Rwanda inavyodhibiti madhara ya taka za vifaa vya umeme

SERIKALI ya Rwanda imewekeza dola za Marekani milioni 1.5 katika mradi wa kusimamia na kudhibiti taka zitokanazo na vifaa vya umeme (e-waste) ili kuzifanya kuwa na manufaa badala ya madhara.

Kituo hicho kiko katika wilaya ya Bugesera, Jimbo la Mashariki, kilomita 35 kutoka katika jiji la Kigali. Udhibiti wa taka zitokanazo na vifaa vya umeme ni tatizo linalokua kwa haraka duniani.

Nchi nyingi zinazoendelea, ambazo pia huonekana kuwa tayari kugeuzwa dampo la kutupia taka hizo, zimekuwa zikikubali kuviagiza vifaa hivyo kutoka nje kwa bei karibu na bure na hazionekani kuwa na mipango inayoeleweka ya namna ya kusimamia na kudhibiti athari za taka hizo hatari baada ya matumizi yake kuisha.

Rwanda, hata hivyo, imesimamisha uagizaji wa kompyuta zilizotumika (mitumba) kutoka nje. Mpango uliopo ni kuchunguza bidhaa hizo za kizamani zilizopo sasa na kuchambua vifaa ambavyo bado vina thamani ili kuvihuisha (recycling) kwa matumizi mengine ili kuzuia athari zitokanazo na mitumba hiyo.

Rwanda imepania kukamilisha ndoto mbili kubwa ambazo; mosi ni kuwa nchi ya kwanza isiyokuwa na uchafuzi wa mazingira na pili, kuwa kitovu cha maendeleo ya teknolojia katika eneo hili la Afrika Mashariki.

Wakati wa mahojiano, Olivier Mbera, meneja wa mradi huo, anasema mkakati wao unaogharimu dola za Marekani milioni 1.5 unatoa ufumbuzi wa “mwisho mzuri wa maisha” kwa taka zitokanazo na vifaa vya umeme ili kuzuia athari zake mbaya kwa afya za watu na mazingira kwa ujumla.

Mbera anasema, mpango huo mpya utasaidia kuhifadhi rasilimali za asili, kuzalisha ajira zinazohusu mazingira bora kwa wananchi, na kupunguza athari mbaya zinazotokana na vifaa hivyo kwa afya za binadamu na mazingira. Anasema, katika awamu ya kwanza ya mradi huo, ajira zipatazo 1,000 zitatengenezwa.

Kwa mujibu wa Mbera, Rwanda ilifanya uchunguzi kuhusu taka zitokanazo na vifaa vya umeme kama vile seti za luninga, mabirika ya kuchemshia maji, friji, kompyuta na bidhaa nyingine za aina hiyo zikuwa zimezagaa kila mahali na hivyo kuwa vigumu kuzikusanya na kuzihuisha tena.

Kulingana na ripoti ya Umoja wa Mataifa, mwaka juzi 2016, tani 44.7 za taka zitokanazo na vifaa vya umeme zilizalishwa duniani kote. Lakini Mbera anasema ndani ya nchi kama Rwanda, kama utarundika rundo la taka za bidhaa zitokanazo na umeme zilizokuwa zinazalishwa kila mwaka ni sawa na ukubwa wa jengo lenye ghorofa zaidi ya 20 endapo zitarundikwa pamoja.

Anasema Rwanda pekee inaweza kuzalisha kati ya tani 10,000 hadi 15,000 za taka zitokanazo na vifaa vya umeme kwa mwaka na kwamba mradi wao una uwezo wa kushughulikia tani 7,000 za taka hizo kwa mwaka.

Katika kipindi cha miezi sita ya majaribio, kituo hicho kimekusanya tani 120 za taka zitokanazo na vifaa vya umeme; kuhuisha upya kompyuta 400, na kudhibiti tani 60 za carbon dioxide kati ya tani 279 huku zilizobaki pia madhara yake yakipunguzwa.

Mbera anasema kuwa hapo awali, serikali ilitumia maghala ili kutunzia taka zitokanazo na vifaa vya umeme katika kuepusha athari zake kwa watu na mazingira. “Lakini sehemu kubwa ya taka hizi zilitelekezwa kwenye madampo ya taka na hivyo kufukiwa ardhini ambamo zinaathiri maji yanayopita chini ya ardhi na taka zilizowazi kuendelea kuathiri anga lilaozungika eneo husika,” anasema.

Anasema Rwanda pia imeanzisha kampeni ya kuelimisha jamii kuhusu madhara ya kuishi karibu au kuzungukwa na taka zitokakazo na vifaa vitumiavyo umeme. Meneja mradi huyo anafafanua kuwa kituo hicho pia kinatumia taka hizo ili kupata metali au madini muhimu.

Anasema aina zaidi ya 15 ya vifaa vya umeme vimekuwa vikivunjwa na kuhuishwa upya ili kupata bidhaa zingine nzuri au kuondolewa kabisa katika mazingira. Bandari ya Dar es Salaam.

“Kituo hiki kilichoko Bugesera ni cha pili cha aina yake Afrika, na kina vifaa vya kisasa kiasi kwamba kinaweza kuhuisha tani 7,000 za taka zitokanazo na vifaa vya umeme kwa mwaka.

Usimamizi endelevu wa taka zitokanazo na vifaa vya umeme ni suala muhimu katika kuboresha mazingira,” Mbera anasema. Kituo kingine cha aina hiyo kwa sasa kiko Afrika Kusini.

KINAVYOFANYA KAZI

Wakati taka zinapoletwa, huchambuliwa, hujaribiwa, kisha kuachanishwa vipande vipande. Kompyuta zenye matatizo kidogo na zinazoweza kurekebishwa na hivyo kurudi kufanya kazi haziharibiwi.

Badala yake, zinarekebishwa na kuwekewa vifaa vinavyopungua na kisha kupelekwa mashuleni. Kuna makubaliano kati ya kituo hicho cha kuchakata taka zitokanazo na vifaa vya umeme na wizara ya elimu ili kupokea kompyuta iliyofanyiwa ukarabati na kurejea kufanya kazi katika shule za msingi.

Rwanda ina sera ya kila mwanafunzi mmoja kuwa na kompyuta moja inayolenga kuimarisha mafunzo ya Teknolojia ya Mawasiliano (Tehama) katika shule za msingi. Taka zitokanazo na vifaa vya umeme mara zote siyo mali isiyofaa kabisa.

Vifaa vinavyookena kuwa bado na thamani vilivyo ndani ya taka hizo hutolewa kwa ajili ya matumizi mengine. Mbera anafafanua kwamba baadhi ya vitu wanavyopata kutoka kwenye taka hizo kwa ajili ya matumizi mengine ni pamoja na alumini, shaba na madini mengine ya thamani yaliyomo ndani ya vifaa hivyo.

Kituo hicho hakijaanza kuyeyusha metali zilizoko kwenye bodi mama za bidhaa hizo (circuit boards) na hivyo nyingi husafirishwa kwenda Japan ambako huuzwa kwa Dola 50,000 kwa tani.

Mfuko unaoendesha mradi huo wa Rwanda Green Fund, ulianzishwa ili kukabiliana na uharibifu wa mazingira na kudhibiti mabadiliko ya tabianchi. Mfuko unatoa fedha katika miradi ya umma na ya kibinafsi ambayo ina uwezekano wa kuleta mabadiliko chanya katika mazingira ukilenga kutekeleza mkakati wa Rwanda wa kujenga uchumi wenye nguvu, lakini ambao pia ni rafiki wa mazingira.

Halikadalika mfuko huo unatoa msaada wa kitaalamu ili kuhakikisha kunakuwa na mafanikio katika uwekezaji wowote unaofanywa na mfuko huo. Mnamo Aprili 2014, serikali ya Rwanda, kupitia Mfuko huo ilitenga dola milioni 1.5 ili kuanzisha mradi huo wa kuchakata na kudhibiti taka zitokanazo na vifaa vya umeme.

Mkakati huo unahusisha pia mfumo wa kitaifa wa kuchakata na kuhuisha taka na mpango wa nchi nzima wa kukusanya taka, kuzifumua na zile zinazofaa kutumika tena katika viwanda vya Rwanda au nje ya nchi.

KUTENGENEZA AJIRA

Kituo hicho kwa sasa kimeajiri watu 30 na idadi kadhaa ya wanafunzi wa vyuo mbvalimbali hupata nafasi ya kujifunza kwa vitendo katika mpango huo. Mara vituo 30 vya kukusanya taka zitokanazo na vifaa vya umeme vitakapoanzishwa katika kila wilaya nchini kote, ajira zaidi ya 1,000 zitapatikana.

KWA NINI AFRIKA?

Nchi nyingi katika bara hili hupokea mithili ya ‘zawadi’ kompyuta za kizamani, betri za simu zilizotumika, mafriji na majiko ya kupikia ya umeme kwa bei karibu na bure. Mnamo mwaka 1998, baadhi ya nchi za Afrika zilipitisha Mkataba wa Bamako uliokuwa unazuia uagizaji wa taka hatari (mitumba), ikiwa ni pamoja na kompyuta za kizamani, simu za mkononi na vifaa vingine vya umeme.

Licha ya makubaliano hayo, Afrika bado ni mpokeaji mkubwa wa vifaa vya umeme vilivyo karibu kabisa kumaliza muda wake wa kutumika kutoka nchi zenye viwanda.

MIPANGO YA BAADAYE

Kwa sasa, kituo cha Bugesera kinamilikiwa chote na serikali lakini mipango ya baadaye ni kuhusisha pia wawekezaji binafsi katika kukiendsha. Kwa sasa kituo kinafanyia kazi taka zitokanazo na vifaa vya umeme zinazozalishwa Rwanda pekee, lakini Mbera anasema wanatarajia baadaye kuanza kuagiza taka za aina hiyo kutoka katika maeneo mengine ya ukanda huu.

Anasema kuna mipango ya kujenga mtambo wa kuyeyusha na hatimaye kutumia madini yenye thamani yaliyomo kwenye taka hizo kwa ajili ya kuzalisha bidhaa zingine. Kituo cha Bugesera kimeonesha pia namna serikali ya Rwanda ilivyo makini katika kulinda afya ya wananchi wake kwa kuzingatia kuwa betri zinazotumika katika baadhi ya vifaa hivyo zina madini ya lead na zebaki ambayo ni hatari kwa maisha ya binadamu.

Makala haya yalitoka kwa mara ya kwanza Januari 10, 2018 katika gazeti la The Observer la Uganda