Yanga pumzi muhimu leo

WAWAKILISHI wa Tanzania katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika Yanga leo wana kibarua kizito cha kusaka ushindi katika mchezo wa mwisho wa mtoano dhidi ya MC Alger utakaochezwa usiku Algeria.

Yanga itashuka dimbani ikiwa na kumbukumbu ya ushindi wa bao 1-0 iliyopata wiki iliyopita katika mchezo uliochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara wanahitaji sare au ushindi wowote kuwawawezesha kusonga mbele hatua ya makundi.

Ikiwa watafanikiwa basi watajiwekea historia nyingine mpya baada ya mwaka uliopita kufanikiwa kuishia hatua hiyo.

Kikosi hicho kitamkosa mchezaji tegemeo Obrey Chirwa ambaye alibaki Dar es Salaam kutokana na matatizo yake na klabu.

Lakini pengine uwepo wa Donald Ngoma, Amis Tambwe, Thaban Kamusoko, Haruna Niyonzima kwa kushirikiana na wengine ukasaidia timu hiyo kusonga mbele.

Yanga imekuwa na utofauti mkubwa katika mechi za ugenini licha ya kupoteza mara nyingi, lakini imekuwa ikicheza mchezo wa nguvu kuliko inavyokuwa nyumbani japokuwa imekuwa haisaidii.

Wanakutana na MC Alger ambayo imekuwa ikijitahidi katika michezo ya nyumbani kufanya vizuri.

Katika michezo iliyopita timu hiyo ya Algeria ilifungwa 2-1 dhidi ya Benchem United ya Ghana kisha nyumbani kwao katika mchezo wa marudiano wakashinda 4-1.

Aidha, walifungwa mabao 2-1 ugenini na nyumbani kwao wakashinda 2-0 dhidi ya Renaisance hiyo yote ikiwa ni michezo ya awali ya michuano hiyo ya Shirikisho.

Kwa kuangalia mechi hizo inaonyesha wazi kuwa ni timu yenye nguvu hasa inapokuwa mbele ya mashabiki wake kwenye uwanja wao wa nyumbani.

Lakini pia, kwa kuangalia mchezo dhidi ya Yanga walikuwa wakicheza kwa kujilinda zaidi wakiamini kwamba kila kitu watamaliza kwao.

Wachezaji wa kuogopwa ni Awady Said, Goveri Kaled na Nekkache Hichem, ambao wanaonekana nmi hatari zaidi.

Yanga iliondoka juzi kwenda Algeria huku kocha wake msaidizi Juma Mwambusi akit- amba kuwa wanakwenda kumalizia kazi na kuwataka mashabiki wa timu hiyo na Watanzania kwa ujumla kuwa watulivu.