Maendeleo ya dini na Kiswahili

ASILI ya Lugha ya Kiswahili ni Pwani ya Afrika Mashariki. Kabla ya kuja wageni wa Kiarabu, Kijerumani na baadaye Waingereza, lugha ya Kiswahili ilikuwa inazungumzwa katika upwa wa Afrika Mashariki.

Ushahidi wa kihistoria na kiisimu unabainisha hivyo. Zilikuwapo lahaja mbalimbali ambazo zilikuwa zinazungumzwa katika Pwani ya Afrika Mashariki. Wageni hao tuliowataja hapo juu na wengine waliopita katika Pwani hii ya Afrika Mashariki kwa lengo la kufanya biashara au kueneza dini walitumia lugha hizi kwa ajili ya mawasiliano. Makala haya hayana lengo la kuelezea historia ya Kiswahili tangu kipindi cha ujio wa wageni hawa, bali yatajikita zaidi kuangalia mchango wa wageni hawa hasa tukiangalia upande wa dini walizoleta huku Afrika.

Tunajua kabisa wageni hawa walipokuja, walikuja na dini zao. Waarabu walileta Uisilamu na Wazungu wakaleta Ukristu. Dini hizi zote zina mchango mkubwa katika kukua kwa msamiati wa Kiswahili. Makala haya yatachambua baadhi ya maneno yanayotumika kanisani na misikitini na jinsi yalivyochangia kukua kwa Kiswahili. Kwa mfano, tunapoelekea kipindi hiki cha Pasaka utasikia maneno mengi yanayohusiana na ufufuko wa Yesu Kristo. Hali kadhalika, tunapoingia katika kipindi cha Sikukuu za Kiislamu, kwa mfano sikukuu ya Idd el fitri utasikia maneno mengi yanayoambatana na sikukuu hiyo.

Maneno haya licha ya kutajwa sana katika kipindi husika yana mchango katika lugha yetu ya Kiswahili. Yapo maneno yaliyozoeleka hata kufikia hatua ya kuzalisha misemo, ambayo inatumika hadi leo. Hapa tutataja orodha ya baadhi ya maneno na asili yake na misemo iliyozalishwa hasa upande wa dini ya Kikristo.

Neno              Asili ya neno

Pasaka            Kiebrania (pasakh)

Aleluya/          Kiebrania haleluya (hallelujah)

Msalaba          Kiebrania

Masiya/masihi Kiebrania

Kanisa            Kiarabu

Sadaka           Kiarabu

Zaka              Kiarabu

Injili               Kiarabu

Madhabahu     Kiarabu

Kristu             Kiingereza

Toba              Kiarabu

Divai              Kifaransa

Katika orodha hii ya maneno, utaona kuwa lugha ya Kiarabu imetoa maneno mengi zaidi kuliko lugha nyingine ingawa si lengo letu kulinganisha lugha hizi. Kiebrania pia kina mchango mkubwa katika msamiati wa kanisani ingawa ni lugha ambayo pengine haitajwi sanazinavyoweza kupeana maneno na kutumika katika lugha nyingine. Kwa mfano, neno kama aleluya limetoka katika lugha ya Kigiriki (allelouia) likaazimwa na Walatini (alleluia), Kutoka kwa Walatini likachukuliwa na Waebrania (hallelujah) na hatimaye Waswahili nao tukalichukua na kulitumia.

Ingawa katika katika mataifa yaliyochangia kukua kwa msamiati wa Kiswahili. Maneno haya yameingia katika lugha ya Kiswahili na yamekubalika na kurasimishwa. Hii ndiyo tabia ya lugha zote duniani na namnaKiswahili tunatumia maneno yote mawili kutoka Kilatini na Kiebrania. Waingereza nao wametumia neno hili kutoka katika Kilatini (alleluia).

Hivyo utaona kuwa hakuna lugha inayoweza kutamba na kusema haijakopa neno lolote kutoka katika lugha nyingine, la hasha, lugha zinategemeana na kukamilishana. Maneno yanaweza kutoka katika lugha moja na kwenda katika lugha nyingine. Neno kanisa limetoka katika lugha ya kiarabu, lakini neno hili katika lugha ya Kiswahili linatumiwa zaidi na Wakristo kuliko wanavyolitumia Waislamu.

Maneno kama zaka na sadaka yametoka katika lugha ya Kiarabu lakini manenohaya katika Kiswahili hutumiwa na pande zote mbili kwa Wakristo na kwa Waislamu. Yapo maneno mengi ambayo yametokana na uga wa dini ambayo yamekopwa kutoka lugha za kigeni. Maneno haya yamekuwa na mchango mkubwa katika lugha ya Kiswahili na hasa katika kusheheneza msamiati na istilahi za uga wa dini kwa Waswahili.

Kutokana na maneno haya kuingizwa katika lugha ya Kiswahili na kuwa maneno rasmi katika lugha ya Kiswahili baadhi ya maneno haya yamekolea na hata kupewa misemo ya Kiswahili na kutumika katika maisha ya kawaida ya WaswahiliMfano wa maneno yaliyopata misemo ya Kiswahili ni haya yafuatayo; kanisa, sadaka, injili, msalaba na toba nk. Siku hizi unaweza kusika mtu akisema, “Bwana, mimi sijaja kufanya kazi ya kanisa hapa,” Mtu akisema hivyo, watu wanamwelewa haraka tu na hakuna anayeuliza maana ya usemi huo. Tena unatumiwa na watu wote, wa madhehebu ya Kikiristo na wasio Wakisto.

Au wakati mwingine unasikia “Sijaja kutangaza injili, huku nimekuja kutafuta hela” au utamsikia “Hapo ndugu yangu umetoa sadaka tu, kubali yaishe! Aidha, watu huambiana “Huu ni msalaba wako, ubebe bila manung’uniko” Bila shaka umeweza kugunduakuwa semi zote hizo zimetokana na mazingira ya kidini na hasa dini ya Kikristo. Bila ya kuwepo dini hiyo, huenda tusingekuwa na maneno hayo na misemo hiyo.

Semi hizo zimekuwa zikitumiwa hivyo kurejea maisha ya mwanzo na hasa Ukristo ulipoingia miaka ya nyuma. Kwa mfano, ukichukua sentensi ya kwanza, sijaja kufanya kazi ya kanisa, sijaja kutangaza injili, hapo umetoa sadaka, semi zina maana zinazoshabihiana. Kufanya kazi ya kanisa ni kufanya kazi isiyokuwa na malipo, kutangaza injili ni kazi inayohesabiwa kuwa haina malipo, ingawa kiuhalisia ina malipo, vinginevyo wachungaji na wainjilisti wangeshaacha kazi hiyo. Lakini katika dhati yake ni kwamba kazi hiyo haina malipo, malipo ni kwa Mwenyezi Mungu.

Mtu anapokuambia hapo umetoa sadaka ni kwamba umefanya kazi mabayo hutegemei kupata faida kutokana nayo. Mtu akikuambia kuwa huo ni msalaba wako ni kwamba, anamaanisha kuwa hilo ni jambo linalokuhusu wewe mia kwa mia, kwa hiyo ulikabili kwa namna lilivyo. Misemo hii inaposemwa au kuambiwa watu, hakuna anayehoji au kuuliza maana yake. Bali watu hujua maana zake bila kuuliza maana ya semi hizo. Hii inaonesha kuwa maneno na misemo hii imfahamika vyema kwa Waswahili. Misemo iliyotokana na mazingira ya dini na hasa dini ya Kikristo.

Mwanzoni kanisa lilikuwa linatoa misaada, hivyo watu waliona kama vile kazi yoyote isiyo kuwa na malipo ilifananishwa na kazi ya kanisa. Ndio maana utaona semi zote tulizokwisha zitaja hapo juu zinaonyesha kuwa kazi ya kanisa haina malipo, malipo ni kwa Mungu. Maneno kama malaika linafananishwa na mtoto mdogo asiyekuwa na mawaa, asiye na dhambi.

Utasika malaika huyu, hajuai kitu. Mtoto mdogo hana dhambi hivyo hawezi kukukosea au kwenda kinyume na taratibu kwa makusudi. Wakati mwingine, malaika hufananishwa na mwanamke mrembo, Mfano, Mwanamke, yule ni mzuri kama malaika, na ndio maana tukawa na wimbo unaoitwa.

‘Malaika’ Malaika, nakupenda malaika, nashindwa na mali sina………” Pengine unaweza kuwa unajua misemo mingi mingine inayotokana na dini yoyote ile, ujue kuwa misemo hiyo ipo kwa kuwa dini fulani imekuwapo na hivyo kuchangia idadi ya maneno, istilahi na misemo inayotokana na uga huu wa dini katika Lugha ya Kiswahili. Pamoja na kuwa lengo la kuletwa kwa dini hizi ilikuwa ni kumpatanisha binadamu na Mungu wake kutokana na dhambi, lakini kwa upande mwingine dini hizi zimechangia sana maendeleo ya lugha ya Kiswahili hasa kuongezeka kwa idadi ya msamiati, istilahi na misemo mbalimbali. Tukumbuke kuwa kila ubaya una pacha ya uzuri.