Ahmad Rais mpya CAF

Rais wa Chama cha Soka Madagascar, Ahmad Ahmad amechaguliwa kuwa Rais mpya wa Shirikisho la Soka Barani Afrika(CAF) baada ya kumbwaga mkongwe Issa Hayatou aliyekuwa akishika wadhifa huo kwa miaka 29.

Ahmad ameshinda uchaguzi uliofanyika mji mkuu wa Ethiopia, Addis Ababa kwa kupata kura 34 huku Hayatou akiambulia 20.

Ripoti zimesema baada ya matokeo kutangazwa wajumbe walishangilia huku wakijimwaga katikati ya ukumbi wa mkutano.

Ahmad mwenye umri wa miaka 57 aliwahi kucheza soka na ana elimu ya ukocha.

Alichaguliwa kuwa Rais wa chama cha Soka Madagascar mwaka 2013.

Akizungumza na waandishi wa baada ya uchaguzi huo Ahmad alisema, "Unapojaribu kufanya kitu, una maana unaweza kukifanya, "Kama siwezi kukifanya, siwezi kujaribu." Hayatou ameongoza CAF tangu 1988.