Yanga mambo safi

SAFARI ya Yanga kwenda Lusaka, Zambia, kwa ajili ya mechi dhidi ya Zanaco ya huko imenogeshwa baada ya wachezaji hao kulipwa mishahara ya miezi miwili kati ya mitatu waliyokuwa wanadai.

Yanga inatarajiwa kuondoka kesho kwenda Lusaka kwa ajili ya mechi ya marudiano ya Ligi ya Mabingwa itakayochezwa mwishoni mwa wiki hii.

Mechi ya kwanza iliyofanyika wiki iliyopita timu hizo zilitoka sare ya bao 1-1. Habari za uhakika kutoka kwa mmoja wa wachezaji wa Yanga zilisema wachezaji wote walilipwa fedha zao jana tayari kwa safari hiyo.

Awali, Katibu Mkuu wa Yanga Charles Mkwasa alikiri klabu hiyo kukumbwa na ukata baada ya Mwenyekiti wao, Yusuf Manji kupata matatizo dhidi ya serikali hali iliyofanya klabu hiyo kukosa fedha za kulipa mishahara ya baadhi ya watumishi wake, kwa vile wanalipwa na kampuni ya Quality inayomilikiwa na Manji.

Mkwasa alisema hivi karibuni kwamba hata kama Mwenyekiti wao amepatwa tatizo, Yanga ni klabu kubwa hivyo haiwezi kushindwa kulipa mishahara ya watumishi wake.

Aidha habari zaidi zinasema huenda ‘jeuri hiyo ya fedha kwa klabu hiyo ni kutokana na kulipwa fedha za haki ya matangazo za Azam Media ilizozikataa kwa takriban miaka mitatu sasa.

Azam hutoa Sh milioni 100 kwa timu za Ligi Kuu kwa ajili ya kurusha mechi zao, Yanga ilikataa kuchukua fedha hizo ikidai ni ndogo. Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi Ahmad Yahaya aliliambia gazeti hili kuwa Yanga walikwenda kuomba fedha zao na kuambiwa waandike barua rasmi.

“Wameandika na tumeshawalipa fedha zao Sh milioni 100, tutawalipa kwa awamu,” alisema.

“Tumelipwa tunashukuru maana kweli tulikuwa na hali mbaya na kwa vile na sisi tuna familia zinatutegemea,” alisema mmoja wa wachezaji hao.

Kulipwa huko mishahara ni utekelezaji wa ahadi za Mkwasa ambaye hivi karibuni alisema ataendelea kulipa malimbikizo kwa wachezaji wanaodai fedha zao za mishahara taratibu.