Hatari ya uzazi katika umri mdogo

MIONGONI mwa mambo ambayo Johari hawezi kuyasahahu maishani mwake ni uzazi wake wa kwanza, ambao ulisababisha aongezewe chupa tano za damu baada ya kujifungua.

Johari (siyo jina lake halisi), mkazi wa Kilwa, mkoani Lindi alipata ujauzito akiwa na umri wa miaka 15 na kujifungua mwaka mmoja baadaye (akiwa na miaka 16). “Nilinusurika maisha yangu kupotea wakati nikiwa mjauzito na pia wakati wa kujifungua,” anasimulia binti huyo ambaye sasa ana umri wa miaka 17 akiendelea kumlea mtoto wake mdogo.

Johari anasimulia jinsi alivyolazimika kuhamishwa kutoka Kilwa Kisiwani kwenda Hospitali ya Wilaya ya Kilwa kwani ilikuwa lazima akajifungulie katika hospitali kubwa ili kunusuru maisha yake.

“Nilitolewa Kilwa Kisiwani baada ya kuonekana kuwa kutokana na afya yangu, natakiwa kujifungua katika hospitali kubwa. Nilikuwa na tatizo la upungufu wa damu toka nilipokuwa mjamzito.

Nililazwa mara kwa mara na kuongezewa damu,” anasema Anaongeza: “Lakini wakati mwingine nilielekezwa na manesi kula mboga za majani ili kuongeza damu na pia nilipewa na dawa za kuongeza damu”.

Kwa mujibu wa binti huyu, baada ya kurejea nyumbani, bado afya yake haikuwa nzuri hivyo aliendelea kula mbogamboga na vitu vingine vya asili ili kumwongezea damu kama alivyoelekezwa na wahudumu wa hospitali.

Anasema hospitalini, wauguzi walimueleza kuwa matatizo aliyoyapata yanatokana na kupata ujauzito katika umri mdogo, kwani mwili haukuwa umejiandaa vya kutosha kupata mtoto. Johari anakiri mwenyewe kuwa hakufuata maelekezo kwa usahihi, hasa matumizi ya dawa za kuongeza damu ambazo alitakiwa kumeza kila siku.

“Kwa kweli nilipata shida sana kujifungua, niliona kama napoteza maisha lakini Mungu alinisaidia afya yangu baadaye ikaimarika,” anasimulia Johari. Anawageukia wenziwe na kusema: “Nawashauri mabinti wenzangu kujitunza kwanza, angalau wavumilie waweze kuwa na umri sahihi na wanapokuwa wajawazito wahakikishe wanafuata maelekezo yote akina mama tunayoambiwa hospitali.”

Mama wa binti huyo anasema hatasahau mateso aliyoyapata katika kumlea binti yake huyo katika kipindi cha ujauzito. “Mpaka anajifungua namshukuru Mungu, ametusumbua sana, tulikuwa hatulali vizuri, alikuwa anapungukiwa damu mara kwa mara na alikuwa amedhoofu sana na hasa kwa kuzingatia pia kwamba mwili wake ni mdogo sana,” anasema mama huyo.

Daktari Bingwa wa Wanawake katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Dk Jeremiah Mahamba anasema binti chini ya miaka 18 ni mtoto ambaye maumbile yake hayajakomaa vizuri kubeba mimba, kujifungua na kulea mtoto.

“Hawa watoto mara nyingi wanakuwa na shida hasa ya lishe na wako kwenye hatari ya kupata upungufu wa damu, kifafa cha mimba, fistula na pia hawafuatilii kliniki wakati wa ujauzito ni mpaka apate mtu wa kumsukuma,” anasema Dk Mahamba na kuongeza kuwa wengi wao mimba zao huwa siyo za kutarajia.

Dk Mahamba anasema wengi wao hujifungua kwa upasuaji kwa sababu nyonga zao zinakua bado ndogo na akijifungua kawaida wengi huishia kupoteza mtoto kwa sababu ya kukaa na uchungu muda mrefu na mtoto kukaa njiani kwa muda mrefu. Anasema athari hutokea hata katika malezi ya mtoto.

“Wengine hata mtoto akiugua hawezi kujua mapema kutokana na umri wake,” anasema Dk Mhamba. Taarifa za uzazi wilayani Kilwa zinaonesha kuwa kati ya Januari na Novemba 2018, kinamama 5,844 walikuwa wamejifungua na 1,255 kati yao walikuwa na umri chini ya miaka 20.

Kadhalika katika kipindi hicho kinamama waliojiunga na huduma ya kliniki kutokana na ujauzito ni walikuwa 8,533 na kati ya hao wenye umri chini ya miaka 20 walikuwa ni 1,710. Afisa Afya wa Wilaya ya Kilwa, Ennocentia Mangosongo anasema: “Kati ya kina mama hao, 86 wamejifungua kwa upasuaji, hata hivyo tunashukuru hakukuwa na vifo, ingawa vifo vya vichanga ni 32”.

Mangosongo anataja sababu ya vifo vya vichanga kuwa ni wanaobeba mimba katika umri mdogo kuchelewa kupata huduma za kliniki. “Tatizo ni kwamba mabinti hawa hujificha kwanza kwa sababu wanajua wakija hospitali watahojiwa nani aliyewapa ujauzito,” anasema Mangosongo.

Alikopita Johari Johari alihitimu darasa la saba katika Shule ya Msingi Kilwa Kisiwani na baada ya hapo alianza kuuza samaki wa kukaanga akiwatembeza muda wa jioni sehemu mbalimbali za mji wa Kilwa Masoko.

Anasema alihitimu darasa la saba akiwa na miaka 15 na akiwa katika kutembeza samaki alishawishiwa na kijana anayeishi naye Kilwa Kisiwani kwa sasa, wakaingia kwenye uhusiano wa kimapenzi ambako alipata ujauzito.

“Haukua umri sahihi wa kushiriki mapenzi lakini nilishawishika mtaani wakati natembeza samaki kuuza,” anasimulia. Anasema katika kuuza samaki wanazunguka huku na huko kutafuta wateja hata nyakati za usiku.

Mwenyekiti wa Kata ya Kilwa Masoko, Athuman Ally anasema hawajafanya utafiti kujua ukubwa wa tatizo la mimba na ndoa za utotoni, lakini anaakiri kwamba wapo mabinti wengi ambao wameolewa au kujifungua katika umri mdogo.

“Hakuna wazazi wanaokuja kushitaki au kwenda polisi, ni kama wazazi wanashirikiana na watoto hawa, jambo ambalo litafanya ugumu zaidi kutokomeza ndoa na mimba za utotoni,” anasema Ally.

Anasema binti anapopata ujauzito, wazazi wake hushirikiana na wazazi wa mwanaume aliyempa mimba binti yao ili asifungwe. “Hawamtaji ili asifungwe baadaye amuoe binti yao,” anasema.

Ally anasema sababu kubwa anayoiona ni uelewa mdogo, umasikini katika familia nyingi na pia familia kuogopa kuvunja undugu. Anasema mabinti ambao hupata mimba katika umri mdogo, watoto wao huwa na afya mbaya, kwani hawana uwezo wa kuwapa malezi stahili.

“Kwanza binti anakuwa hajui namna sahihi ya kutunza mtoto na hata kujitunza mwenyewe, lakini hata akijua huwa hana fedha za matunzo, kula na kulisha. Mtoto hula chochote anachopata hapo nyumbani,” anasema.

Kauli ya mwenyekiti huyo inaungwa mkono na Mangosongo ambaye anasema uelewa wa mabinti wenye umri mdogo kuhusu masuala ya uzazi ni mdogo hivyo kutozingatia maelekezo wanayopewa kliniki, hasa chanjo na dawa.

“Wengi utakuta kutokana na kutofuatilia vizuri dawa, wanakuwa na tatizo la upungufu wa damu kwa sababu mahudhurio yao kliniki ni hafifu na pia ufuatiliaji mdogo wa dawa hasa za kuongeza damu,” anasema.

Anasema wengi wa akinamama hao wenye umri mdogo husaidiwa wakati wa kujifungua kwa watoto wao kuvutwa au kufanyiwa upasuaji kutokana na maumbile yao kutokomaa kuhimili uzazi.

Anaongeza kuwa wengi pia huwa hawajajiandaa kisaikolojia kuwa mama, hivyo huwa wagumu kunyonyesha, hasa mwanzoni na kushindwa kuzingatia maelekezo ya matunzo kwa watoto.

Mangosongo anatoa mwito kwa wazazi na walezi wanaowalea mabinti kuwahimiza kwenda hospitali pale wanapopata ujauzito ili waanze kliniki mapema, wapate chanjo na dawa stahili.

Kwa mujibu wa Shirika la Kimataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF), watoto wachanga waliozaliwa na mama mwenye umri mdogo, wanakabiliwa na hatari kubwa zaidi ya kupoteza maisha kuliko wale waliozaliwa na mama wa umri mkubwa.

UNICEF linaeleza kuwa kwa kila vichanga 1,000, vinavyozaliwa na mama wa umri wa chini ya miaka 20, vichanga 41 hupoteza maisha ndani ya mwezi mmoja baada ya kuzaliwa.

Kwa mujibu wa shirika hilo, mama anapokuwa na umri wa miaka 20 hadi 29, idadi ya vifo vya vichanga hupungua hadi kufikia vifo 22 kwa kila vichanga 1,000 vilivyozaliwa hai. Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu anasema serikali inatambua kuwepo na idadi kubwa ya wasichana wanaoolewa katika umri mdogo.

Akizungumza katika uzinduzi wa Utafiti wa Kitaifa kuhusu Sababu na Athari za Ndoa za Utotoni, uliofanywa na taasisi ya Repoa katika mikoa mbalimbali nchini kati ya mwaka 2015 na 2016, Mwalimu anasema serikali inachukua hatua kadhaa za kukabiliana na tatizo hilo licha ya kuwapo kwa vikwazo.

Waziri huyo anataja moja ya vikwao hivyo kuwa ni Sheria ya Ndoa ya 1971. Sheria hiyo inaruhusu mabinti wenye umri chini ya miaka 18 kuolewa. Sheria hiyo inakinzana na sheria nyingine kadhaa ikiwamo Sheria ya Mtoto ya 2009 ambayo inamtambua mtu yeyote mwenye umri chini ya miaka 18 kuwa ni mtoto, hivyo kuwa na uhusiano naye ni kufanya kitendo cha ubakaji.