Yanga pumzi muhimu leo

WAWAKILISHI wa Tanzania katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika Yanga leo watakuwa ugenini wakitafuta ushindi katika mchezo wa marudiano dhidi ya Zanaco utakaochezwa Lusaka, Zambia.

Yanga itashuka dimbani ikitoka kulazimishwa sare ya bao 1-1 dhidi ya mabingwa hao wa Zambia katika mchezo wa kwanza uliochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Mshindi wa mchezo huo atasonga mbele kwa hatua ya makundi huku atakayefungwa atashuka katika mashindano ya Shirikisho la Afrika.

Tayari timu hizo zimefahamiana vizuri baada ya kuoneshana ubabe kila mmoja akicheza kwa nguvu nyingi katika mchezo wa kwanza zikifahamiana pia mapungufu yao.

Kutokana na matokeo ya mchezo wa kwanza, Yanga inapewa uwezekano mdogo wa kusonga mbele baada ya kucheza kwa kiwango cha chini, ikionekana kuzidiwa na Zanaco, lakini inaweza kupenya endapo itarekebisha makosa ya awali.

Kocha Msaidizi Juma Mwambusi kabla ya kwenda Zambia alisema hautakuwa mchezo rahisi kwao lakini ni lazima wapambane na kuhakikisha wanapata matokeo mazuri.

Hatahivyo, Yanga itawakosa wachezaji wake tegemeo ambao ni majeruhi Donald Ngoma na Amis Tambwe. Wengine ambao walibaki Dar es Salaam ni Beno Kakolanya, Malimi Busungu, Antony Matheo, Pato Ngonyani na Yusufu Mhilu.

Wachezaji tegemeo katika kikosi cha Yanga kwa sasa ni Simon Msuva, Thaban Kamusoko, Deus Kaseke, Haruna Niyonzima, Obrey Chirwa na Deogratius Munishi ambao hutarajiwa kuwaongoza wengine katika kufanya vizuri.

Msimu uliopita katika raundi kama hii, Yanga ilicheza na Al Ahly kwenye Uwanja wa Taifa na kulazimishwa sare ya bao 1-1.

Katika mchezo wa marudiano uliochezwa Misri ikafungwa mabao 2-1 na kuangukia katika Kombe la Shirikisho ambalo ilicheza hatua ya makundi.

Bado Yanga wana kazi ya kuhakikisha kuwa wanafuta rekodi mbaya ya nyumbani na ugenini kwa kupambana na kupata matokeo mazuri.

Kwa upande wa Kocha wa Zanaco, Numba Mumamba kabla ya kurudi kwao Zambia alisema anawasubiri Yanga kuwamaliza nyumbani kwao.

Alisema wanajua mapungufu ya Yanga yako upande gani wanachosubiri ni kumaliza kila kitu katika mchezo, kwani nia yao ni kusonga mbele.

Mchezaji aliyekuwa msumbufu kwenye ngome ya Yanga katika mchezo wa kwanza alikuwa ni Attram Kwake aliyeisawazishia timu yake bao baada ya Yanga kuongoza kipindi cha kwanza 1-0.

Pia, Zimiseleni Moyo alikuwa akiwapoteza Kamusoko na Kelvin Yondani katika mchezo wa kwanza.