuna uhakika kama wachezaji wetu watatuletea medali yoyote.

TIMU YA TAIFA YA NDONDI

Ndondi ndiyo mchezo wa kwanza kuiletea Tanzania medali kutoka katika Michezo ya Jumuiya ya Madola wakati bondia Titus Simba (sasa marehemu) alipotwaa medali ya fedha mwaka 1970.

Bondia huyo wakati wa uhai wake alikuwa mahiri na hilo lilidhihirisha katika michezo hiyo iliyofanyika Edinburg, Scotland. Tanzania ilipata medali zingine za ndondi kupitia kwa akina Willy Isangura aliyepata medali ya shaba michezo hiyo ilipofanyikia Brisbane, Australia 1982.

Michezo iliyofuata ilifanyika mwaka 1990 Auckland, New Zealand, ambapo katika ngumi Haji Ally pamoja na Bakari Mwambeya walipata medali za fedha na shaba katika uzito tofauti.

Mwaka 1994 michezo hiyo ilifanyikia Vancouver, Canada, ambapo bondia Hassan Matumla alitwaa medali ya fedha katika michezo hiyo. Tanzania ilitwaa medali yake ya kwanza ya dhahabu katika ndondi pale bondia Yombayomba alipotwaa medali katika michezo ya 1998 ilipofanyikia Kuala Lumpur, Malaysia.

Na huo ndiyo ulikuwa mwisho wa mabondia wa Tanzania kutwaa medali katika michezo hiyo ambapo miaka 2002, 2006, 2010 ma 2014 hakuna bondia aliyerudi na medali yoyote.

GOLD COAST 2018

Katika Michezo ya Jumuiya ya Madola mwaka huu, Tanzania inatarajia kupeleka tena timu ya ndondi lakini maandalizi yake bado yanasuasua kwani hadi sasa timu haiku katika kambi ya kudumu.

Mabondia na makocha wa timu hiyo wanalalamikia timu kutokuwa na vifaa, hawana mahitaji mengine muhimu, kitu ambacho kinarudisha nyuma mazoezi yao. Pamoja na viongozi wa Shirikisho la Ndondi Tanzania (TBF) kusisitiza kuwa mazoezi yanakwenda vizuri, ukweli unabaki pale pale kuwa timu hiyo haina maandalizi ya kutosha.

Timu hiyo iliwahi kujipima dhidi ya mabondia wa klabu za hapa nchini kama ngome, JKT na Magereza badala ya kujipima na mabondia kutoka nje, ambao wangekuwa kipimo tosha.

Uongozi wa TBF unadai kuwa umeandaa mashindano ya kimataifa mjini Dodoma, ambapo yatajulikana kama Mabingwa wa Mabingwa, na wamezialika timu kutoka nje. Hata hivyo, hakuna uhakika kama mashindano hayo yatakuwa kweli ya kimataifa, kwani ni vigumu kwa kipindi hiki kuandaa mashindano ya kimataifa alafu zikaja nchi nyingi, kwani ziko katika maandalizi ya Michezo ya Jumuiya ya Madola.

Uongozi wa TBF katika kipindi chao chote cha miaka minne umeshindwa kabisa kupeleka timu kuanzia mashindano ya Afrika, Kanda na hata ya Dunia. Uongozi huo hadi sasa unashindwa kuiweka timu ya ndondi katika kambi ya kudumu na badala yake unavizia kambi ya TOC, ambayo mara nyingi huwa mwezi mmoja kabla ya michezo husika na wakati mwingine haipo kabisa kama hakuna fedha.

BFT wanashindwa nini kuiweka timu yao kambini wakati vyama au mashirikisho mengine yameweza kama Riadha (RT) na vingine? Tukubali tusikubali, matumaini ya timu ya ndondi kurudi na medali ni madogo sana, tofauti na ahadi kubwa zinazotolewa na viongozi wao kuwa mabondia wanaendelea vizuri na mazoezi.

TIMU YA TAIFA RIADHA

Timu ya taifa ya riadha inatarajia kuingia katika kambi ya kudumu West Kilimanjaro wilayani Siha mkoani Kilimanjaro. Pamoja na kutoanza kambi ya kudumu, lakini tayari wanariadha wake wako katika mazoezi makali kwa ajili ya mashindano mbalimbali ikiwemo Michezo ya Jumuiya ya Madola 2018.

Katibu Mkuu wa RT, Wilhelm Gidabuday amesema kuwa timu hiyo itaingia kambini kuanzia Januari 20 West Kilimanjaro. Timu hiyo ndiyo angalau ina matumaini ya kurudi na medali kutokana na maandalizi yake, licha ya kutokuwa na nyota Alphonce Simbu, ambaye atashiriki London Marathon itakayofanyika Aprili 22. Wanariadha wengine walioko katika maandalizi hayo wanaendelea vizuri na tayari wengi wao wameshafikia viwango vya kushiriki michezo hiyo.

MEDALI ZA RIADHA MADOLA

Tanzania ilianza kupata medali ya kwanza katika Michezo ya Jumuiya ya Madola mwaka 1974, ambapo ilipata medali mbili kutoka kwa Filbert Bayi na Clever Kamanya huko Christchurch, New Zealand.

Michezo hiyo pia ilikuwa na historia ya aina yake kwa Tanzania kwani Bayi alivunja rekodi ya dunia katika mbio za meta 1500. Mbali na kuweka rekodi ya dunia, pia mwanariadha huyo aliweka rekodi ya Jumuiya ya Madola, ambayo inadumu hadi sasa wakati tukielekea katika Michezo hiyo ya Gold Coast. Sasa ni zaidi ya miaka 40 rekodi ya Bayi katika Michezo ya Jumuiya ya Madola haijavunjwa na haitarajiwi kuvunjwa katika michezo hiyo ya Gold Coast.

MEDALI ZINGINE ZA MADOLA

Tanzania katika Michezo ya Jumuiya ya Madola ilipata medali kupitia kwa wanariadha, Gidamis Shahanga, Bayi, Zakaria Barie, Juma Ikangaa, Simon Robert (sasa marehemu). Wanariadha wengine walioliletea taifa medali kutoka Michezo ya Jumuiya ya Madola ni pamoja na Simon Mrashani, Gerway Suja, Francis Naali, John Yuda, Samson Nyonyi, Fabiano Joseph na Zakaria Malekwa.

MATOKEO YA 2018

Watanzania tusitegemee matokea mazuri sana kutoka Gold Coast, kwani huko sana sana tutavuna tulichopanda katika maandalizi ya timu zetu.