Tunasajili kwa malengo- Aveva

RAIS wa Simba, Evans Aveva amewashusha presha mashabiki wa timu yake kuhusu usajili wanaofanya akisema ni maagizo ya kocha wao mkuu Joseph Omog.

Tangu dirisha la usajili kwa ajili ya msimu wa mwaka 2017/2018 lifunguliwe Juni 15 mwaka huu, tayari Simba imeshafanya usajili wa wachezaji sita mpaka sasa. Dirisha la usajili linatarajiwa kufungwa Agosti 6.

Akizungumza kwenye hafla ya futari iliyoandaliwa na mashabiki na wanachama wa kundi la Whatsap la Simba Head Quarter Dar es Salaam juzi, Aveva alisema hawajakurupuka kwenye usajili, hivyo mashabiki wao wasiwe na hofu.

“Usajili tunaoufanya huu ni baada ya kupata ripoti ya benchi letu la ufundi chini ya kocha wetu Omog, hivyo mshabiki wetu haina haja ya kuhofia,” alisema. Alisema kamati yao ya usajili chini ya Zacharia Hanspoppe imejipanga kuhakikisha haifanyi makosa kwenye usajili kwani haitaki kufanya vibaya kitaifa na kimataifa msimu ujao.

Simba ambayo haijashiriki michuano ya kimataifa kwa miaka minne, imemaliza msimu uliopia ikiwa nafasi ya pili baada ya kufikisha pointi 68 sawa na Yanga iliyotwaa ubingwa kwa uwiano mzuri wa mabao.

Mpaka sasa Simba imewasajili John Bocco, Shomari Kapombe, Aishi Manula kutoka Azam, Jamal Mwambeleko, Yusuf Mlipili na Ally Shomari huku ikidai kuwa iko kwenye mazingira mazuri ya kumrejesha mshambuliaji wake wa zamani Mganda, Emmanuel Okwi.

“Tunafanya usajili kwa umakini kwani lengo letu msimu ujao, tunahitaji mpaka kwenye Pasaka tayari tumeshatangaza ubingwa na kuepukana na hili suala la kwenda kukata rufaa Fifa. Aveva alisema usajili wao wanahitaji kupata wachezaji watakaoifanya Simba kupata pointi za kutosha.

Aidha, alisema malengo yao, baada ya kumaliza usajili, wamalize uwanja wao wa Bunju. “Muda wowote kuanzia sasa tutaleta ajenda hii mezani kwa wanachama wetu ya kuhakikisha tunatandika nyasi zetu katika uwanja wa Bunju kwa ushirikiano mzuri na umoja wetu kama ilivyokuwa katika suala la kusapoti timu,” alisema.

Katika hatua nyingine, Mwenyekiti wa Baraza la Michezo Tanzania (BMT), Dionis Malinzi amewataka viongozi wa Simba kuwa wamoja katika kipindi cha usajili ili kuipatia timu mafanikio. “Umakini muhimu, haiwezekani viongozi muwe hampatani, hapo hamuwezi kupata mafanikio,” alisema.

Kauli hiyo ya Malinzi ambaye ni mnazi wa Simba imekuja baada ya kuwepo kwa minong’ono ya chini chini kwamba viongozi wa Simba hawakuwa na maelewano mazuri kwa msimu wote uliopita jambo lililochangia kwa kiasi kikubwa timu hiyo kukosa ubingwa.

Aidha Malinzi aliwataka viongozi kuwa makini kwenye suala la usajili ili wasisajili mamluki. “Usajili pamoja na mambo mengine lakini uzingatie mapenzi ya dhati ya mchezaji, sio mnasajili mchezaji anafuata fedha tu bila kujali maumivu ya wanachama timu inapofanya vibaya,” alisema.