Yanga, Toto mechi ya maumivu Taifa

MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu soka Tanzania bara Yanga wana kazi nzito leo katika mchezo dhidi ya Toto Africans utakaochezwa kwenye uwanja wa Taifa Dar es Salaam.

Mchezo huo unatarajia kuonyesha taswira ya bingwa wa msimu huu lakini pia, kuna uwezekano mkubwa wa Toto Africans kushuka daraja kama watakubali kipigo. Licha ya timu hizo kuhusishwa kuwa na mahusiano ya karibu, huenda ukawa ni mchezo mgumu kwa kila mmoja. Yanga inataka ushindi ili kujihakikishia nafasi ya kuwa bingwa na Toto inataka ushindi kujinusuru katika hatari ya kushuka daraja. Yanga iwapo itashinda mchezo huo itafikisha pointi 68, pointi ambazo kama Simba itashinda mechi yake ya mwisho dhidi ya Mwadui itazikisha, lakini Yanga ikiwa na silaha ya mechi yake ya mwisho dhidi ya Mbao.

Hivyo Simba inatakiwa kuomba mambo mawili kwa wakati mmoja, Yanga ifungwe na Mbao na yenyewe iifunge Mwadui mabao mengi ili kuipiku Yanga kama ikibidi bingwa aamuliwe kwa wingi wa mabao. Kupoteza mechi ya leo kwa Toto iliyo nafasi ya pili kutoka mkiani, kunaashiria kuungana kwake na JKT Ruvu kushuka daraja. Mchezo wa mwisho wa Yanga dhidi ya Mbao FC unatabiriwa kuwa mgumu kutokana na timu hiyo ngeni msimu huu kuwaondosha wakongwe hao kwenye kombe la FA. Kocha Msaidizi wa Yanga Juma Mwambusi amesema hawawezi kuidharau Toto Africans, wataingia kwa tahadhari kusaka pointi tatu.

Alisema mchezo huo utakuwa mgumu kwani Toto wanaweza kucheza vizuri ili kutafuta matokeo ya kujinusuru kwenye hatari ya kushuka daraja na wao wanahitaji kutetea taji lao hivyo, ni muhimu kwao kupambana. “Kikubwa tumejiandaa vizuri kuhakikisha kesho (leo), Mungu anatusaidia na kuondoka na pointi tatu. Toto ni timu nzuri inaweza kucheza mchezo mzuri kwasababu inataka matokeo,” alisema