Ndolanga, Rage wamcheka Hayatou

VIONGOZI wa zamani wa kilichokuwa Chama cha Soka Tanzania (FAT) sasa TFF, Muhidini Ndolanga na Ismail Rage wamefurahia anguko la rais wa Shirikisho la Soka Afrika (Caf), Issa Hayatou, wakidai amevuna alichopanda.

Hayatou aliangushwa na rais wa Chama cha Soka Madagascar, Ahmad Ahmad katika uchaguzi mkuu wa Shirikisho hilo uliofanyika mjini Addis Ababa, Ethiopia na kumaliza utawala wa miaka 29 ya Mcameroon huyo kwenye soka la Afrika.

Ahmad alishinda uchaguzi huo kwa kura 34 kati ya 54 zilizopigwa.

Ndolanga na Rage waliwahi kufanya kazi na Hayatou walipokuwa viongozi wa FAT kwa muda mrefu kabla ya Rage aliyekuwa katibu mkuu kushindwa na Michael Wambura kwenye uchaguzi wa mwaka 2011 na kurejea tena kama makamu wa pili wa rais wa TFF katika uchaguzi wa mwaka 2014 huku Ndolanga aliyekuwa mwenyekiti akishindwa na Leodegar Tenga kwenye uchaguzi wa mwaka huo.

Wakizungumza na gazeti hili jana kwa nyakati tofauti, viongozi hao walisema wana matumaini makubwa na rais mpya, Ahmad kwamba ataongoza taasisi hiyo bila ubaguzi kama ilivyokuwa kwa Hayatou.

“Nilifanya nae kazi na mimi niliondoka yeye (Hayatou) akabaki simuonei huruma hata kidogo kwa sababu ameyataka mwenyewe hasa alipofanya watu wajinga kwa kubadilisha kanuni, kwamba wajumbe wa kamati ya utendaji ya Caf ndio pekee wanaoruhusiwa kugombea, maamuzi hayo ni ya kijinga kabisa ningekuwa na uwezo wa kuifuta kanuni hiyo ningeifuta,” alisema Ndolanga.

Alisema katika uongozi usiongoze mpaka watu wakuchoke na kuondoka kwa aibu na hicho ndicho kilichotokea kwa Hayatou.

“Kaongoza miaka mingi sana na hili liwe funzo kwa viongozi wetu wa soka hapa nyumbani, kwamba vipindi viwili vya miaka minne minne vinatosha kabisa kufanya mabadiliko kwenye mpira haina haja kuongoza miaka mingi,” alisema.

Kwa upande wa Rage alisema, Amefurahi kuondoka kwa ‘mbuyu’ huo sababu hakuwa na msaada kwa nchi nyingi za Afrika hasa za Afrika Mashariki, Kati na Kusini.

“Nchi zetu hazikupewa msaada kabisa alikuwa akiangalia Magharibi tu, mfano kwenye kamati ndogondogo za Caf kajaza wa Magharibi tu, alikuwa mbaguzi sana yule bwana na alikuwa mroho wa madaraka pia, na ukitaka kuamini hilo angalia fainali za vijana chini ya umri wa miaka 17 zilipangwa kufanyika Madagascar, lakini alivyoona rais mpya ametangaza kugombea yeye akaziondoa akazipeleka Gabon, natamani Ahmad azirudishe tena Madagascar… yaani katika watu waliofarijika Hayatou kuondoka pale, mimi ni mmoja wao,” alisema Rage.

Matokeo ya uchaguzi wa jana yanamaanisha kubadilisha utawala wa soka kwa mara ya kwanza tangu Mcameroon Hayatou alipochukua madaraka mwaka 1988.

Ahmad, ambaye alionekana kukubalika, anakuwa rais wa saba wa Caf ndani ya miaka 60 ya historia ya shirikisho hilo. Matokeo hayo yalipokewa kwa shangwe nyingi na wajumbe wa mkutano mkuu wa Caf ambapo Ahmad alibebwa mabegani na baadhi ya wajumbe na kumpeleka mbele ya ukumbi baada ya matokeo kutangazwa.

Ahmad mwenye umri wa miaka 57 alisema: “Unapojaribu kufanya kitu, unamaanisha kwamba unaweza, kama siwezi nisingegombea. “Huu ni ushindi mtamu, unapofanya kazi kwa bidii kwa miaka na miezi mingi na ukafanikiwa, ni jambo bora”.

Ahmad, ambaye alikuwa bosi wa soka Madagascar mwaka 2003, ataongoza shirikisho hilo kwa miaka minne na ameahidi kuendesha taasisi hiyo kisasa na kufanya mambo kwa uwazi zaidi.

Kazi yake ya kwanza, alisema mapema baada ya kuchaguliwa jana ni kutangaza kanuni mpya na pia kuhakikisha zinafuata na viongozi wa soka wa Afrika.

Kuondoka kwa Hayatou ni mabadiliko makubwa kwa soka ya Afrika na kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 70 pia atapoteza nafasi yake Fifa.

Aliwahi kupata ushindani kwenye nafasi hiyo mara mbili na mara zote alikuwa akiibuka na ushindi mnono. Lakini safari hii alishinda kwa kura 20 pekee, na kuondoa matumaini yake ya kuongoza kwa kipindi cha nane na kuongoza kwa zaidi ya miongo mitatu.

“Issa Hayatou amefanya mengi kwa soka ya Afrika lakini ni wakati sasa kukaa pembeni,” alisema George Afriyie, makamu wa rais wa chama cha soka cha Ghana. Rais wa chama cha soka cha Liberia Musa Bility aliongeza: “Afrika imefanya mabadiliko makubwa ambayo ilikuwa tayari kuyafanya”.

Akizungumzia uchaguzi huo, rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi amempongeza Ahmad kuukwaa urais na kumuahidi shirikisho lake litampa ushirikiano wa kutosha.