TRA kufa na TFF hadi kieleweke

MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) imekataa kulisamehe Shirikisho la soka nchini (TFF), deni la sh bilioni 1.6 linazodaiwa. Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi wa TRA, Richard Kayombo alisema jana Jijini Dar es Salaam kuwa kodi wanayokatwa TFF ni ya halali kwa kuwa inatambulika kisheria na wala si uonevu kama wanavyodai.

TFF inadaiwa kiasi hicho kama kodi na faini ya malimbikizo ya kodi ya mishahara ya makocha wa zamani wa timu ya soka ya Taifa Stars. Kayombo alisema kodi hiyo inatokana na mishahara ya makocha na kila mfanyakazi nchini anatakiwa kulipa kodi na kuwa makocha hao walikuwa wakiingiza kipato ambacho wanatakiwa kukatwa kodi na TRA.

Akizungumzia hoja ya Katibu Mkuu wa TFF, Mwesigwa Selestine juzi kuwa kulikuwa na mazungumzo kati ya TFF na Wizara ya Fedha na Mipango na Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ambapo ilikubaliwa TRA waache kuikata TFF fedha hizo, Kayombo alisema hakuna maelekezo kwenye kulipa kodi bali sheria na sheria ni lazima ifuatwe.

Alisema kama TFF wanataka sheria ibadilishwe, basi wapeleke suala hilo bungeni. “Hakuna suala la msamaha wala suala la kupewa maelezo tofauti na kulipa. Na kama inatakiwa kufanyika kwa mabadiliko kwa aina hii ya kodi, basi waende bungeni kwa kuwa hili ni suala la kisheria na kama kubadilishwa basi ni bungeni,” alisema.

TRA inaidai TFF kodi kutoka kwenye mishahara ya makocha, Marcio Maximo kutoka Brazil na Martin Nooij wa nchini Denmark inayofikia Sh bilioni 1.6. Makocha hao waliajiriwa kwa mkataba na TFF kama mwajiri lakini mishahara yao ilikuwa ikilipwa na Serikali kupitia wizara husika.

TFF wamekuwa wakipinga kukatwa kodi kwa madai mishahara hawakuwa wakiilipa wao. Sheria ya kodi inataka kila mwajiri kulipa kodi anayoikata kwa mfanyakazi wake.

Mwesigwa alisema juzi deni la TRA lililobakia ni sh Milioni 400 ambazo huenda zikafanya TFF iziondoe timu za Taifa, Taifa Stars na Ngorongoro Heroes michuano ya kimataifa Hata hivyo, alipobanwa jana kama watazitoa timu baada ya TRA kuwakatalia, Mwesigwa alisema wataendelea kuwasiliana na TRA na mamlaka husika ili wapunguziwe deni hilo.