Vita ya kushuka daraja

MSIMU wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwa mwaka 2016/17 unamalizika leo, huku Yanga ikijiandaa kukabidhiwa Kombe lake itakapocheza dhidi ya Mbao FC kwenye Uwanja wa CCM Kirumba.

Ligi hiyo inakamilika wakati Yanga mbali na kutwaa taji hilo kwa mara ya tatu mfululizo, pia imefuzu tena kuliwakilisha taifa katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa wa Afrika msimu ujao.

Hii ni mara ya 27 kwa Yanga kutwaa ubingwa huo wakati Simba wamelitwaa taji hilo mara 18 tu na hivyo kuifanya timu hiyo ya Jangwani kuwa bingwa wa kihistoria. Mechi za leo zitakazokuwa na msisimko zaidi ni zile ambazo zitazikutanisha timu zilizoko katika hatari ya kushuka daraja.

Tayari JKT Ruvu iliyoshiriki ligi hiyo kwa karibu misimu 10, imeshashuka daraja, hivyo leo zinatafutwa timu mbili zitakazoungana nao. Yanga ina pointi 68 wakati wapinzani wao Simba wako katika nafasi ya pili baada ya kujikusanyia pointi 65, hivyo kuhitaji ushindi dhidi ya Mwadui na wakiombea dua baya Yanga ifungwe na Mbao FC.

Katika dua hilo baya dhidi ya Yanga, Simba wenyewe wanatakiwa kushinda kuanzia mabao 31-0 dhidi ya timu hiyo ya Shinyanga, kitu ambacho ni kigumu kutokea katika soka. Ukiangalia rekodi ya ufungaji mabao Simba na hata timu zingine zinazoshiriki ligi hiyo, hakuna iliyowahi kufunga au kufungwa zaidi ya mabao sita, hivyo itakuwa miujiza, endapo wekundu hao wa Msimbazi watafunga mabao 13-0 au zaidi.

Yanga ni kama inasubiri kukabidhiwa taji lake hilo leo wakati Simba imejihakikishia nafasi ya pili, ambayo msimu huu haitoi mwakilishi wa Tanzania katika Kombe la Shirikisho Afrika. Simba sasa nguvu zao wanazielekeza katika fainali ya Kombe la Shirikisho itakayofanyika Dodoma wikiendi ijayo dhidi ya Mbao FC, ili iweze kupata nafasi ya kushiriki mashindano ya kimataifa msimu ujao.

Timu hiyo kwa misimu minne imeshindwa `kupanda ndege’ baada ya kumaliza Ligi Kuu Tanzania Bara ikiwa nje ya nafasi ya pili, ambayo Azam FC ndio ilikuwa ikishika mara kwa mara. Timu za Toto Africans, Ndanda, Mbao, African Lyon pamoja na Majimaji kati ya hizo mbili zitaungana na JKT Ruvu kushuka daraja kama zitashindwa kucheza karata zao vizuri katika mechi za leo.

Toto ina pointi 29 endapo leo itaifunga Mtibwa Sugar itafikisha pointi 32 na kuzipita Ndanda, Mbao na African Lyon,kama timu hizo zitafungwa au kutoka sare katika mechi zao za mwisho leo.

Nazo Ndanda na Mbao ambazo kila moja ina pointi 30 zikishinda leo zitaweza kufikisha pointi 33 na kuziacha Toto Africans na African Lyon zikiifuata JKT Ruvu shimoni. African Lyon ikishinda leo itafikisha pointi 34 na kujinasua kabisa katika janga la kushuka daraja, kwani itakuwa imezipita Toto Africans, Ndanda na Mbao hata kama nazo zitashinda mechi zao za leo.

Timu za Mbeya City, Prisons, Mwadui, Stand United, Ruvu Shooting, Mtibwa Sugar, Kagera Sugar na Azam FC, hazina presha ya kushuka daraja, kwani ziko katika nafasi nzuri. Tayari timu za Mji Njombe, Lipuli ya Iringa na Singida United zimeshapanda daraja tayari kwa ajili ya msimu ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara.