‘Chuki, wivu vinaweza kusababisha shinikizo la damu, kisukari

KABLA ya kwenda hospitali, Jackson John (siyo jina halisi) hakujua kuwa ana tatizo la shinikizo kubwa la damu. John mwenye umri wa miaka 62 na mkazi wa Dar es Salaam anasema: “Nilikwenda hospitali kwa ajili ya kupata tiba ya jicho langu lililokuwa linauma sana. Lakini baada ya ku pimwa, nilikutwa na shinikizo la damu likiwa 187/143. Kwa kweli nilipata mshituko kwa sababu sikutarajia kuwa na ugonjwa huu,” anasema.

Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo kutoka Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Tatizo Waane anasema msukumo wa kawaida wa damu ni 120/80 mmHg. Mtu atabainika kuwa na shinikizo kubwa la damu endapo msukumo wa damu utakuwa juu ya 140/90mmHg.

Akichunguzwa kwa zaidi ya mara tatu na msukumo wa damu ukaendelea kuwa juu ya 140/90, basi moja kwa moja atahesabika kuwa ana shinikizo kubwa la damu.

Lakini ikitokea msukumo wa damu ukawa chini ya 100/60mmHg, atahesabika kuwa na shinikizo la chini la damu. Kwa kuzingatia vigezo hivyo, John ni mgonjwa wa shinikizo kubwa la damu ambaye anashauri jamii kujenga utamaduni wa kupima afya mara kwa mara ili kujua hali kiafya.

“Kwa sababu hata mimi sikujijua hadi nilipokwenda hospitali,” anasema John. John anawakilisha kundi la watu wanaoishi na magonjwa sugu yasiyo ya kuambukiza bila kujijua kutokana na kutokuwa na utamaduni wa kupima afya mara kwa mara.

Hakujua kuwa msukumo wake wa damu katika mwili unazidi kiwango cha kawaida. Analo shinikizo kubwa la damu ambalo linaloweza kusababisha madhara mwilini.

Kitaalamu, moyo unapopiga husukuma damu kwenye mishipa ya damu ili isambae mwilini kote. Katika kitabu cha ‘Mtindo wa Maisha na Magonjwa yasiyo ya Kuambukiza’ kilichochapishwa mwaka 2013, inaelezwa shinikizo kubwa la damu linaweza kusababisha kupasuka kwa mishipa ya damu kichwani na kusababisha kiharusi ambacho ni miongoni mwa sababu kubwa ya vifo vya watu wazima.

Kitabu hicho kilichotayarishwa na Chama cha Kisukari Tanzania (TDA) kinachoelimisha jamii juu ya dalili, athari na kinga, kinasema shinikizo kubwa la damu husababisha moyo kupanuka na hatimaye kushindwa kufanya kazi yake ya kusukuma damu.

Wataalamu kupitia chapisho hilo wanataja madhara mengine ni kuharibika kwa mishipa ya damu kwenye figo na hatimaye figo kushindwa kufanya kazi yake ya kusafisha damu.

Madhara mengine ni mishipa mikubwa ya damu kuharibika kwa sababu ya kuvuja kwa virutubishi vilivyo kwenye damu na kusababisha kiharusi, ugonjwa wa moyo au miguu kutopata damu ya kutosha.

Watu wengi wenye shinikizo kubwa la damu huwa hawana dalili zozote huku wengine wanaweza kuwa na dalili za kuumwa kichwa mara kwa mara; kutoona vizuri; kizunguzungu; moyo kupiga kwa nguvu au haraka haraka.

Dalili nyingine ni kutokwa na damu puani; maumivu ya kifua au kupumua kwa shida na uchovu wa mara kwa mara.

Ili kugundua kama una shinikizo kubwa la damu, wataalamu wanashauri kuwa ni vyema kupima msukumo wa damu kila unapoenda kwenye kituo cha tiba au kupima angalau mara moja kwa mwaka. Inaelezwa kuwa wakati mwingine, watu wenye shinikizo kubwa la damu ghafla, wanaweza kuwa na dalili za kiharusi. Inashauriwa kwamba ni vyema mtu akiona dalili hizi asisite kutafuta msaada wa mhudumu wa afya.

Visababishi vya shinikizo kubwa la damu Sababu zinazochangia mtu kupata shinikizo kubwa la damu ni pamoja na matumizi ya chumvi kupita kiasi hasa ya kuongeza mezani.

Vingine ni utumiaji wa pombe kupita kiasi, utumiaji wa tumbaku na bidhaa zake, msongo wa mawazo kutokana na vitu kama vile majanga na unyanyasaji wa kijinsia.

Wasiwasi, wivu, chuki, hasira huongeza msukumo wa damu na uwezekano wa kupata shinikizo la damu na kisukari. Umri mkubwa hususani kuanzia miaka 60 na kuendelea ni kisababishi kingine cha tatizo hilo.

Lakini pia, iwapo ndani ya familia ipo historia ya shinikizo kubwa la damu, upo uwezekano wa kupata tatizo. Wakati huo huo uzito mkubwa kupita kiasi na kutofanya mazoezi unachochea tatizo.

Aidha ugonjwa wa kisukari huendana na shinikizo kubwa la damu. Kuzuia shinikizo kubwa la damu Shinikizo kubwa la damu linaweza kuzuilika kwa kupunguza matumizi ya chumvi. Wataalamu wanashauri chumvi isizidi kijiko kidogo cha chai kwa mtu mmoja kwa siku.

Unaweza kupunguza matumizi ya chumvi kwa kutoongeza chumvi wakati wa kula mezani, na kuepuka vyakula vyenye chumvi kwa wingi kama vile chips, soseji, nyama choma, na samaki waliohifadhiwa kwa chumvi.

Mambo mengine ya kuzingatia ni kuepuka kunywa pombe kupita kiasi. Inashauriwa ya kuwa wanawake wasizidishe chupa moja ya bia, au glasi moja ya mvinyo au toti mbili za pombe kali kwa siku: waume wasizidishe mara mbili ya vipimo hivyo. Jambo jingine ni kufanya mazoezi ya viungo mara kwa mara na kujishughulisha na kazi mbalimbali mradi mwili upate mazoezi ya angalau nusu saa kila siku.

Zoezi linalotosha ni lile linaloufanya mwili kutoka jasho au moyo kwenda mbio kidogo, hivyo kutembea kama konokono haitoshi. Inashauriwa kuepuka uzito mkubwa kupita kiasi kwa kula kwa kiasi na kufanya mazoezi; kula matunda na mboga mboga kila siku; na kuepuka matumizi ya tumbaku na bidhaa zake.

Inabidi pia kupunguza msongo wa mawazo kwa kujiwekea viwango sahihi kulingana na uwezo wako, kuwa na taratibu za kazi, na kupata muda wa starehe na kupumzika, kama vile kuhudhuria sherehe mbali mbali, ngoma, na ibada za dini. Usingizi wa kutosha ni muhimu na kwa mtu mzima inashauriwa usipungue saa saba kila siku.

“Hivi ni visababishi vya shinikizo kubwa la damu na magonjwa mengine yasiyoambukiza kama vile kisukari,” anasema Dk Waane.

Anasisitiza jamii kubadili mtindo wa maisha unaosababisha shinikizo la damu, ikiwemo kuepuka matumizi ya chumvi nyingi na vyakula vyenye mafuta mengi.

Mlo wenye matunda na mboga mboga kwa wingi ndiyo unashauriwa kwa ajili ya kukabili siyo tu shinikizo kubwa la damu bali pia magonjwa mengine yasiyo ya kuambukiza yanayosababisha vifo vya mamilioni ya watu duniani.

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), shinikizo linaathiri watu wapatao bilioni 1.1 duniani sawa na asilimia 14 ya idadi ya watu wote duniani. WHO inataja ugonjwa huu kusababisha vifo milioni 7.5 ambavyo ni sawa na asilimia 12.8 ya vifo vyote vya duniani.

Takwimu za shirika hili la dunia zinaonesha kuwa Afrika ina kiwango kikubwa cha kuenea kwa ugonjwa huu. Wanaume wanakabiliwa na ugonjwa huu kuliko wanawake.

Takwimu za WHO za mwaka 2014, zinaonesha vifo vitokanavyo na shinikizo kubwa la damu nchini Tanzania vimefikia 3,424 kwa mwaka.

Maradhi haya huwakumba wanaume zaidi wenye umri wa kuanzia miaka 45 na kwa wanawake ni wenye umri wa miaka 65 na kuendelea. Lakini pia watoto wanaweza kupata maradhi haya kutokana na sababu sawa na watu wazima.