`Simba ni ushindi tu Mwanza’

VINARA wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Simba wametamba kuendeleza vichapo kwa timu za Mwanza wakati leo watakapocheza dhidi ya Toto Africans kwenye Uwanja wa CCM Kirumba hapa.

Simba Jumatatu nusura itolewe nishai baada ya kuwa nyuma kwa mabao 2-0 hadi dakika 10 za mwisho lakini walisawazisha na kuibuka na ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Mbao FC kwenye uwanja huohuo.

Kocha msaidizi wa timu ya soka ya Simba SC Jackson Mayanja ameahidi ushindi dhidi ya Toto Africans.

Akizungumza wakati wa mazoezi wa timu yake jana katika Uwanja wa CCM Kirumba,Mayanja alisema timu yake iko tayari kwa ajili ya mchezo huo na kuhakikisha wanapata ushindi.

“Maandalizi yamekamilika vizuri sana na tunangoja mechi ifike tuweze kuondoka na alama tatu jambo ambalo ni muhimu kwetu ili kuweza kuhakikisha tunasonga mbele na kuchukua ubingwa, “ alisema Mayanja.

Mchezaji huyo wa zamani wa timu za Lowi FC,Esperance,KCC FC na El Masry alisema timu yao imerekebisha makosa yao na wapo tayari kwaajili ya ushindi.

Akielezea kuhusiana na rufaa yao dhidi ya Kagera Sugar,kocha huyo wa zamani wa Uganda Cranes,Coastal Union, Bunamwaya FC na URA alisema timu ya Kagera Sugar walifanya makosa makubwa sana kumchezesha Mohamed Fakhi jambo liliopelekea wao kuadhibiwa.

Mayanja alisema mchezaji Joseph Mwanjali atakosa mechi ya leo kutokana na majeruhi ila wachezaji wengine wote wako safi.

Msimamizi mkuu wa kituo hiki Juma Msaka ambaye pia ni katibu mkuu wa chama cha soka wilaya ya Ilemela(IDFA) alisema ataendelea vyema na usimamizi wake mzuri kuhakikisha wana hakikisha usalama wa mashabiki na mali zao uwanjani kuwa upo vyema.

Mchezaji huyo wa zamani wa Mwatex alisema uongozi wao umejipanga vyema kuhakikisha wanawakamata watu wote watakaouza tiketi feki.

Msaka alisema tiketi zitapatikana leo katika uwanja wa Nyamagana, Pasiansi na shule ya msingi Kitangiri. Msaka amewaomba wadau na wapenzi wa soka kuwahi uwanjani ili kuepuka msongamano wa watu getini.

Msaka alisema bei za tiketi ni elfu 5000 kwa mzunguko,Jukwaa kuu ni 10,000/- na 20,000 kwa viti maalumu.

Yanga ambao leo wana kibarua Algeria katika mchezo wa mchujo wa Kombe la Shirikisho Afrika, inashika nafasi ya pili katika msimamo wa ligi hiyo ikiwa na pointi 56 lakini wana mchezo mmoja mkononi.