Simba kupata silaha 11

KOCHA wa Simba, Joseph Omog amesema wiki ijayo anatarajia kupata kikosi cha kwanza cha wachezaji 11, baada ya kucheza mechi mbili za kirafi ki dhidi ya timu za Orlando Pirates na Bidvest Wits zote zinashiriki Ligi Kuu Afrika Kusini.

Hii ni wiki ya pili sasa Simba imepiga kambi nchini humo, ikijifua kwa ajili ya kujiandaa na msimu mpya wa Ligi Kuu Tanzania Bara, huku lengo kubwa la kocha huyo raia wa Cameroon, kutwa taji ambalo linashikiliwa na mahasimu wao Yanga.

Akizungumza na gazeti hili kutoka Johanesburg, kocha Omog alisema mechi hizo mbili ndiyo zitampa taswira kamili ya ubora wa kikosi chake, baada ya kufanya mazoezi magumu kwa muda wote ambao wapo nchini humo.

“Nimependekeza kucheza na timu hizo mbili, kwa sababu ndiyo kipimo kizuri kwa mazoezi, ambayo tumeyafanya hapa, lakini kitu kikubwa kwangu sio kuangalia matokeo, bali ninachotaka kuona ni namna gani wachezaji wameyashika yale tuliyowafundisha na jinsi wanavyoyafanyia kazi,”alisema Omog.

Kocha huyo alisema atajitahidi kutoa nafasi kwa kila mchezaji katika mechi hizo mbili ili aweze kuona uwezo wa kila mmoja wao kwa sababu hiki ndiyo kipindi ambacho anasaka kikosi cha kwanza hivyo itapendeza akatoa nafasi kwa kila mchezaji aweze kuonesha uwezo wake.

Omog alisema kwa maandalizi waliyofanya anaamini msimu ujao watakuwa ni moja ya timu inayopigania ubingwa wa Ligi ya Bara, na anawashukuru viongozi wa timu yake kwa kuwapa maandalizi mazuri na sasa kazi imebaki kwao kurudisha shukrani kwa kutwaa mataji yote ambayo watagombania.

Kikosi cha Simba kinatarajia kurejea nchini Agosti sita, na siku mbili baadaye kitashuka kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam, kupambana na Rayon Sports, ikiwa ni siku maalumu kwa timu hiyo (Simba Day), ambayo hufanyika kila mwaka dhumuni lake kubwa ni kutambulisha wachezaji wapya pamoja na jezi.