Ni Malinzi, Madega, hadi kieleweke Wambura urais TFF

RAIS wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi amechukua fomu ya kutetea nafasi yake hiyo kwenye uchaguzi mkuu ujao. Malinzi amechukua fomu hizo baada ya TFF kukaidi agizo la Baraza la Michezo la Taifa (BMT) la kuitaka TFF kusitisha uchaguzi huo hadi Julai Mosi itakapokutana na uongozi TFF.

Wanamichezo wengine waliochukua fomu jana ofisi za TFF Jijini Dar es Salaam ni Katibu Mkuu wa zamani wa kilichokuwa Chama cha Soka Tanzania (FAT), Michael Wambura. Wambura anawania Umakamu wa Rais TFF huku Mwenyekiti wa zamani wa Yanga, Imani Madega akichukua fomu kuwania urais wa TFF.

Vigogo hao na wengine waliochukua fomu kupitia mtandao wa TFF wanatakiwa kurejesha fomu hizo TFF Juni 20, zitakapojadiliwa TFF. Malinzi, Wambura na Madega walifika TFF kwa nyakati tofauti huku kila mmoja akiionesha fomu kwa wanahabari waliokuwa nje kufuatilia.

Ofisa Habari wa TFF, Alfred Lucas alisema wagombea wa TFF walio nje ya Dar es Salaam watapata fomu kwa kutuma barua pepe kwenye Anwani ya barua pepe hii inalindwa kutokana na spambots. JavaScript lazima iwe itawezeshwa kwa kuweza kuona.. Alisema wagombea wa mikoani watatakiwa kulipia ada ya kuchukua fomu kupitia Benki ya CRDB katika akaunti namba 01J1019956700.

Wanaogombea urais wanatakiwa kulipia ada ya sh 500,000, umakamu wa rais sh 300,000 na ujumbe wa kamati ya utendaji sh 200,000. Lucas alisema, baada ya kulipia ada benki, mgombea atawasilisha stakabadhi ya malipo TFF na kupewa fomu kuwania nafasi aitakayo.

Wakati vigogo hao wakichukua fomu, Wajumbe wawili wa Kamati ya Utendaji ya TFF, Ahmed Mgoyo na Wilfred Kidau hawatagombea tena. Walitangaza uamuzi wao juzi na Lucas alisema Malinzi amempongeza Mgoyi kwa uamuzi huo.

Malinzi pia alimpongeza Francis Amin Michael kwa kuchaguliwa kuwa Rais wa Chama cha Mpira wa Miguu cha Sudan Kusini (SSFA). Alisema anaamini Amin atashirikiana na wadau na Serikali ya Sudan Kusini kuendeleza soka, hasa Baraza la Soka la Afrika Mashariki (CECAFA) ambako TFF ni mwanachama pia.

Amesema hayo huku TFF ikiwa imekataa kutii agizo la Baraza la Michezo Tanzania (BMT) kuitaka TFF kusitisha uchaguzi hadi Julai mosi. Katibu Mkuu wa BMT, Mohamed Kiganja aliiandikia TFF barua isitishe uchaguzi hadi watakapokutana na Kamati ya Utendaji ya TFF.

Kiganja alisema aliiandikia TFF barua kwa sababu imeitisha uchaguzi Agosti 12 Dodoma bila kuiarifu BMT kinyume cha kanuni za BMT. Kiganja alisema BMT ndiyo pekee yenye mamlaka ya kusimamia uchaguzi wa vyama vyote vya michezo nchini jambo lililopingwa na Katibu Mkuu wa TFF, Mwesigwa Selestine juzi.

Mwesigwa alisema hawatasitisha uchaguzi wao kwa sababu uko kikatiba na akasema wako tayari kukutana na BMT kabla ya Julai Mosi. Kiganja alipoulizwa jana kuhusu TFF kukaidi agizo lake, alikataa kusema lolote lakini Mwenyekiti wa zamani wa BMT, Said El Maamry alisema hakuna tatizo BMT kusimamia uchaguzi TFF mradi hawabebi mgombea wao. Mjumbe wa zamani wa BMT, Juma Pinto naye alisema BMT ina meno ya kusimamia uchaguzi wa TFF na ilifanya hivyo kwa vyama vingine.