Tshabalala ang’ara tena Simba

MCHEZAJI Mohammed Hussein (Tshabalala) wa Simba juzi alitangazwa kuwa mchezaji bora wa msimu wa timu hiyo. Akizungumza katika hafla ya futari iliyoandaliwa na mashabiki wa kundi la Whatsap la Simba Head Quarter (Simba HQ) Dar es Salaam juzi, Ofisa Habari wa Simba, Haji Manara alisema Tshabalala amepata tuzo hiyo kutokana na nidhamu yake msimu wa mwaka 2016/2017.

“Binadamu huyu amecheza mechi zote 30 za Ligi Kuu na mechi zote za kombe la FA isipokuwa ya fainali tu dhidi ya Mbao alitolewa kipindi cha kwanza baada ya kuumia… ana nidhamu ya hali ya juu, hana kadi nyekundu,” alisema.

Tshabalala pia ndiye mchezaji bora wa Ligi Kuu msimu wa mwaka 2016/2017 tuzo aliyopata mwishoni mwa msimu ambapo alizawadiwa sh milioni 10 kutoka kwa wadhamini wa ligi, kampuni ya simu za mkononi ya Vodacom.

Tshabalala alikabidhiwa tuzo hiyo na Mwenyekiti wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Dionizi Malinzi ambaye pia alitoa sh milioni moja kama pongezi kwa mchezji huyo. Mbali na Malinzi, Tshabalala ambaye anatembelea magongo kwa sasa kutokana na kuumia kwenye fainali za kombe la FA dhidi ya Mbao, alipata karibu sh milioni mbili alizochangiwa na wadau wa Simba waliofika kwenye futari hiyo.

Aidha mchezaji wa timu ya vijana ya Simba, Mosses Kitandu pia alipewa tuzo ya kuwa mchezaji bora wa msimu na Malinzi alimzawadia sh laki tano. Tshabalala aliliambia gazeti hili kwamba hajisikii vibaya kwa kipindi hiki anachojiuguza kwani aliumia akiipigania timu yake na kuisaidia kupata ubingwa wa FA kwa ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Mbao.

“Napata maumivu ya kawaida, ila sijisikii vibaya wakati tumeshapata kombe na mwakani tuna uhakika wa kushiriki michuano ya kimataifa, hali hiyo inanipa faraja kwamba nimeumia kwa sababu maalum,” alisema.

Akizungumzia usajili na ujio wa beki mwenzake, Shomari Kapombe kutoka Azam, Tshabalala alisema timu yake imefanya usajili mzuri ana imani safu yao ya ulinzi itaimarika zaidi. “Naamini ujio wa Kapombe utakuwa msaada mkubwa kwetu, sina mashaka nae,” alisema