Mayanga ataja Stars mpya

KOCHA Mkuu wa timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’, Salum Mayanga ametangaza kikosi cha wachezaji 26 kwa ajili ya maandalizi ya michezo ya kufuzu michuano ya Ubingwa wa Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ndani (Chan) na lile la Afcon.

Kikosi hicho ambacho hakina wachezaji wanaotokea Zanzibar kitakachoingia kambini Machi 19 kwa ajili ya mechi za kirafiki za kimataifa zilizopo kwenye kalenda ya FIFA.

Pia Mayanga hajawaita mabeki wa Yanga, Juma Abdul na Kevin Yondan, Mwinyi Aggrey Morris na David Mwantika wa Azam na kusema Haji Mwinyi na wachezaji wengine wa Zanzibar hajawaita kwa sababu anasubiri maamuzi ya kikao cha Shirikisho la Soka Afrika (CAF) Machi 16 kuhusu kuipa uanachama nchi hiyo.

Akizungumza wakati akitangaza kikosi cha Taifa Stars na benchi la ufundi, Mayanga alisema anaamini wachezaji wanaounda kikosi hicho wana uwezo na watafanya vizuri kwenye mashindano na michezo ya kirafiki “Mshambuliaji Mbaraka Yusuph wa Kagera Sugar nimemjumuisha baada ya kuwa kwenye kiwango bora na mabeki Shomari Kapombe, Hassan Kessy na Abdi Banda ni muda hawajaonekana Taifa Stars wakati wana uwezo mzuri, kwani kwenye timu zao wanafanya vizuri,” alisema Mayanga.

Kikosi kamili ni makipa Aishi Manula (Azam), Deogratius Munishi ‘Dida’ (Yanga) na Said Mohammed (Mtibwa Sugar).

Mabeki ni Shomary Kapombe, Gardiel Michael na Erasto Nyoni (Azam) FC, Hassan Kessy na Andrew Vincent (Yanga), Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ na Abdi Banda (Simba) na Salim Mbonde (Mtibwa Sugar).

Viungo ni Himid Mao, Salum Abubakar ‘Sure Boy’ na Frank Domayo (Azam), Jonas Mkude, Said Ndemla, Muzamil Yassin na Shiza Kichuya (Simba), Farid Mussa (DC Tennerife), Hassan Kabunda (Mwadui FC) na Simon Msuva (Yanga).

Washambuliaji ni Mbwana Samatta (KRC Genk, Ubelgiji), Thomas Ulimwengu (AFC Eskilstuna, Sweden), Ibrahim Hajib (Simba), Mbaraka Yussuf (Kagera Sugar) na Abdulrahman Mussa (Ruvu Shooting).

Benchi la ufundi ni Patrick Mwangata ambaye atakuwa kocha msaidizi pia kocha wa makipa, meneja ni Danny Msangi, mtunza vifaa ni Ally Ruvu, daktari Richard Yomba na daktari wa viungo ni Gilbert Kigadya.

Mayanga alisema timu itacheza mechi mbili za kujipima nguvu katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam dhidi ya Botswana Machi 25 na Burundi Machi 28.

Mayanga alisema mechi hizo ni maandalizi ya michezo ya kufuzu michuano ya ubingwa wa Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wanaocheza ndani (CHAN) na Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON).

Taifa Stars itacheza na Rwanda kuwania tiketi ya CHAN mwakani nchini Kenya mchezo utakaochezwa Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam kati ya Julai 14 na 16 kabla ya kurudiana Uwanja wa Amahoro, Kigali kati ya Julai 21 na 23.

Ikifanikiwa kuitoa Rwanda, Tanzania itacheza na mshindi kati ya Uganda na ama Sudan Kusini au Somalia katika raundi ya tatu, mechi ya kwanza itachezwa kati ya Agosti 11, 12 na 13 na marudiano kati ya Agosti 18, 19 na 20, mwaka huu.