Rooney ndani ya Taifa

LEO ndio leo. Asiye na mwana aeleke jiwe. Everton, timu inayocheza Ligi Kuu England inaweka historia nchini kwa kucheza mechi Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Everton itavaana na bingwa wa Kombe la SportPesa, Gor Mahia ya Kenya katika mechi ya kirafiki iliyoandaliwa na SportPesa inayochezesha michezo ya kubahatisha.

Kivutio kikubwa katika mechi hiyo anatarajiwa kuwa mshambuliaji nyota wa zamani wa Manchester United, Wayne Rooney aliyejiunga na timu hiyo wiki iliyopita. Rooney alikuwa akisubiriwa kwa hamu na mashabiki wa soka nchini ambao hadi juzi walikuwa hawana uhakika kama atakuja na timu hadi alipothibitisha kupitia tweeter.

Mechi hiyo inatarajiwa kuvuta maelfu ya mashabiki katika uwanja huo wenye uwezo wa kubeba watazamaji 60,000 na mamilioni duniani kote watakaofuatilia matangazo ya SuperSport itakayorusha mubashara. Kiingilio cha mechi hiyo ni Sh 8,000 kwa jukwaa la VIP na Sh 3,000 kwingineko.

Mgeni rasmi ni Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan. Ni mechi ya kihistoria kwa kuwa mashabiki watamwona Rooney na wenzake mubashara Taifa lakini pia itasaidia kuitangaza Tanzania katika utalii. Ili kuwapa ahueni Everton kutokana na Dar es Salaam kuwa na hali ya hewa ya joto tofauti na Ulaya, mechi hiyo itaanza saa 11 jioni.

Kocha wa Gor Mahia, Dylan Kerr alisema jana ni heshima kubwa kwake kucheza na Everton yenye wachezaji nyota duniani. Kerr raia wa Uingereza aliyewahi kuinoa Simba alisema ingawa ana wiki moja na Gor Mahia, anaamini mechi itakuwa nzuri yenye upinzani.

Kocha wa Everton, Koeman amesema kila mchezaji wake akiwemo Rooney atacheza dakika 45 wakilenga kuimarisha viungo vyao. Mechi hiyo ni ya maandalizi ya ligi yao. Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Harrison Mwakyembe amewaomba Watanzania kujitokeza kwa wingi uwanjani.

Mwakyembe alisema jana ujio wa Everton ni muhimu katika kuitangaza nchi katika utalii. Alisema timu hiyo imeipa nchi heshima kubwa kwani sasa kila kona ya dunia wanazungumzia timu yenye mchezaji nyota duniani, Rooney.

Everton iliwasili jana Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) saa 3 asubuhi kwa ndege binafsi, ikiwa na wachezaji 25 kivutio akiwa nyota wao, Rooney. Baada ya kuwasili, Everton walipitia jengo jipya la VIP na kulakiwa na Waziri Mwakyembe.

Rooney alikuwa mmoja wa wachezaji wa mwisho kutokea na kulakiwa na Mwakyembe. Wafanyakazi wa JNIA, abiria na mashabiki walijitokeza kuwalaki wachezaji hao kabla hawajapanda basi la kisasa lililobandikwa stika za Sports Pesa, wadhamini wa ziara.

Mapokezi yao yalipambwa na shangwe za raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) (wenye tisheti nyeupe pichani) waliocheza ngoma kumpokea Yannick Bollasie. Wakongo hao walijipanga nje ya uzio wakiimba jina lake Bolasie, raia wa DRC.

Everton waliondoka JNIA kwa kusindikizwa na pikipiki ya Polisi hadi Hotel Sea Cliff. Hoteli walishindana kupika huku kundi lingine likienda kufanya shughuli za jamii kwa kucheza na timu ya watoto albino Uwanja wa Taifa.

Phil Jagielka na Dominic Calvert-Lewin walishindana na Davy Klaassen na Matty Pennington kupika chakula cha asili ya Tanzania. Jags na Dom walishindana kupika ugali na Davy na Matty kuandaa nyama choma.

Walisaidiwa na mpishi mkuu wa Sea Cliff Hotel, Niko. Chakula kilionjwa na Balozi wa Everton, Graham Stuart aliyemteuea mshindi. Shughuli nyingine ya jamii waliyofanya ni kutembelea shule ya Uhuru Mchanganyiko.

Wakiwa huko waliwafariji watoto wenye ulemavu wa kutoona, mtindio wa ubongo na ulemavu wa kutosikia ambapo ili kujua machungu wanayopitia nao waliziba macho yao na kucheza nao mpira. Waliojifunika macho ni Leighton Baines, Yannick Bolasie, Ademola Lookman na Idrissa Gana Gueye.

Walitumia mpira wenye kengele. Baines alikaririwa na mtandao wa evertonfc.com: akisema wachezaji wote wanaamini elimu ni muhimu kwa kila mtoto. Alisema wana furaha Shirika la Misaada ya Maendeleo la Uingereza (FFID) kuwasaida watoto 18,000 wenye matatizo nchini.

Walisema ni fursa ya kipekee kujionea matatizo ya watoto hao wanaoweza kusaidiwa na soka. Kundi lingine lilitembelea kituo cha timu ya albino inayofundishwa na Kocha Alex Kashaha aliyewaeleza historia ya timu hiyo.

Kashasha alisema Albino United ilianzishwa kuionesha dunia hata wao wanaweza kucheza soka licha ya kuathiriwa na joto kwenye mwili. Wengine walitembelea maonesho ya sanaa na mila za kabila la Wamasai na kufurahia. Jioni walifanya mazoezi Uwanja wa Taifa kupasha. Ni wazi mechi ya leo itakuwa si ya mtoto kutumwa dukani bali mashabiki husika kuiona.