Kaburu kikaangoni

SAKATA la kadi tatu za njano za mchezaji Mohamed Fakhi wa Kagera Sugar linazidi kuchukua sura nyingine na sasa Makamu mwenyekiti wa Simba, Geofrey Nyange ‘Kaburu’ na wafanyakazi wawili wa bodi ya ligi (TPLB) wamewekwa kikaangoni.

Kwa karibu wiki ya pili sasa kumekuwa na mgogoro kati ya Simba na Kagera Sugar, baada ya Simba kukata rufaa kamati ya saa 72 ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kupinga ushindi wa Kagera Sugar kwa vile ilimchezesha Fakhi akiwa na kadi tatu za njano.

Katika mechi hiyo iliyofanyika kwenye uwanja wa Kaitaba, Bukoba, Kagera Sugar ilishinda mabao 2-1. Kamati ya saa 72 iliipoka Kagera pointi tatu na mabao matatu na kuipa Simba baada ya kujiridhisha kwamba Fakhi hakustahili kucheza mechi hiyo kwa vile alikuwa na adhabu ya kadi tatu za njano hivyo alipaswa kusimama mechi moja.

Uamuzi wa kamati ya saa 72 uliifanya Kagera kuandika barua TFF ikiomba marejeo ya adhabu hiyo na ndipo suala hilo ikapewa Kamati ya Sheria na Hadhi kwa wachezaji iliyokuwa na kikao tangu Jumanne ya wiki hii ikiwahoji watu mbalimbali.

Katibu Mkuu wa TFF, Selestine Mwesigwa alisema jana kuwa maamuzi ya kamati hiyo yatawekwa hadharani leo lakini habari za uhakika zilizopatikana jana zinasema Kaburu ambaye pia ni mjumbe wa kamati ya utendaji ya TFF pamoja na wafanyakazi wa bodi ya ligi Joel Balisidya na Rose Msamila wapo kikaangoni baada ya kuonekana kuhusika katika sakata hilo.

Habari za uhakika kutoka ndani ya kamati hiyo iliyo chini ya Mwenyekiti Richard Sinamtwa, huenda Kaburu na watendaji hao wa bodi ya ligi wakafungiwa. “Ni kweli Fakhi alikuwa na kadi tatu za njano kabla ya mechi ya Simba, wafanyakazi wa bodi ya ligi ndio waliovujisha siri na kumpa Kaburu faili, ndio maana kamati inataka kutoa adhabu kwao iwe fundisho siku nyingine wajue kutunza siri za taasisi,” kilisema chanzo cha habari.

Watendaji hao wa bodi ndio wanaohusika na utunzaji kumbukumbu za mechi zote za ligi. “Fakhi ni kweli alikuwa na kadi tatu lakini jambo hilo lilikuwa la kiofisi zaidi wahusika wa bodi ya ligi wengeweza kuwaambia Kagera kabla ya mechi kama tahadhari lakini si kukaa kimya”.

Habari zaidi zinasema, kamati hiyo haitabadilisha maamuzi ya kamati ya Sheria na hadhi kwa wachezaji na kwamba pointi ilizopokwa Kagera zitabaki kwa Simba kwa vile ni kweli Fakhi alikuwa na kadi tatu za njano na kanuni inawalazimisha kuwapoka ushindi timu husika.