Yanga kujipoza kwa Polisi

YANGA inatarajia kucheza mechi ya kujipima nguvu dhidi ya Polisi Dodoma Machi 25 mwaka huu kwenye uwanja wa Jamhuri Dodoma.

Katika barua ya Katibu Mkuu wa Yanga Charles Mkwasa kwenda kwa Chama cha soka Dodoma (Dorefa) alisema wamekubali mwaliko wa kucheza mechi hiyo ili kuunga mkono harakati za serikali kuhamia Dodoma.

“Tumekubali kucheza mchezo huo hivyo Dorefa mnaweza kuendelea na maandalizi,” ilisema barua hiyo ya Mkwasa. Hiyo itakuwa mechi ya pili kwa Polisi Dodoma kucheza na mmoja ya vigogo vya soka nchini, wiki iliyopita ilicheza mechi ya kirafiki na Simba ambapo ilifungwa mabao 3-0.

Akizungumza na gazeti hili jana Katibu Mkuu wa Polisi Dodoma, Michael Mtebene alisema amefurahi uongozi wa Yanga kukubali timu yao kucheza nao kwani inasaidia kuinua soka mkoani kwao.

“Pamoja na kujenga umoja na undugu kupitia michezo kitendo cha kupata michezo ya kirafiki na Yanga na Simba kunaamsha ari ya soka kwa mashabiki,” alisema Mtebene.

Yanga inakwenda kucheza mechi hiyo ikiwa siku chache baada ya kutolewa kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa na Zanaco baada ya kutoka suluhu juzi, lakini ikitupwa nje ya bao la ugenini baada ya kulazimishwa sare ya bao 1-1 katika mechi ya kwanza iliyochezwa nyumbani kwenye uwanja wa Taifa Dar es Salaam mwishoni mwa wiki. Yanga sasa inajipanga kucheza kombe la Shirikisho Afrika.