Serengeti Boys kuweka historia mpya Cecafa

MICHUANO ya Baraza la Soka Kusini mwa Afrika (Cecafa) kwa vijana chini ya umri wa miaka 17 inatarajiwa kutimua vumbi kuanzia Aprili Mosi mwaka huu nchini Burundi.

Vijana wengi waliopo kambini kwa muda mrefu ni wale wenye umri chini ya miaka 16. Lakini hiyo haisumbui baada ya Kocha wa timu ya taifa ya vijana, Serengei Boys, Oscar Mirambo kusema kuwa ni muhimu kushiriki bila kujali umri ili kupata uzoefu.

Gazeti hili lilifanya mazungumzo hivi karibuni na Kocha Mirambo kuelezea mikakati yao, changamoto na nafasi ya vijana hao kuelekea kwenye michuano ya Cecafa. Anasema michuano hiyo imekuja wakati muafaka na wanaisubiri kwa hamu kubwa kuitumia kutengeneza kikosi cha vijana chini ya umri wa miaka 17 kitakachoshiriki fainali za Mataifa Afrika (Afcon 2019).

Tanzania itakuwa mwenyeji wa michuano hiyo mikubwa hivyo, wanatengeneza kikosi kipana kitakacholeta ushindani wa hali ya juu na ikiwezekana kubakiza ubingwa. Anasema wanataka kutumia Cecafa kujitathmini kiwango chao lakini pia, wakijipa matumaini mapya kuwa ni lazima wakacheze kiushindani na kuchukua Kombe.

Licha ya kuwa na vijana wengi ni wadogo zaidi kiumri, anasema ni fursa ya kipekee kuitumia katika kutengeneza historia nyingine. “Tuna vijana wengi wadogo wenye vipaji, tumethibitisha kushiriki Cecafa tukiamini ni sehemu muhimu kwetu kujipima uwezo wetu, na kuangalia namna ya kujipanga zaidi tukielekea kwenye Afcon,” anasema.

Anasema baada ya michuano hiyo mikubwa ukanda huu watakuwa wamejipima kwa kiasi chake, ingawa wanatarajia kuendelea kujiimarisha kwa kuomba mechi tofauti kutoka katika nchi zilizoendelea kisoka.

“Ni lazima tuendelee na maandalizi makubwa kwani tutakapotoka Cecafa na kujitambua tupo katika nafasi gani, tutazidi kujipanga kwa kadiri siku zinavyokwenda hakika tutakuwa tumepata majibu,” anasema.

Harakati za kuwezesha Tanzania kucheza fainali za vijana chini ya umri wa miaka 17 zilianza kuhamasishwa tangu misimu iliyopita chini ya viongozi kadhaa waliopita wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).

Licha ya kufanya promosheni kubwa kwa vijana hasa mwaka jana hata hivyo, walifanikiwa kushiriki fainali zilizopita ingawa waliishia hatua ya makundi na yale malengo ya kufika fainali yalikwama.

Lakini ipo nafasi mwakani ya kudhihirisha ubora tena wakiwa nyumbani. Ni ukweli usiopingika Watanzania wanataka kuona mapinduzi ya kufanya vizuri katika michuano hiyo mikubwa.

Na mchakato wa kuyafikia mafanikio hayo tayari ulianza tangu msimu uliopita ambapo waliitwa vijana wengi na kucheza mechi kadhaa za kirafiki ili kuchuja na kubaki walio bora wa kupeperusha vyema bendera ya Tanzania.

Kocha Mirambo anasema kwa sasa kuna vijana 34 wanaendelea na kambi ya mwisho ya kufanya mchujo kubakiza 30 ambao wanatarajiwa kwenda Burundi kwenye Cecafa kwa maandalizi ya Afcon.

Anasema waliitwa zaidi ya vijana 50 na tayari walikuwa wakipunguza kila wakati kulingana na mechi kadhaa za ndani, walikuwa wakicheza dhidi ya klabu mbalimbali za Ligi Kuu na timu za madaraja ya chini na kutumia kama kipimo dhidi ya wale waliowahitaji. Alibainisha wengi wana vipaji lakini hawawezi kubaki wote ni lazima kufanya mchujo na kubaki wachache kwani wanazidiana kulingana na nafasi wanazohitaji.

KINACHOMPA JEURI

Anasema Serengeti ya msimu huu siyo ya kuchezea ni pita mbali, akimaanisha ubora wa wachezaji waliopo huwezi kulinganisha na waliopita, kwani waliopo sasa ni zaidi ya wale ni kama mara mbili yake.

“Kwa kweli Serengeti ya sasa imetuumiza kichwa katika uchaguzi wa wachezaji, kila unayemuona ni mzuri kiasi kwamba unapata shida umchague nani na umwache nani, wengi ni wazuri,” anasema.

Mirambo anasema msimu huu wamechagua kwa makini tofauti na njia iliyotumika msimu uliopita, ndiyo maana imekuwa ni kazi kubwa kuchuja. Anasema anakiamini kikosi alichonacho kina uwezo wa kufanya mapinduzi katika ukanda huu wa Afrika Mashariki.

Sababu ni kwa vile eti, msimu uliopita walifanikiwa kufanya hivyo, kwa kuwa ndio timu pekee ya ukanda huu iliyofikia hatua ya kucheza makundi katika michuano ya Afcon. “Bado sisi ni bora upande wa vijana na hata mwaka huu tutakuwa hivyo, kulingana na wachezaji wazuri tulionao, lazima tukiendeleze kuletea taifa heshima kubwa,” anasema.

Michuano hiyo ya Cecafa inatarajiwa kushirikisha nchi za Kenya, Uganda, Burundi, Rwanda, Sudan na kwingine ambako wataalikwa. Kabla ya kuelekea kwenda kwenye michuano hiyo anasema ni lazima wapate mechi za kirafiki za kujiandaa na kuwaondoa wachezaji kwenye uoga wa kushiriki mashindano makubwa.

Mchezo huo utafanyika kambi ijayo ya maandalizi hayo kwani hivi karibuni walihitaji mchezo wa kimataifa ikashindikana. “Tutafurahi zaidi iwapo tutatafutiwa hata zaidi ya mechi moja kwasababu lengo letu ni kujipanga na kukiandaa kikosi chetu kwenda kushindana na siyo kushiriki kwasababu ni wadogo,” anasema.

Anasema kwa sababu wanatengeneza timu ya Afcon michuano mingi itawasaidia kujiimarisha na kukaa mguu sawa kueleeka huko. CHANGAMOTO ZILIZOPO Changamoto ya kwanza anasema ipo katika uteuzi wa kikosi cha kwanza.

Kwa sababu kila wanayemuangalia ni bora, kwani hupata wakati mgumu wa kufikiria nani aanze na nani kubaki benchi. “Unapokuwa na wachezaji watatu au zaidi kwenye nafasi moja, uwezo hautofautiani ni kazi kubwa,” anasema na kuongeza kuwa ndiyo maana huwa wanawaeleza wachezaji hao waendelee kuonyesha ushindani.

Anasema wakionyesha ushindani kazi kubwa itabaki kwao kama benchi la ufundi kuendelea kutazama ni nani kuanza kikosi cha kwanza na nani kubaki. Kingine anasema wachezaji wengi ni umri chini ya miaka 16 na bado wapo shuleni.

Kuna wakati wanahitajika shule na ili kuhakikisha hawakosi vipindi inawalazimu kuwatafuta walimu kuja kuwafundisha kambini wasipitwe na masomo. “Utakuta muda tunaowahitaji kambini wanatakiwa kuwa shule na ili wasikose vipindi tumekuwa tukiwatafuta walimu kuja kuwafundisha wakiwa huku kuenda sambamba na wenzao,” anasema.

USUMBUFU WA KLABU

Zipo klabu kadhaa hapa nchini zimeanza kuwatolea macho vijana hao zikionesha nia ya kuwahitaji katika vikosi vya vijana. Kocha huyo anasema kuna klabu ambazo zimefika pale lakini hawezi kusema ni zipi ni kweli zimeonesha nia dhidi ya baadhi ya wachezaji.

“Tunachotaka kuangalia siyo uwezo binafsi wa wachezaji uwanjani, pia ulezi, tunaangalia klabu bora ambazo zinathamini programu za vijana, zinatoa mafunzo bora, zina makocha wazuri ndipo ambapo na sisi tunawashauri kwenda huko kwa manufaa yao ya baadaye,” anasema.

Pia, anasema wanaangalia timu itakayowapa nafasi vijana kucheza siyo aende ilimradi tu, na kwenda kukaa benchi mpaka anapoteza kipaji chake. Siyo mara ya kwanza kwa timu kuwanyemelea wachezaji hao vijana, tayari kuna baadhi ya vijana kutoka Serengeti Boys iliyopita walijiunga na timu mbalimbali zinazocheza Ligi Kuu na nyingine Ligi Daraja la Kwanza.

Kuna vijana wanaonekana kwenye timu kubwa kama Ramadhan Kabwili, Yohana Mkomola (Yanga), Nashon Naftali (JKT Ruvu) na wamekuwa wakionesha kiwango kizuri. Inawezekana wapo baadhi ya wengine kwenye timu nyingine bado hawajapata nafasi ya kuonekana wakicheza.

Anasema baadhi ya wachezaji walipata ushauri kutoka kwenye benchi lao la ufundi na wengine walienda wenyewe bila kuomba ushauri na wanachokiona ni faida na hasara za kushauriwa au kutoshauriwa.

ANACHOKIAMINI KOCHA

Anasema mchezaji mzuri ni yule aliyepata mazoezi mazuri na siyo kipaji kipekee ambacho kinaweza kumbeba mtu. “Ukipata nafasi ya kuandaliwa katika mazoezi na ukapata mechi kama mchezaji mdogo inamjenga na kumfanya aonekane ni bora, hata kama ana kipaji kikubwa cha aina gani kama hafanyi mazoezi na kupata mechi za ushindani hauwezi kufika mbali,” anasema.

Ili waendelee kuwa wachezaji na wakaweza kushindana inategemea kama wanapata mazoezi, muda wa kucheza na mechi za ushindani. Kocha huyo anasema jambo muhimu katika kuelekea kwenye mafanikio ya kufanya vizuri Cecafa na hatimaye Afcon kunahitajika ushirikiano kwa wachezaji, benchi la ufundi na viongozi wa TFF. Pia, uhamasishaji wa wadau kuichangia timu hiyo unahitajika kuanzia sasa ili kuwa na maandalizi mazuri na siyo kusubiri dakika za mwisho za lawam