Kocha kuisuka Yanga upya

KOCHA Msaidizi wa Yanga, Juma Mwambusi amesema haikuwa kazi rahisi kutinga makundi Ligi ya Mabingwa wa Afrika na kuangukia katika Kombe la Shirikisho.

Yanga mwishoni mwa wiki ilitolewa katika Ligi ya Mabingwa wa Afrika baada ya kutoka suluhu na Zanaco nchini Zambia baada ya kutoka sare ya 1-1 katika mchezo wa kwanza jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na gazeti hili Mwambusi alisema pamoja na kutolewa katika mashindano hayo, lakini sasa wanajenga Yanga mpya na yenye ushindani.

“Michuano ilikuwa migumu na tumejifunza mengi tangu tumeanza kushiriki na mpaka sasa tunaondolewa, tumejipanga kukiboresha kikosi chetu katika msimu ujao ili tuweze kufanya vizuri zaidi,“ alisema.

“Licha ya kushindwa kufuzu hatua ya nusu fainali tumejifunza mengi ikiwepo nidhamu ya mchezo na nidhamu ya mchezaji husika uwanjani,” alisema Mwambusi.

Mwambusi alisema wamejenga msingi mzuri wa timu kitaifa na kimataifa, hivyo watanzania waelewe wamejenga Yanga mpya na ya ushindani.

Kwenye hatua ya awali Yanga iliitoa Ngaya de Mbe ya Comorro kwa mabao 6-1 na sasa imeangukia kucheza Kombe la Shirikisho.