FIFA: TFF leteni hesabu za fedha

SHIRIKISHO la Soka la Kimataifa (Fifa) limeliagiza Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kupeleka mahesabu yake ya fedha ya mwaka na ripoti ya mkaguzi wake rasmi wa mahesabu.

Fifa imetoa agizo hilo katika barua iliyoandikwa Julai 6, 2017 na Mkurugenzi wa Uanachama na Maendeleo wa Fifa, Veron Osengo Omba. Katika barua yake kwa Kaimu Rais wa TFF, Wallace Karia ambayo gazeti hili limeona nakala yake, Omba ameiagiza TFF kupeleka pia, ripoti ya maendeleo ya miradi ya Fifa.

Amesema hayo katika barua aliyomwandikia Karia kueleza Fifa inavyofuatilia uendeshaji soka baada ya Rais Jamal Malinzi kushitakiwa. Malinzi na Katibu Mkuu wa TFF, Mwesigwa Celestine na Mhasibu Nsiande Mwanga wako mahabusu Keko wakikabiliwa na kesi ya jinai.

Wanakabiliwa na mashitaka 28 likiwemo la kutakatisha fedha yaliyofunguliwa dhidi yao na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru). “Tunakuandikia kutaka taarifa za mambo yanayoendelea ndani ya TFF hivi sasa.

Kufuatia mashitaka yaliyofunguliwa dhidi ya Malinzi na Mwesigwa Juni 26, 2017, tunaomba ututaarifu shughuli TFF zinavyoendeshwa sasa,” alisema. Omba alisema, wakati kesi ya kina Malinzi ikiendelea, ni vyema uongozi wa muda TFF na menejimenti yake ukawa unawasiliana na Fifa.

Katika kujua kinachoendelea, Omba alimtaka Karia kuifahamisha FIFA, mazingira ya sasa ya ufanyaji kazi TFF na uwezo wao (wanaokaimu) kuendelea kuendesha shughuli za TFF. Pia aliagiza TFF ieleze ilikofikia kuhusu uwasil ishaji ripoti ya ukaguzi ya miradi ya FIFA nchini na mahesabu ya fedha ya mwaka ya TFF na taarifa ya hesabu zilizokaguliwa na mkaguzi.

Alisema mwisho wa vyama wanachama wa FIFA kuwasilisha ripoti hizo za ukaguzi ilikuwa Juni 30 kwa mujibu wa kanuni namba 14 ya FIFA inayohusiana na masuala ya miradi. Pia alisema, kwa mujibu wa waraka namba 1588 wa FIFA uliotumwa Juni 30, 2017, TFF inatakiwa kutuma FIFA, nakala ya katiba yake ya sasa na kanuni za uchaguzi kwa rejea zao.

FIFA imetoa maagizo hayo wakati TFF ikiendelea na taratibu zake za uchaguzi mkuu uliopangwa kufanyika mjini Dodoma Agosti 12. Barua hiyo ndiyo ilikuwa msingi wa habari yetu ya jana iliyosema FIFA haimtambui Karia bali Malinzi, ambayo ilitokana na chanzo chetu ndani ya TFF lakini haikuwa na usahihi wa kutosha.

Habari hiyo iliyochanganya wasomaji wetu, viongozi wa TFF na wadau mbalimbali wa soka nchini ilipotosha kwa kuonesha kuwa FIFA haimtaki Karia bali inamtaka Malinzi TFF wakati katika barua yake kwa Karia, Omba amemweleza kuwa anamshukuru kwa ushirikiano wake mkubwa na yuko tayari kuendeleza kuwasiliana naye akiwa na tatizo.