Taifa Stars ya tatu Cosafa

TIMU ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars imetwaa medali ya shaba baada ya kuifunga kwa penalti Lesotho katika mchezo wa kusaka mshindi wa tatu katika Kombe la Cosafa.

Mchezo huo ilibidi bingwa apatikane kwa penalti baada ya timu hizo kutoka suluhu katika dakika 90 za kawaida. Kwa ushindi huo, Taifa Stars imepata dola za Kimarekani 10,000 (sawa na zaidi ya Sh milioni 22) na kutwaa medali ya shaba katika mashindano hayo.

Tanzania katika mchezo huo iliibuka na ushindi wa mabao 4-2 dhidi ya Lesotho baada ya kupigiana penalti baada ya kumalizika kwa mchezo huo.Katika mchezo mwingine wa kusaka nafasi ya nne na tano, wenyeji Afrika Kusini walipata ushindi kiduchu wa bao 1-0 dhidi ya Namibia katika mchezo uliochezwa mapema juzi.

Lesotho ilikosa nafasi kibao licha ya kutawala mchezo huo baada ya kushindwa kuutumbukiza mpira ndani ya kimia. Huo ulikuwa ni mchezo wa tatu wa Lesotho katika mashindano hayo, ambayo ilianzia hatua ya robo fainali, wakati Tanzania huo ulikuwa ni mchezo wake wa sita ndani ya wiki mbili.

Katika kipindi cha kwanza kiungo anayecheza soka Marekani, Thabantso Jane shuti lake lilipoteza mwelekeo huku Kefuoe Mahula na Sera Motebang nao wakipoteza nafasi za wazi. Taifa Stars nao nusura wapate bao katika dakika za mwisho za mchezo lakini Mzamiru Yasin alipaisha juu ya lango.

Shujaa wa Taifa Stars alikuwa kipa Said Mduda aliyepangua penalti ya nahodha wa Mamba hao, Thapelo Mokhehle baada ya Sera Motebang kugongesha kwenye mwamba wa kulia mkwaju wake na kurudi uwanjani.

Waliofunga penalti za Lesotho ni Hlompho Kalake na Tsoanelo Koetle wakati Shiza Kichuya aligongesha mwamba wa juu penalti ya kwanza ya Tanzania. Walioifungia Taifa Stars ni nahodha Himid Mao,Simon Msuva, Abdi Banda na Raphael Daudi na kupata ushindi wa 4-2.

Ushindi wa Stars kwa Lesotho umekuja siku 25 baada ya timu hizo kutoka sare ya 1-1 Juni 10, katika mchezo wa ufunguzi wa Kundi L kufuzu Kombe la Mataifa ya Afrika Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam. Fainali ya Cosafa Castle 2017 itachezwa leo kwenye Uwanja wa Royal Bafokeng, Phokeng Rusternburg kati ya Zambia na Zimbabwe