Yanga yamewakuta

KIPIGO cha mabao 4-0 kutoka kwa MC Alger mjini Algiers juzi kiliichanganya Yanga na kuachwa na ndege baada ya kuchelewa kufika uwanja wa ndege kwa safari ya kurudi nyumbani.

Yanga imeaga rasmi michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kufungwa idadi hiyo ya mabao na kutolewa kwa jumla ya mabao 4-1 baada ya kushinda bao 1-0 nyumbani wiki mbili zilizopita.

Akizungumza kwa simu Katibu Mkuu wa Yanga, Charles Mkwasa alikiri kutokea kwa tukio hilo ambapo alisema ndege ilichelewa kwa dakika chache kutoka ilipochezewa mechi mpaka uwanja wa ndege kutokana na foleni.

Hata hivyo alisema walishafanya marekebisho na kikosi hicho sasa kilitarajiwa kuwasili saa 11 alfajiri ya leo badala ya usiku wa jana.

Wachezaji walioachwa na ndege ni Deogratius Munishi ‘Dida’, Beno Kakolanya, Juma Abdul, Oscar Joshua, Haji Mwinyi Mngwali, Andrew Vincent ‘Dante’, Kelvin Yondani, Thabani Kamusoko, Haruna Niyonzima, Deus Kaseke, Emmanuel Martin na Donald Ngoma.

Yanga inarudi kwa makundi kama ilivyoondoka. Kundi lingine ni lile linalotarajiwa kuondoka keshokutwa kupitia Dubai likiwa na nahodha wake Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Hassan Kessy, Said Juma ‘Makapu’, Simon Msuva, Geoffrey Mwashiuya, Juma Mahadhi na Amissi Tambwe.

Pia katika kundi hilo kulikuwa na viongozi wa benchi la ufundi chini ya kocha mkuu George Lwandamina, Juma Mwambusi (kocha msaidizi), Kocha wa viungo Noel Mwandila, kocha wa makipa, Juma Pondamali, Meneja Hafidh Ally, Daktari Edward Bavu na Mchua Misuli, Jacob Onyango.

Timu hiyo sasa inakabiliwa na kibarua cha kutetea mataji yake lile la Ligi Kuu na lile la Kombe la Shirikisho, FA. Itacheza mechi ya robo fainali ya Kombe la FA dhidi ya Prisons mwishoni mwa wiki hii kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam.

Tayari Simba, Azam na Mbao zimeshafuzu hatua hiyo. Kwa upande wa taji lake la Ligi Kuu, Yanga inakimbizana kwa karibu na hasimu wake Simba inayoongoza kwa pointi 62.

Yanga ipo nafasi ya pili ikiwa na pointi 56 lakini ikiwa na michezo miwili kibindoni.