Mayanja aipa saluti Toto

KOCHA msaidizi wa Simba SC, Jackson Mayanja amekipongeza kikosi chake kwa kutoka sare ya bila kufungana dhidi ya Toto Africans akisema mechi hiyo ilikuwa ngumu.

Simba imemaliza michezo yake ya Kanda ya Ziwa na sare hiyo iliyoipa pointi moja na hivyo kuwa kileleni kwa pointi 62 ikibakiza michezo mitatu imalize ligi.

Timu hiyo inayosaka ubingwa kwa mwaka wa tano sasa, imebakiza mechi dhidi ya African Lyon, Stand United na Mwadui, zote ikizicheza kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam.

Akizungumza baada ya kumalizika mechi hiyo iliyochezwa kwenye uwanja wa CCM Kirumba Mwanza, Mayanja alisema hana budi kuwapongeza wachezaji wake kwani wapinzani wao walicheza kwa kuwakamia na rafu nyingi.

“Nashukuru tumetoka salama hata hivyo, tunajipanga kwa mechi za mwisho Dar es Salaam tukiamini bado tupo kwenye nafasi nzuri ya kutwaa ubingwa,” alisema.

“Mchezo na Toto ulikuwa mzuri sana tulitaka kupata alama zote tatu lakini hatukuweza kupata, TotoAfricans walicheza kwa kutupania muda wote,” alisema.

Simba inarudi kutoka Kanda ya Ziwa ikiambulia pointi tatu.

Baada ya kushinda rufaa yake ya kupinga Kagera kumtumia Mohamed Fakhi katika mechi dhidi yao ambapo alicheza akiwa na kadi tatu za njano. Hivyo, pamoja na kufungwa mabao 2-1.

Lakini imepata pointi hizo ambapo jana bosi wa bodi ya Ligi Boniface Wambura aliwaandikia barua rasmi kuwafahamisha ushindi wa rufaa hiyo.

Pointi nyingine tatu ilizipata katika mechi dhidi ya Mbao, ambapo ilishinda mabao 3-2 baada ya kuwa nyuma kwa 2-0 kwa dakika 82 kabla ya kuibuka na kupata ushindi huo.

Kwa upande wa Toto, haiko kwenye nafasi nzuri pamoja na kupata pointi hiyo, bado ipo kwenye ukanda wa kushuka daraja ikiwa na pointi 26.

Kocha wake Fulgence Novatus alisema timu yake ilicheza vyema dhidi ya Simba na kuzuia mashambulizi ndio maana wakapata sare hiyo.

Alisema timu yao itaendelea kufanya mazoezi kwa kujituma zaidi ili kutimiza ndoto yao ya kubakia katika Ligi Kuu.