Mhariri HabariLeo atetea kiti TWFA

MHARIRI Msaidizi wa habari za michezo wa gazeti hili, Zena Chande ametetea kiti chake cha ujumbe wa Mkutano Mkuu wa Shirikisho la Soka (TFF) katika Uchaguzi wa Chama cha Soka la Wanawake Tanzania (TWFA), uliofanyika Dar es Salaam jana.

Zena aliyekuwa akitetea nafasi hiyo, alipata kura 44 kati ya 52 zilizopigwa, huku mpinzani wake Salma Wajeso akiambulia kura nane. Katika nafasi ya Mwenyekiti, Amina Karuma alifanikiwa kutetea kiti chake kwa kura 47 huku kura tano zikimkataa, licha ya kuwa mgombea pekee wa kiti hicho.

Rose Kisiwa alitetea nafasi yake ya Makamu Mwenyekiti kwa kupata kura 46 na kura sita zikimkataa. Naye mwandishi mwandamizi wa Nipashe, Somoe Ng’itu alichaguliwa kuwa Katibu Mkuu kwa kura 49 huku kura mbili zikimkataa na Katibu msaidizi alichaguliwa Theresia Mung’ong’o aliyepata kura 44 na kura nane zikimkataa.

Nafasi ya Mhazini ilikwenda kwa Hilda Masanche kwa kupata kura 25 huku kura 24 zikimkataa na kura tatu zikiharibika na nafasi ya wajumbe wa Kamati ya Utendaji ilikosa watu baada ya wagombea kushindwa kufikia nusu ya kura za wajumbe.

Wajumbe wa Kamati ya Utendaji ilihitaji watu wanne na wagombea walikuwa wanne ambao ni Triphonia Temba kura 15, Chichi Mwidege kura 12, Mwamvita Kiyogoma kura 9 na Jasmine Soudy kura saba.

Akizungumza wakati wa kutangaza matokeo hayo, Mwenyekiti Kamati ya Uchaguzi ya TWFA, Wakili George Mushumba, alisema wagombea hao walihitaji kupata kura zaidi ya nusu ya wapiga kura, ambao ilikuwa ni 52 ili wawe wajumbe.

“Najua katiba inaruhusu kuteua wajumbe wawili, lakini hao waliogombea wameshindwa hivyo uongozi uliochaguliwa utaona namna inayofaa ili waweze kuendelea na kazi zao za kuendeleza soka la wanawake,” alisema Mushumba.

Pia Mushumba aliwashukuru wagombea na wajumbe wa mkutano huo kwa ushirikiano walioonesha kwa kamati kipindi chote kuanza kwa mchakato wa uchaguzi na kuwataka kufanya kazi kwa kushirikiana ili kuleta maendeleo.

Naye Mwenyekiti wa TWFA, Amina Karuma aliwashukuru wajumbe kwa kuwarudisha madarakani kwa kishindo na kuishukuru Kamati ya Uchaguzi kwa kazi nzuri waliyofanya kwa kusimamia uchaguzi. “Bila ushirikiano na ninyi sisi hatuwezi kufanya chochote hivyo naomba tuendelee kushirikiana ili tuzidi kufanya mazuri zaidi ya hayo tuliyokwisha kufanya,” alisema Karuma.