Diamond, Kiba kurekodi wimbo wa Serengeti Boys

KATIKA kuhakikisha watanzania wanapata hamasa ya kuishangilia timu ya soka ya Taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 17, ‘Serengeti Boys’ wanamuziki maarufu wa Bongo Fleva, Nassib Abdul ‘Diamond’ na Ali ‘King’ Kiba watarekodi wimbo maalumu wa kuhamasisha kampeni za kuchangia timu hiyo kuelekea Gabon.

Serengeti Boys imefuzu fainali za vijana za Afrika zitakazofanyika kwenye mji wa Libreville, Mei 14 mwaka huu, ikiwa ni mara ya kwanza kwa Tanzania kushiriki kwenye fainali hizo kwa vijana wa umri huo.

Mjumbe wa kamati ya hamasa ya timu hiyo, Maulid Kitenge alisema mbele ya waandishi wa habari Dar es Salaam kuwa tayari ala za wimbo huo utakaoimbwa na Kiba na Diamond kwa kushirikiana na wasanii Mwasiti, Darassa, Vanessa Mdee na Msagasumu, imeshatengenezwa na wasanii wametumiwa kwa ajili ya kuingiza sauti.

“Ali Kiba yuko Marekani lakini amekwishatumiwa ala ili aingize sauti ila Diamond yupo nchini na ametumiwa na wameahidi kufanya hivyo mara moja na kurejesha kazi hizo, ili na wasanii wengine waingize sauti zao,” alisema Kitenge.

Alisema wimbo huo utakapokamilika Watanzania wanaweza kuununua kama mwito wa kwenye simu zao pia utasambazwa kwenye vyombo vyote vya habari kwa ajili ya kupigwa kuhamasisha Watanzania.

Kiba na Diamond hawajawahi kufanya wimbo wa pamoja na kwa muda mrefu imekuwa ikidaiwa wana bifu ingawa Diamond juzi alisema hana tatizo na mwenzake huyo na yupo tayari kufanya naye kazi.

Naye Mwenyekiti wa Kamati ya hamasa ya Serengeti Boys ambayo ipo chini ya serikali, Charles Hilary alisema wameweka mikakati ya kukusanya fedha kwa ajili ya kuisaidia timu hiyo.

Serengeti Boys inahitaji Sh bilioni moja kushiriki michuano hiyo.

“Tuliteuliwa mwezi uliopita na ni muda mfupi sana kabla ya mashindano kuanza lakini tumekutana na tumeweka mikakati ya kupata kiasi cha bilioni moja na kauli mbiu ni ‘Kutoka Gabon kwenda India kwenye fainali za dunia’”, alisema Hillary.

Timu nne zitakazoshika nafasi za juu kwenye michuano hiyo zitafuzu fainali za kombe la dunia kwa vijana wa umri huo zilizopangwa kufanyika India Novemba mwaka huu.

Hillary alisema msaada wanaouhitaji siyo fedha tu bali vyakula, usafiri wa ndege na vifaa kwa ajili ya kambi inayotarajiwa kuwa Morocco.

Aidha alisema njia ambazo wameoanisha kupata fedha ni kupitia kila halmashauri kuchangia kiasi cha Sh milioni moja na namba ya simu ambayo kila mtanzania anaweza kuweka fedha na kupiga akachangia.

“Kila mtanzania anaweza kuchangia kuanzia Sh 500 na kwa kuzingatia wingi wa watanzania tutakuwa tumepata fedha za kutosha na pengine kubaki kwa ajili ya kuipeleka timu hiyo India kwani tunaamini tutafuzu,” alisema Hillary.

Pia Hillary alisema kiwanda cha bia cha Serengeti na Mamlaka za Hifadhi za Taifa (TANAPA) wameonesha nia ya kushirikiana na kamati kutokana na jina la timu hiyo kufanana na moja ya bidhaa/ huduma zao.

Naye mjumbe wa kamati hiyo, Beatrice Singano alisema wachangiaji wanaweza kuchangia kwa kutumia mitandao ya simu ya Airtel, Tigo na Vodacom na kulipia kwa Selcom ni namba 223344.