TFF yaigomea BMT uchaguzi mkuu

SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) limekataa kusitisha mchakato wa uchaguzi mkuu wake Agosti 12 kama lilivyoagizwa na Baraza la Michezo Tanzania (BMT) Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu wa TFF, Mwesigwa Selestine wakati akizungumza na wandishi wa habari Dar es Salaam jana.

Hata hivyo, alikiri TFF kupokea barua ya BMT inayotaka wasitishe uchaguzi huo hadi itakapokutana na viongozi wa TFF. Badala yake, alisema, TFF imeiandikia BMT kuomba wakutane kabla ya Julai mosi, tarehe ambayo BMT ilipendekeza kukutana na Kamati ya Utendaji ya TFF.

“Tunatarajia kukutana nao maana naamini wanafanya hivi kwa sababu ya afya ya mpira wa miguu lakini hatutasimamisha uchaguzi kwa sababu utakuwa nje ya katiba,” Selestine aliwaambia waandishi. Alisema katiba ya TFF inawataka uchaguzi kufanyika kabla ya Agosti kumalizika hivyo wakisitisha mchakato watakuwa wanakiuka katiba na kuleta matatizo.

“Uchaguzi Mkuu wa TFF ni agenda moja tu katika mkutano huo. Ukisitisha mchakato wa uchaguzi, unaweza kujikuta umefika mwakani bila kufanya uchaguzi. Pia kamati inayosimamia uchaguzi ipo kihalali kulingana na katiba ya TFF,” alisema.

Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya TFF, Revocatus Kuuli mapema wiki hii alitangaza kuwa uchaguzi mkuu wa TFF utafanyika Agosti 12 mjini Dodoma. Alisema, fomu za kugombea zitaanza kutolewa leo ambapo ada ya kuwania urais ni sh 500,000, umakamu wa rais ni sh 300,000 na ujumbe wa Kamati ya Utendaji ni sh 200.000 kwa kila moja.

Juni 13 Katibu Mkuu wa BMT, Mohamed Kiganja aliiandikia TFF barua akiagiza isitishe kwanza uchaguzi huo kwa sababu hawajaijulisha BMT kuhusu uchaguzi huo. Pia barua hiyo iliwataarifu TFF Kamati ya Nidhamu, Rufaa na Usuluhishi ya BMT inataka kukutana na Kamati ya Utendaji ya TFF Julai Mosi saa nne asubuhi katika ofisi za baraza zilizopo Uwanja wa Taifa.

Selestine alisema wao wana katiba yao inayojitegemea na wanapaswa kuwasilisha BMT, matokeo ya uchaguzi lakini siyo kuwajulisha juu ya mchakato wa uchaguzi. Hata hivyo, katika barua yake, Kiganja alinukuu kanuni na sheria inayoipa BMT, mamlaka ya kusimamia uchaguzi akidai ndio pekee yenye mamlaka ya kusimamia uchaguzi wa vyama vya michezo hadi leo.

Wakati huo huo, Wajumbe wa kamati ya Utendaji ya TFF, Ahmed Mgoyi na Kidao Wilfred wametangaza kutogombea nafasi yoyote katika uchaguzi mkuu huo. Mgoyi amekuwa Mjumbe wa Kamati ya Utendaji kwa muda mrefu (2004-2017) tangu enzi za utawala wa Leodgar Tenga. Mgoyi amekuwa Mjumbe anayewakilisha Kanda ya Tabora na Kigoma na Kidao anawakilisha Kanda ya Dar es Salaam.

Katika waraka wake aliotoa katika vyombo vya habari, Mgoyi alisema ameamua kwa ridhaa yake kutoa fursa kwa wengine kugombea na kuomba radhi kwa watu ambao hawakutarajia atatoa uamuzi huo. Naye Kidao ambaye alichaguliwa 2013 amesema hatatetea nafasi yake katika uchaguzi mkuu ujao wala kugombea nafasi yoyote ya juu katika uchaguzi huo.