Tulieni, ushindi upo - Mwambusi

KOCHA msaidizi wa Yanga, Juma Mwambusi amewataka mashabiki wa timu hiyo na watanzania kwa ujumla kuwa watulivu na kwamba wanakwenda Algiers kushinda.

Yanga inatarajiwa kucheza na MC Alger ya Algeria kesho katika mechi ya mchujo kuingia makundi kwenye michuano ya kombe la Shirikisho Afrika.

Katika mechi hiyo, Yanga inahitaji sare ili isonge mbele baada ya kushinda bao 1-0 katika mechi ya kwanza iliyochezwa wiki iliyopita kwenye uwanja wa Taifa Dar es Salaam.

Akizungumza saa chache kabla ya kuondoka jana, Mwambusi alisema wamejipanga kushinda mechi hiyo hivyo mashabiki wao hawana haja ya kuwa na wasiwasi.

“Tunajua wapinzani wetu watatugeuka kwamba walivyocheza nyumbani itakuwa tofauti na kwao, lakini sisi tumejipanga kupata matokeo mazuri Jumamosi (kesho),” alisema.

Yanga iliondoka jana kuelekea Algiers kwa mafungu, kundi la kwanza likiondoka saa 10 jioni na la pili lilitarajiwa kuondoka saa mbili usiku.

Wachezaji walioondoka saa 10 jioni na ndege ya Emirates ni Nahodha Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Hassan Kessy, Said Makapu, Simon Msuva, Geoffrey Mwashiuya, Juma Mahadhi na Amissi Tambwe.

Aidha kundi hilo pia liliondoka na benchi la ufundi kocha mkuu wa Yanga, George Lwandamina, Mwambusi, Kocha wa mazoezi ya utimamu wa mwili, Noel Mwandila, kocha wa makipa, Juma Pondamali, Meneja Hafidh Ally, Daktari Edward Bavu na mchua isuli, Jacob Onyango.

Kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa Yanga, Charles Mkwasa, kundi hilo la kwanza liliondoka kupitia Dubai na kundi la pili lililotarajiwa kuondoka saa mbili usiku lilipitia Istanbul, Uturuki.

Kundi hilo litakuwa na wachezaji Deogratius Munishi ‘Dida’, Beno Kakolanya, Juma Abdul, Oscar Joshua, Haji Mwinyi Mngwali, Andrew Vincent ‘Dante’, Vincent Bossou, Kelvin Yondani, Thabani Kamusoko, Haruna Niyonzima, Deus Kaseke, Emmanuel Martin na Donald ngoma.