Zanzibar kimeeleweka Caf

ZANZIBAR imepata uanachama rasmi wa Shirikisho la Soka Afrika (Caf) katika mkutano mkuu wa shirikisho hilo uliofanyika Addis Ababa, Ethiopia.

Katika uchaguzi huo, Zanzibar ilipigiwa kura za ndio kwa kishindo na sasa inakuwa mwanachama wa 55 wa Caf.

Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi ndiye aliyepeleka pendekezo hilo Caf na kupigiwa kura na wajumbe 54.

Kwa muda mrefu Zanzibar ilikuwa ikipambana kupata nafasi hiyo ambapo sasa itakuwa ikisimama yenyewe kwenye michuano ya kimataifa ya Caf na pia kupata misaada moja kwa moja kutoka kwa shirikisho hilo.

Awali, Zanzibar ilitambulika kama Tanzania na hivyo kuwa na timu moja ya taifa iliyochanganyika wachezaji wa Bara na Zanzibar kwenye michuano ya kimataifa.

Hii ikafanya kuwe na Ligi ya Muungano iliyokuwa ikishirikisha timu nne, mbili zilizoshika nafasi ya juu kwenye ligi ya bara na mbili kwenye ligi ya Zanzibar ambapo bingwa aliwakilisha nchi kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa.

Mwanzoni mwa miaka ya 2000, Zanzibar ilipata uanachama wa muda wa Caf ambapo iliruhusiwa kushirikisha klabu zake kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho Afrika na ndipo ligi ya Muungano ikafa kwa vile haikuwa na maana tena.

Aidha kwa upande wa timu za Taifa, Zanzibar sasa itashirikisha timu zake yenyewe kwenye michuano ya Caf bila kuchanganyika na timu ya taifa ya Bara, Taifa Stars.

Zanzibar imekuwa ikishirikisha timu yake yenyewe kwenye michuano ya Baraza la vyama vya soka kwa nchi za Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) kwa vile ni mwanachama anayejitegemea kwenye baraza hilo.