Huyu ndiye Edward Moringe Sokoine

“OLE wao wale wanaotumia nafasi zao za umma na serikali, kuiba, kuhujumu uchumi, kupokea rushwa, maana salama yao ni kudra za Mwenyezi Mungu labda nisiwajue.”

Hayo ni maneno aliyowahi kuyatamka Edward Moringe Sokoine, wakati akihutubia mkutano wa kikao cha Halmashauri Kuu wa CCM (NEC) mjini Dodoma, saa chache kabla ya kutokea kwa kifo chake. Leo miaka 33 imepita tangu atoe maneno hayo baada ya serikali wakati huo kuamua kupambana na uzembe makazini (uwajibikaji dunia), ulanguzi, rushwa na biashara ya magendo (siku hizi ufisadi).

Mpaka leo kauli yake inaishi, inatumika, inaamsha hali ya uzalendo na maadili ya taifa. Kama ilivyokuwa baada ya ujio wa Rais John Magufuli serikalini, wakati huo wanasiasa na viongozi wengi waandamizi walikuwa wameanza kuishi kinyume na misingi mikuu ya taifa hili, misingi mikuu ya chama chao na msingi mkuu wa uwajibikaji. Kama nchi tunakumbuka kifo cha mpendwa wetu huyo kwa yale mazuri aliyoifanyia Tanzania kwa ujumla wake.

Wasira anavyomwelezea Sokoine Jana, wakati akihojiwa na kituo kimoja cha redio, mwanasiasa mkongwe nchini, Stephen Wasira, alimwelezea Sokoine kama mchapa kazi na mzalendo wa kweli. Wasira ambaye alifanya kazi na Sokoine akiwa mbunge na kisha mkuu wa mkoa huku Sokoine akiwa Waziri na baadaye Waziri Mkuu, anataja mifano mingi inayothibitisha namna Sokoine alivyokuwa mchapa kazi huku akiwa tayari muda wowote kufa kwa ajili ya Tanzania.

“Wakati wa vita dhidi ya Nduli Iddi Amini, mimi nilikuwa mkuu wa mkoa wa Mara na Sokoine alikuwa Waziri wa Ulinzi. Mikoa ya Kanda ya Ziwa ikiwemo Mara ndio ilikuwa mstari wa mbele katika kukusanya wanamgambo wa kwenda kusaidia vitani, kutafuta vyakula na hata ng’ombe kwa ajili ya kusaidia vijana wetu waliokuwa mstari wa mbele. “Ilikuwa ni kawaida kwa Sokoine kukupigia simu usiku wa manane kutaka kujua mahala mlipofikia na kutofanya hata sisi muda mwingi kufanya kazi hata usiku na muda wote kuwa na majibu…

Mtu anapokupigia simu saa nane usiku maana yake ni nini? Bila sgaja ni kwmaba mtu huyu alikuwa halali,” anasema Wasira. Wasira anasema Sokoine alianzisha mfuko kwa ajili ya maendeleo ya Watanzania ambako alikuwa anaweka sehemu kubwa ya mshahara wake na kuishi kwa kutegemea mifugo aliyokuwa akifuga kijijini kwao, Monduli. Wasira anasema kumbukumbu zake zinaonesha kwamba kifo cha Sokoine ndicho kilimliza Mwalimu Julius Nyerere ambaye alikuwa akijiandaa kuachia madaraka ya uongozi wa nchi mwaka uliokuwa unafuata hadharani.

“Alikufa kaka yake ambaye alikua anampenda sana lakini Mwalimu hakutoka machozi (hadharani), hata alipokufa mdogo wake lakini kifo cha Sokoine kilimtoa machozi,” anasema. Baadhi ya nukuu zake “Ole wake kiongozi mzembe na asiye na nidhamu nitakayemkuta: Kiongozi wa siasa hana usalama wa aina yoyote. Usalama wake ni kudra ya Mungu na wananchi peke yake. Viongozi wazembe na wabadhirifu wahesabu siku zao. Labda tusiwajue. Hawa hatuna sababu ya kuwapa imani, kuwa tutawalinda kama vitendo vyao ni viovu” - 26 Machi 1983.

“Vijana leo wengi wana mali zaidi kuliko wazee waliofanya kazi miaka thelathini hadi arobaini. Lakini wanaitaka Serikali ndiyo iwaulize mali hiyo wameipata wapi. Hivi kwa nini mzazi asimuulize mwanawe, ‘mali hii umeipata wapi?” - 23 Oktoba 1983. “Wajibu wa kila Mtanzania, kila familia na kila anayekula ni kujilisha mwenyewe. Si wajibu wa Taifa kumlisha mtu. Unaweza ukasaidiwa unapopatikana na janga. Lakini kama hakuna janga ni wajibu wa kila mtu aweze kujitosheleza kwa chakula na atoe ziada kwa Taifa” - 4 Oktoba 1983.

“Serikali inasimamia bei, lakini Serikali yetu itakwenda mpaka itasimamia bei ya mhogo, dagaa na bei ya kila kitu? Haiwezekani, vitu vingine ni lazima vizalishwe kwa wingi ili bei yenyewe iweze kujirekebisha” - 24 Septemba 1983. “Juu ya suala hili la mapato kutolingana na matumizi ni kwamba tungependa kupunguza uongezaji wa wataalamu wasiohitajika katika Serikali na katika mashirika ya umma mpaka hapo hali yetu ya uchumi itakapokuwa katika hali nzuri” - 23 Oktoba 1982 “Katika nchi inayojali haki na usawa, majeshi hayana budi yawe ni chombo cha kulinda haki na maslahi ya walio wengi.

Na kamwe hayaruhusiwi kuwa ni chombo cha wachache wenye kujali nafsi zao na kusahau maslahi ya walio wengi” – 1 Februari 1977. Kifo chake Sokoine alifariki dunia Aprili 12, 1984 saa 10 jioni wakati akitoka Dodoma kwenda Dar es Salaam baada ya gari yake kupata ajali kwa kugongwa na gari lililokuwa likiendeshwa na mkimbizi kutoka Afrika Kusini aliyejulikana kwa jina la Dube.

Ajali hiyo ilitokea katika kijiji cha Wami Dakawa, sasa Wami Sokoine kilichoko umbali wa kilometa 40 kabla ya kufika Morogoro Mjini. Inasemekana kwamba, baada ya kikao cha NEC, karibu viongozi wakubwa wa kitaifa waliondoka mjini Dodoma kwa ndege, lakini yeye akasema wazi kuwa ni muumini wa sera ya kilimo ni uti wa mgongo wa taifa, hivyo alipendekeza kusafiri kwa njia ya barabara. Lengo lake lilikuwa ni kujionea mashamba makubwa na maendeleo ya kilimo kwa ujumla wakati akipita barabarani. Mchango wake kwa taifa Sokoine aliamini katika haki, usawa na uwajibikaji na pia aliamini katika siasa za Ujamaa zaidi ya siasa yeyote ile.

Aliamini kwamba maendeleo huja kwa watu kujituma kufanya kazi halali na bidii na kwamba ni vibaya sana kutajirika kwa njia ya kunyonya wengine kwa njia kama za ulanguzi na kadhalika. Pamoja na kuamini katika mabadiliko chanya, Sokoine alikuwa mzalendo hasa kwa taifa hili ambaye aliichukia kwa vitendo rushwa, uhujumu uchumi, ulanguzi na magendo. Alikuwa mtu wa vitendo na kamwe alikuwa si mtu wa kupenda kulalamikalalamika na ndio maana akaanzisha vita dhidi ya uhujumu uchumi, biashara ya ulanguzi na magendo.

Sokoine alitunza na kutukuza tamaduni za kiafrika na utaifa wa mtanzania. Alipotokea Sokoine Sokoine alizaliwa tarehe 1/8/1938 katika wilaya ambayo wakati huo ilijulikana kama Maasai Land ambayo kwa sasa inafahamika kama wilaya ya Monduli. Hii ni wilaya iliyoko mkoani Arusha. Alipata elimu yake ya msingi Monduli, akafaulu kujiunga na Shule ya Sekondari Umbwe, hii ilikuwa ni kuanzia mwaka 1948 mpaka 1958.

Alipomaliza elimu yake alijiunga rasmi na chama cha TANU 1961, kisha alipata nafasi ya kwenda nchini Ujerumani mwaka 1962 mpaka 1963 kusomea mambo ya uongozi na utawala. Aliporudi akateuliwa kuwa ofisa mtendaji wilaya ya Maasai Land na kutokana na ufanyakazi wake uliotukuka wilayani Monduli wananchi hawakuwa na budi kumchagua kuwa mwakilishi wao bungeni, yaani mbunge wa Monduli. Ufanisi wake kiutendaji ulionekana machoni mwa watendaji wakuu wa serikali na hususani kwa hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere.

Ndipo akachaguliwa kuwa Naibu wa Wizara ya Mawasiliano na Usafiri. Hii ilikuwa mwaka 1967. Kama hiyo haitoshi, nyota ya kiuongozi ilizidi kumwangazia ambapo mwaka 1972 aliteuliwa kuwa Waziri wa Usalama na kisha kuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga taifa kabla ya kuteuliwa kuwa Waziri Mkuu.

Sokoine alikuwa hasa mzalendo na alipenda siasa za ujamaa na hata kupelekea kumwomba Baba wa Taifa ruhusa ya kusimama kwa muda kama waziri mkuu ili aende kusomea zaidi mambo ya ujamaa nchi za nje. Hii ilikuwa mwaka 1981 ambapo Mwalimu alimruhsu na kiongozi huyo kwenda kusoma Yugoslavia. Mwaka 1983 alirudi na kuendelea na nafasi yake kama waziri mkuu mpaka Aprili 12, 1984 alipopata ajali hiyo.