Mtanzania kuchezesha Kombe la Dunia

MWAMUZI wa kike mwenye beji ya Shirikisho la Kimataifa (FIFA), Jonesia Rukyaa ni miongoni mwa waamuzi wa Afrika wanaotarajia kuchezesha michuano ya Kombe la Dunia ya wanawake itakayofanyika Ufaransa mwaka 2019.

Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi aliyasema hayo Dar es Salaam wakati akifunga kozi ya kati ya ukocha iliyowashirikisha wachezaji mbalimbali wa zamani, wadau na na waandishi wa habari.

Rukyaa hivi karibuni alishiriki katika mafunzo na mitihani ya kuchezesha michuano hiyo ya Kombe la Dunia na endapo atafanya vizuri katika mitihani hiyo iliyofanyika Ureno.

Malinzi alisema wakati Rukyaa akitarajia kuchezesha mashindano hayo, lazima wapambane ili timu ya taifa ya wanawake ‘Twiga Stars’ ifanye vizuri na kushiriki michuano hiyo.

Alisema Twiga Stars itaanza mchakato mwakani wa kushiriki michuano ya kufuzu Kombe la Mataifa ya Afrika kwa wanawake itakayofanyika Ghana.

“Rukyaa atatangulia Ufaransa, tunahitaji tufanye vizuri kwa wanawake, ambako kuna shida sasa, tukifuzu michuano ya Afrika tutakwenda kupambana ili tumalize katika tatu bora na kushiriki michuano hiyo ya dunia, “ alisema.

Alisema timu tatu za Afrika zitakazofanya vizuri kwenye michuano ya Afrika ya Ghana ndizo zitawakilisha kwenye michuano ya dunia.

Malinzi alisema soka la wanawake bado lina shida, kwani licha ya kuanzisha ligi na kupata mabingwa wapya Mlandizi Queens, hakuna michuano ya klabu bingwa Afrika.

Alisema kwa kuwa nchi za Ukanda wa Afrika Mashariki zina ligi zao, mpango uliopo ni kuishawishi Baraza la Soka Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) kuanzisha ligi ya wanawake kisha baadaye wapate nguvu kuishawishi Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kuanzisha klabu bingwa ya wanawake Afrika.

Bahati ya Rukyaa ilianza kufunguka mwaka jana alipochaguliwa kuchezesha baadhi ya mechi za wanawake katika michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika zilizofanyika Cameroon.

Katika hatua nyingine, Malinzi aliwaasa makocha wahitimu ambao hawatapata timu za kufundisha kuanzisha vituo vya soka kwa ajili ya kuendeleza na kukuza vijana wenye vipaji.

Jumla ya makocha 27 walihitimu mafunzo hayo ngazi ya kati yaliyoanza Februari 27 mwaka huu na kumalizika jana. Malinzi aliahidi kuwapa baadhi vifaa muhimu vya mazoezi kama ‘beaps’ 20 na ‘Cone’ 22 huku pia, akiwahimiza kujifunza teknolojia mpya ya kutambua wachezaji na mwenendo wa mchezo uwanjani.

Alisema uadilifu ni muhimu hivyo, makocha hao wanapaswa kuandaa vikosi vyao kwa ajili ya kucheza mpira na sio kuzungumza maneno mengi yasiyokuwa na tija katika michezo.

Mbali na hilo, Malinzi ameomba Watanzania kuwaombea kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF) utakaofanyika Alhamisi ya wiki hii ambapo Rais mstaafu wa TFF, Leodegar Tenga ni miongoni mwa wagombea.