Dk Kiruswa alivyopitia milima, mabonde kupata ubunge Longido

“HII safari ya kuusaka ubunge wa jimbo la Longido ilikuwa ngumu sana kwani ilikuwa na vikwazo vya kila aina kwani familia yangu na baadhi ya wana Longido walisononeka, walisikitishwa na ilifika mahali walikata tamaa lakini walijikaza na kumtanguliza Mungu kwa kila jambo hatimaye tumeshinda.’’

Kauli hii ni ya Dk Stephen Lemomo aliyechaguliwa kuwa Mbunge wa Longido katika uchaguzi mdogo uliofanyika hivi karibuni. Msimamizi wa uchaguzi wa jimbo hilo, Juma Mhina alimtangaza kuwa mshindi kutokana na kura 41,258 sawa na asilimia 99.1 alizopata na kuwaacha mbali washindani wake wanane.

Dk Kiruswa anasema haikuwa kazi ndogo kupata ubunge huu kwani alitumia muda mwingi sana katika vyombo vya sheria kuusaka. Onesmo Ole Nangole ndiye aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo kwa tiketi ya Chadema aliyeshinda katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.

Hata hivyo, Dk Kiruswa alikwenda mahakamani kupinga ushindi na kufanikiwa hatimaye kukafanyika uchaguzi mdogo. Anasema mke wake, Agnes Kiruswa pamoja na ndugu, jamaa na marafiki walikuwa wakimwomba kuhakikisha wana Longido wanarudishiwa haki yao iliyokuwa imechukuliwa.

Anasema wakati walikata tamaa lakini yeye aliwaambia waendelee kumwomba Mungu ipo siku atafanikiwa. Dk Kiruswa anasema kesi ya uchaguzi iliyokuwa ikisikilizwa na Jaji Mfawidhi wa wakati huo wa Mahakama Kanda ya Bukoba, Jaji Silvangirwa Mwangesi ilichukua muda mrefu sana.

Hatimaye Juni 29 mwaka jana, Jaji Mwangesi alitoa hukumu iliyotengua ubunge wa Nangole akisema haukuwa huru na haki. Hata hivyo, Nangole hakukubaliana kwani alikata rufaa mahakama za juu mara tatu. “Lakini Mungu si Athumani hakuweza kufanikiwa kupata ushindi wowote,” anasema.

Kiruswa ambaye alizaliwa Februari 2, 1963 katika Kijiji cha Engarenaibor na kupata elimu ya msingi katika shule ya kijiji hicho mwaka 1979, anasema kilichopo mbele yake ni kuijenga Longido mpya kwa kasi.

Anasema ushindi huu uliotokana na uchaguzi wa Januari 13 mwaka huu unamwezesha kutumikia wananchi kwa miaka miwili ambayo hata hivyo anasema kisiasa ni michache. Anasema kuwa na mpango kazi wa muda mfupi wenye kuleta tija kwa wananchi wa jimbo hilo lenye changamoto nyingi za maendeleo ili aweze kukubalika tena katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2020.

Kwa mujibu wa Kiruswa, jambo la kwanza ni kuwaunganisha vijana wawe na umoja wa kuwawezesha kukubaliwa kukopeshwa na taasisi za fedha hatimaye wapate mtaji wa kuendesha shughuli za kiuchumi kama vile uendeshaji bodaboda.

Mbunge huyo aliyepata elimu ya kidato cha kwanza hadi cha sita mwaka 1986 katika sekondari katika seminari ya Oldonyosambu kabla ya kujiunga na Shahada ya kwanza ya Maendeleo ya Jamii Chuo Kikuu Cha Daystar nchini Kenya, anasema ni mtaalamu wa kubuni miradi ya maendeleo .

Huduma za jamii Akizungumzia changamoto za elimu,maji,afya na barabara, anasema kwa kushirikiana na viongozi wa juu serikalini, hana shaka kuwa changamoto hizo zitapata majawabu.

‘’Nilimtanguliza Mungu kwa kila jambo na hatimaye nimeweza kufanikiwa nilichokuwa nakitafuata,” anasema Kiruswa mwenye Shahada ya Uzamivu ya Mawasiliano ya Kimataifa na Maendeleo aliyopata katika chuo kikuu cha Regent cha Marekani mwaka 2000 hadi 2004.

Anawataka wana Longido wote kuweka pembeni itikadi zao na kuwa kitu kimoja katika kuleta maendeleo. Akielezea msukumo wa kugombea, Dk Kiruswa anasema alifanya utafiti wa kina kujua changamoto za wananchi wa jimbo hilo kwa kuzunguka kata zote 18 jimboni kwa gharama zake binafsi.

Baada ya kuzunguka miezi sita aliweza kufahamu changamoto zinazowakumba. ‘’Sikubahatisha kugombea ubunge nilikuwa najua changamoto za jimbo la Longido kinagaubaga na sijagombea ubunge kunijinufaisha kwani sina njaa ya namna hiyo katika utendaji wangu wote,” anasema.

Ufugaji Akizungumzia ufugaji, anasema wanaoendesha shughuli hiyo hususani jamii ya kimasai, wanapaswa kubadilika. Anasema elimu ni muhimu kutolewa kwao wafuge kisasa.

Anasema hilo linawezekana kwa kutenga maeneo ya malisho na kupanda nyasi za mifugo na baadhi ya wafugaji kuchunga au kulisha mifugo kwa wakati maalumu. Anaahidi pia kufanya jitihada za kuwataka wafugaji kuuza baadhi ya mifugo kwa ajili ya kujiendeleza, ikiwa ni pamoja na kuwa na nyumba za uhakika na kuwa na maendeleo yao binafsi na familia zao.

‘’Mimi ni mtoto wa mfugaji najua sifa ya mfugaji ya kuwa na mifugo mingi sana lakini hilo linaweza kuwaondoka kichwani taratibu kwa kuwaelimisha na wanaweza kunielewa nina maana gani.”

Akielezea wasifu wake, anasema ana uzoefu wa kazi,uongozi na utafiti kutokana na stashahada ya juu ya matumizi bora ya Ardhi na Maisha ya Watu aliyopata kutoka Chuo Kikuu cha London, mwaka 2004 hadi 2005.

Pia alipata uzoefu wa uongozi kwa kuwa Mkurugenzi wa African Wildlife Foundation Arusha mwaka 2006 hadi mwaka 2011. Nyadhifa nyingine alizowahi kushika na mwaka katika ni; Mratibu wa Maendeleo ya Jamii na Mawasiliano wa World Vision Arusha.

Amewahi kuwa Mhadhiri chuo cha Daystar na chuo cha Regent mwaka 2012 hadi mwaka 2015. Hadi mwishoni mwa mwaka jana, alikuwa Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo cha Kimataifa cha Maendeleo na Uongozi kilichoko Usa River Arusha kinachojulikana kama Ms-TCDC.

Utafiti Aliwahi kufanya utafiti sehemu mbali nchini na nje ya nchi ikiwa ni pamoja Taasisi ya Kimataifa ya Utafiti wa Mifugo cha nchini Kenya (ILRI) mwaka 2004 hadi 2006 . Alifanya utafiti ukimwi miongoni mwa wanajeshi katika nchi zilizo Kusini mwa Jangwa la Sahara2002 hadi 2003.

Mwingine ni utafiti katika Shirika la Kazi Duniani (ILO) juu ya uzalishaji wa sekta zisizo rasmi mwaka 2005. Mkewe Kiruswa Mke wa Dk Kiruswa, Agnes anaelezea ushindi wa mumewe kuwa ni faraja kubwa kwa familia, ndugu na jamaa.

Anasema mumewe hakuwa na amani kwani tangu kuanza kwa kesi, alikuwa akiwaambia wafunge na kuomba ashinde kesi. Vivyo hivyo kwenye uchaguzi ili aweze kushinda. ‘’Mume wangu alikuwa akisema kuwa tunapaswa kufunga na kumwomba Mungu ili tushinde kesi na tulishinda na baada ya kuanza kampeni alisema tena hivyo hivyo na sote tulikuwa tukifanya hivyo na Mungu ametujibu. Kweli Mungu ni mwema kwa jambo la heri,’’ anasema Agnes.

Viongozi wa mila Viongozi wa mila ya jamii ya kimasai maarufu kwa jina la Laigwanani hawakuwa mbali katika kumwombea Dk Kiruswa kushinda uchaguzi huo. Walitabiri ushindi juu yake na baada ya ushindi walimkabidhi kushinda na kumkabidhi rungu kama ishara ya kiongozi wa jamii hiyo kwa wana Longido wote.

Wakiwa katika ofisi ya CCM Longido, walianza kwa kuomba na kumkabidhi rungu hilo ambalo ni ishara kuwa ni kiongozi wa mila wa jimbo hilo . Francis Ikayo ni mwana CCM ambaye anasimulia maisha wakati wa kipindi cha kesi akisema walikuwa wakimsindikiza mahakamani huku wakishindia mihogo.

Ikayo anasema, “kuwa Mungu kamwe hawezi kumtupa mja wake kwani mwanadamu huchelewesha tu riziki za watu lakini Mungu husimamia.” Shahidi aliyekatwa mapanga Isaya Karakakara ni mwanachama mwingine ambaye anasema alikuwa miongoni mwa waliotoa ushahidi.

Anasema kabla ya kwenda kutoa ushahidi, alikatwa mapanga mwili mzima ili kumzuia asiende mahakamani lakini alipopona alikwenda . ‘’Nimeteseka sana na hii kesi na nimeteseka na sana na huu uchaguzi lakini namshukuru Mungu amelipa na leo napata furaha kwa Kiruswa kuwa mbunge,’’alisema Karakara.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM wa wilaya ya Longido, Joseph Ole Sadira anasema ushindi uliopatikana katika jimbo hilo ni furaha kwa wale wote wapenda maendeleo jimboni.

‘’Mungu alisimama na Dk Kiruswa tangu mwaka 2015 na wenye hila sasa wameshikwa na aibu kwa kuwa Mungu alikuwa na mgombea wa CCM, ‘’anasema. Naye Mwenyekiti wa wazazi wa wilaya hiyo, Daniel Sadala anasema kila jambo lina wakati wake .

“Mungu alisimama kuhakikisha Kiruswa anakuwa Mbunge wa Longido.” Sadala anasema kwa sasa wana CCM wote Longido na nje ya Longido na hata wapinzani wanaomfahamu, wanayo furaha kubwa kwamba jimbo limepata mtu makini wa kuliongoza.