UCSAF ilivyokomboa wafanyabiashara, kutimua matapeli vijijini

“KAMA nisingetapeliwa zaidi ya Sh 200,000 na kondakta wa basi mwaka 1982, leo hii ningekuwa mfanyabiashara mkubwa sana.”

Hiyo ni kauli ya Athuman Sabo, mkazi wa kijiji cha Izava, Kata ya Segala wilayani Chamwino, Dodoma ambaye ni mkulima, mjasiriamali na mlinzi katika mnara wa simu uliojengwa na serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) ambao unaendeshwa na Kampuni ya Mawasiliano ya Vodacom. Sabo, mzee wa makamo, aliyasema hayo hivi karibuni wakati wa ziara ya waandishi wa habari wa Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN) waliotembelea baadhi ya wilaya na mikoa ya Kanda ya Kati ya Dodoma, Singida na Manyara ili kubaini namna mpango huo wa serikali kupitia UCSAF ulivyowanufaisha wananchi wa kada mbalimbali kiuchumi na kuyapa maisha yao mabadiliko chanya.

Akizungumzia manufaa ya mnara huo unaohudumia vijiji 11 vyenye wakazi zaidi ya 20,000 kikiwemo Izava chenye wakazi 8,778 na ambacho zaidi ya 5,100 wanapata huduma ya simu na kusifu usikivu wake, Sabo anasema umeibua hamasa ya maendeleo kwa watu wengi kutokana na kuwa na mawasiliano na wenzao wa nje ya kijiji, na hivyo kuwasiliana kwa urahisi na ndugu, jamaa, marafiki na wadau wa sekta mbalimbali ndani na nje ya nchi.

Anajitolea mfano kwamba alianza kufanya biashara katika miaka ya 1970 na kufanikiwa mno, lakini kutokana na kukosekana kwa mawasiliano ya uhakika, alijikuta akikwamishwa na watu waliomtapeli fedha. “Nisikufiche bwana, kwa kutuletea hii minara kwa kweli Serikali imeonyesha jinsi inavyojali watu wake, mpaka wa vijijini. “Mwaka 1982 nilikuwa nafanya biashara ya kununua baiskeli na kuziuza huku kijijini. Ilifika mahali mtaji ulikuwa mkubwa, lakini tulifanya biashara kienyeji.

Kwa mfano, ili niagize mzigo, tulikuwa tunavizia mabasi yanayokwenda Dodoma, Dar es Salaam na kwingineko, hapo unampatia kondakta fedha na maelezo, anakwenda kukuletea mzigo lakini baada ya kumpoza posho kidogo. “Siku ya kurudi inabidi tena kwenda kuvizia na kuchukua mzigo wako. Sasa safari moja bwana, yule kondakta alichukua kama shilingi laki mbili yangu kwa ajili ya mzigo mkubwa wa baiskeli, lakini hakurudi kabisa (anainama na kusikitika). Hapo ndipo aliponiua kabisa. Kwa kweli nilichanganyikiwa kwa sababu ilikuwa fedha nyingi sana wakati ule,” anasimulia Sabo.

Hata hivyo, anasema kuingia kwa teknolojia ya mawasiliano ya simu za mkononi na ambayo serikali imeamua kuwapelekea wananchi vijijini kupitia UCSAF, kumerahisisha ufanyaji wa biashara na hivyo kuwaokoa wengi waliokuwa wanatapeliwa kama ilivyokuwa kwa upande wake. Anasema sasa, kutokana na kuwapo kwa mawasiliano ya uhakika kutokana na kuwa na usikivu mzuri katika kijiji chake kilichopo umbali wa zaidi ya kilomita 60 kutoka barabara kuu ya Dodoma-Babati kupitia Kondoa, na kilometa zaidi ya 170 kutoka Dodoma Mjini, ufanyaji wa biashara umerahisishwa.

Sabo anaendelea kusema; “Pamoja na kulinda mnara wa simu wa Vodacom hapa ambayo ni ajira, mimi bado ni mjasiriamali na ni mkulima pia, nina ekari zaidi ya 15 ambazo wakati wa mavuno aah, uongo mbaya nakuwa mtu mzito. “Sasa basi, kuanzia wakati wa mavuno, nikishavuna nashika simu hapahapa nilipo, natafuta soko tukishaelewana namwambia mtu lete gari, anakuja kupakia mzigo na si lazima aje tajiri.

Anaweza kutuma fedha moja kwa moja kupitia huduma ya M-Pesa, maisha yanaendelea. “Au, nikitaka kuagiza bidhaa, labda mtu anataka pikipiki hakuna kutuma tena kwa mabasi, kwani baada ya kuzungumza na wauzaji nakwenda kwa wakala wa huduma ya pesa, natuma fedha na mzigo naupokea hapahapa kijiji kulingana na maelezo. Hakuna tena ujanjaujanja au biashara za roho mkononi. Unadhani bila kuletewa mawasiliano na Serikali haya yangefanyika? Tungebaki kulekule, lakini sasa tunakwenda sambamba na wafanyabiashara wa sehemu mbalimbali,” anasema.

Anatoa mfano wa mtu mwingine, dalali wa mazao kijijini hapo ambaye aliingia matatani baada ya kutapeliwa shehena kubwa ya mazao, hali iliyosababisha apoteze maisha kwa mshituko. “Kabla ya simu, iliwahi kutokea jamaa alikuwa anaaminiwa kuchukua mazao kwa wakulima naye anachukua mzigo kuupeleka mjini, kisha kuja kuwalipa ingawa kwa kuwapunja mno, hawa madalali ndio waliokuwa wananufaika sana. “Ilivyokuwa ni kwamba, si miaka mingi, akiwa na shehena kubwa ya mazao aliyokusanya kutoka kwa wakulima, alikodi Fuso tatu kubeba mzigo. Jamaa wakapakia na kuondoka.

Wale jamaa hawakupatikana kwa sababu namba walizotumia kwenye magari zilikuwa bandia. Wakamsababishia matatizo dalali wa watu. “Kungekuwa na simu isingefikia hatua hiyo, kwani biashara ingefanyika bila presha na pesa kutumwa, hivyo wale madereva wangejuana na mwenye gari moja kwa moja, lakini jamaa aliingia matatani na wakulima. Lakini kwa zama hizi za mawasiliano ya uhakika, matapeli wa aina hiyo wangekamatwa na pia mkulima sasa ana uwezo wa kuongea na tajiri na kumalizana naye, si kupitia tena mikononi mwa matapeli,” anasimulia.

Zebedayo Nyuda wa kijiji cha Makuro wilayani Singida Vijijini, anasema hofu ya kutapeliwa au kuibiwa iliwaingia wengi, kiasi cha kumfanya hata yeye ashindwe kuwa na akaunti benki katika umri wake wa zaidi ya miaka 65. “Matukio ya kitepeli na wizi yalikuwa mengi, ili kujiepusha sikuwahi kuweka pesa benki, ndiyokwanza nimefungua akaunti mwaka jana na sasa natumia zaidi miamala hii ya simu kutoa na kuweka fedha,” anasema. Ramadhani Kitandu, mfanyabiashara mkubwa wa simu, vifaa vya simu na huduma za mitandao ya simu ambaye pia ni fundi wa simu na madishi kijijini na katika Kata ya Makuro kwa ujumla, anasema hana hofu tena ya kutapeliwa kwa nyakati kama hizo ambazo huagiza sehemu kubwa ya bidhaa zake kwa njia ya simu kutoka Dar es Salaam, Mwanza na kwingineko.

“Uzuri ni kwamba sasa tuna mawasiliano ya uhakika. Nawasiliana na matajiri moja kwa moja, napakia kwenye gari na mzigo unafika hapa bila ya hofu. Naweza kufuatilia mzigo wangu njia nzima nikajua uko wapi. “Simu zimerahisisha sana mambo. Mfano hapa kwangu, nafungua biashara kuanzia mchana kwa sababu asubuhi nakuwa shambani, nina ekari zangu kama 15 hivi na nikija mchana naendelea na biashara hadi usiku. Kabla ya ujio wa simu, ilikuwa lazima kuacha shughuli zote ili kufuatilia mzigo, lakini sasa yote yanafanyika kwa pamoja, biashara zinaendelea, kilimo kinaendelea bila kuathiriwa na safari,” anasema.

Kauli hizo zinaungwa mkono na Mwenyekiti wa kijiji cha Izavi, Sokoine Mbelewa, aliyezungumzia pia manufaa ambayo kijiji chake kimeyapata kutokana na kupelekewa mnara wa simu na UCSAF. Mwenyekiti huyo kijana, anasema mbali ya mawasiliano kupunguza safari ndefu zinazokula muda mwingi wa kuchapa kazi, huduma za kipesa zimeibua ari ya watu kujenga tabia ya kujiwekea fedha, kwani awali hali ilikuwa tofauti kutokana na kuwa mbali na benki. Iliwalazimu kusafiri hadi mjini Dodoma au Kondoa.

“Lakini sasa mtu anauza mazao yake anapokea fedha kwa njia ya simu, hivyo kuokoa muda wa kusafiri umbali mrefu kufuata huduma huku biashara ikiwa imefungwa mpaka utakaporudi. Hili lilikuwa na athari nyingi, nyingine ikiwa hatari ya kuvamiwa na kuibiwa maana unakuwa hujui nani mbaya wako, lakini sasa kila kitu kwa simu, mambo ni mazuri sana.

“Yaani ukiwa na fedha zako kwenye simu uko salama kwa sababu unafanya manunuzi au malipo wakati wowote utakaoona unafaa. Kupitia hizi huduma za pesa iwe M-pesa, TigoPesa, HaloPesa, TTCL au nyingine yoyote, unakwenda kibandani wakati wowote; mtu hajui kuwa labda umeenda kununua vocha, unaweka au kuchukua pesa zako kwa dakika chache halafu unarudi kwenye shughuli zako. Inaokoa sana muda wa watu,” anasema Mbelewa.

Mwitikio wa wananchi wanaonufaika na huduma za mawasiliano ya simu kupitia minara ya UCSAF, bila shaka umetoa taswira kwamba, dhamira ya dhati ya serikali kuwafikia wananchi katika maeneo yasiyo na mvuto wa kibiashara imefanikiwa, hivyo nao kuwafanya wafurahie matunda ya nia njema ya serikali ya fursa sawa za mawasiliano kwa wote, mijini na vijijini.

Hata hivyo, wananchi hao wameonesha kiu zaidi ya kutaka kwenda sambamba ya wenzao wa mijini, hasa kwa kutaka kuboreshewa huduma hadi ya mfumo wa 3G kutoka 2G ya sasa ili waweze pia simu za kisasa kwa ajili ya huduma za intaneti na nyinginezo. UCSAF, mfuko ulianzishwa mwaka 2006, unawezesha mawasiliano ya simu katika maeneo mbalimbali ya vijijini yasiyo na mvuto wa kibiashara kwa kujenga minara ya mawasiliano inayoendeshwa na kampuni za simu za TTCL, Vodacom, Airtel na Tigo katika maeneo mbalimbali nchini.