Simu za mkononi zinavyosababisha ajali barabarani

 JOSEPH Asenga (30) mkazi wa Moshi ni dereva wa bodaboda ambaye hivi karibuni aliripotiwa na vyombo vya habari kuwa alipoteza maisha baada ya kuligonga lori aina ya Scania alipokuwa akizungumza na simu huku akiendesha.

Asenga alipoteza maisha wakati akijaribu kuhama upande wake wakati huo huo dereva wa lori akijaribu kuhama upande wake.

Ndipo waligongana na kusababisha kifo chake. Matukio ya madereva wa vyombo vya moto kupoteza maisha kutokana na kutumia simu, yamekuwa yakijitokeza hadi kufanya polisi kutangaza kuwa dereva atakayekamatwa akiendesha gari huku akizungumza na simu ya mkononi atafutiwa leseni yake.

Agizo hilo lililotolewa na kikosi cha usalama barabarani kwa kushirikiana na Mamlaka ya Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra) mwaka 2010 hata hivyo halikudumu kutokana na mamlaka hizo kukosa nguvu ya kisheria ya kutekeleza hatua hiyo.

Hivi karibuni Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) liliripoti kuwa kuongezeka kwa kasi ya vifo vya watu wanaotembea kwa miguu nchini Marekani na kwa wale wanaoendesha magari, kumetajwa kutokana na watu kutumia simu zao wakati wakiendesha magari au wanapovuka barabara.

Halmashauri inayohusika na usafiri wa barabarani nchini Marekani inakadiria kuwa watembea kwa miguu 6,000 walifariki mwaka 2016 ikiwa ndiyo idadi kubwa zaidi katika kipindi cha miaka 20. Katika kipindi cha miaka sita iliyopita vifo vimeongezeka mara nne zaidi.

Ripoti inasema kuwa masuala kadha yamechangia ikiwemo matumizi ya simu za mkononi na hasa kwa wanaotumia simu za kisasa. Kwa haya yanayotokea Ulaya pia yanatokea nchini kutokana na kutokuwepo sheria yoyote inayokataza madereva kuzungumza na simu wanapoendesha.

Pia ipo sheria inayokataza waenda kwa miguu kuzungumza na simu pale wanapokuwa wanavuka barabara.

Simu za mkononi zimekuwa zikichangia kutokea kwa ajali nchini. Hii ni kutokana na dereva wa vyombo vya moto kuendesha gari wakati huo huo anatuma ujumbe wa maneno kwenye simu au anazungumza na simu.

Sababu nyingine ni wengine kuangalia picha kutoka kwenye mitandao ya simu, jambo ambalo linamfanya umakini barabarani upungue.

Mwanasheria kutoka Chama cha Wanasheria Wanawake (TAWLA), Mary Richard, anasema asasi yake kwa kushirikiana na asasi nyingine wanapigania kuwepo kwa sheria mpya ya usalama barabarani ambayo itapiga marufuku madereva kutumia simu wanapoendesha magari.

Anasema TAWLA inapigania sheria mpya ya usalama barabarani kwa kuwa madereva wanaoendesha magari wakiwa wanatumia simu za mkononi, wako kwenye hatari kubwa ya kusababisha ajali za barabarani.

Anasema idadi ya ajali zinazohusisha watumiaji wa simu ni nyingi na zinaweza kupungua pale sheria ya usalama barabarani itakataa matumizi ya simu.

Mwanaharakati wa masuala ya usalama barabarani Augustus Fungo hivi karibuni alikaririwa kwenye mitandao ya kijamii akifafanua juu ya kasoro katika sheria.

Anasema chini ya sheria ya usalama barabarani Sura ya 168, sheria hiyo ya usalama barabarani wala kanuni zake, haina kipengele chochote kinachopiga marufuku matumizi ya simu, au kuweka ‘headphone’ masikioni na kuendesha gari au hata dereva kuangalia video ndani ya gari.

Fungo ambaye ni mwanachama wa Chama cha Mabalozi wa Usalama barabarani, anasema sababu yenyewe ya msingi ni kwamba hii sheria ya usalama barabarani ni ya mwaka 1973.

Licha ya kufanyiwa marekebisho ya mara kwa mara, marekebisho makubwa kabisa yalifanyika mwaka 1996 wakati huo ndio kwanza simu za mkononi zilianza kuingia nchini.

Je, ni kosa kutumia simu huku unaendesha chini ya kanuni za Sumatra? Fungo anasema majibu ni ndiyo na hapana. Anafafanua kuwa jibu ni ‘ndiyo’ pale unapoongelea kanuni za SUMATRA za mwaka 2007 na pia kanuni za mwaka 2017.

“Kwa sasa sina jibu iwapo kanuni zipi hasa ndizo zinatumika kwani sina uhakika kama zile za mwaka 2017 zimeanza kutumika.

Anasema kanuni za Sumatra za usafirishaji abiria za mwaka 2007, kwa mujibu wa kanuni ya 18(1)(i) ni marufuku kwa dereva kuendesha gari huku akitumia simu.

Anasema Kanuni za Leseni ya Usafirishaji-Magari ya Mizigo za mwaka 2012 kwa mujibu wa kanuni ya 28(1)(h) dereva amekatazwa kutumia simu au kifaa kinachofanana na hicho wakati wa kuendesha gari. “Hivyo basi tunaona kuwa kwa mujibu wa kanuni hizi za usafirishaji ni kosa kuendesha gari huku dereva anatumia simu.

Lakini swali la kujiuliza je, marufuku hii inamhusu kila dereva,” anasema na kuongeza: “Jibu ni ‘hapana’ kwa kuwa kanuni za Sumatra zinamhusu mtu aliyepewa leseni na Sumatra kuendesha huduma ya usafiri na wafanyakazi wake, mtu huyu anaitwa licensee.

“Yaani hadi uwe na leseni ya Sumatra ndiyo kanuni hizi zinakuhusu. Hivyo ndiyo kusema kwamba kama humiliki gari la abiria au la mizigo kanuni hizi hazikuhusu,”anasema.

Je, ni kosa kuendesha gari huku dereva akizungumza na simu kwa mujibu wa kanuni mpya za Sumatra za usafirishaji abiria za mwaka 2017? Fungo anasema hapana kwani kanuni hizi hakuna popote zinapompiga marufuku dereva akizungumza au kutumia simu huku anaendesha gari.

Je, ni kosa kuendesha gari huku dereva akizungumza na simu kwa mujibu wa kanuni mpya za Sumatra za usafirishaji Magari ya Mizigo za mwaka 2017? Fungo anajibu kuwa jibu ni ndiyo kwani Kanuni za Leseni ya Usafirishaji Mizigo, 2012 zimefanyiwa marekebisho na Kanuni za Leseni ya Usafirishaji mizigo za 2017 ambapo katika kanuni hizo mpya kuna vifungu vimefanyiwa marekebisho lakini kifungu 28(1) hakijafanyiwa marekebisho, hivyo kufanya lile kosa la dereva akizungumza na simu huku anaendesha kuendelea kuwa kosa.

“Kwa hiyo iwapo kanuni mpya za Sumatra zimeanza kufanya kazi, siyo kosa tena kwa dereva wa gari la abiria kuendesha huku akizungumza na simu.

“Wakati huo huo ni kosa kwa dereva wa gari la mizigo kuendesha huku akizungumza na simu kwa mujibu wa kanuni ya 28(1). Iwapo kanuni za zamani zinaendelea kutumika, basi ni kosa kwa dereva wa gari la mizigo na yule wa gari la abiria kuendesha huku akizungumza na simu,”anasisitiza.

Mwanasheria wa Kikosi cha Usalama barabarani Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (ASP), Deus Sokoni anasema kwamba katika sheria mpya ya usalama barabarani ambayo wanaendea kuitunga, matumizi ya simu wakati dereva anaendesha gari yatapigwa marufuku.

Anasema madhara ya simu ni makubwa na ndiyo maana serikali imeamua kwamba sheria mpya ihakikishe inaingiza marufuku ya dereva kutumia simu ili kupunguza vifo vinavyotokana na ajali za barabarani.

“Yaani marufuku itakuwa ni kwa dereva kushika simu kwa madhumuni ya kupiga au kuandika ujumbe mfupi wa maneno wakati anaendesha gari,”anasema Sokoni.

Anasisitiza kuwa simu zina madhara makubwa kwani wakati mwingine dereva anaperuzi mitandao ya kijamii au kuangalia picha kwenye mitandao ya kijamii jambo ambalo ni hatari kubwa.

“Binafsi nimeshuhudia gari linagongwa na dereva wake anakufa huku ameshikilia simu mkononi, hii inaonesha kwamba ajali hiyo chanzo chake ilikuwa ni simu,”anasema Sokoni na kuongeza kuwa kwa hali hiyo jambo hilo lazima lipigwe marufuku na sharia.

Anasema kwa sasa sheria ya usalama barabarani haizungumzii lolote kuhusu matumizi ya simu na ndiyo maana Polisi wa usalama barabarani hawakamati mtu ambaye anazungumza na simu kwa sababu hakuna sheria ya kumbana.

Katika nchi zilizoendelea ni marufuku kugusa simu wakati unapoendesha gari au pikipiki. Marufuku hiyo inahusu kuangalia ramani ya mahali unakoenda, kutuma ujumbe au kuangalia mitandao ya kijamii.

Sheria za nchi zingine zinasisitiza kuwa hata kama dereva amesimama kwenye taa za barabarani haruhusiwi kugusa simu bali anashauriwa kuegesha gari pembeni na kutumia simu. Nchini Uingereza faini ya kosa hilo ni paundi 100 zaidi ya Sh 300,000.