‘Mkojo wa Wema Sepetu una bangi’

MKOJO wa msanii wa fi lamu na Miss Tanzania wa zamani, Wema Sepetu umekutwa na chembe chembe za dawa za kulevya aina ya bangi. Hayo yalielezwa jana na Mkemia kutoka ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Elias Mulima (40) katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Alisema uchunguzi wa sampuli ya mkojo wa Wema uliowasilishwa kwao ulikuwa na chembe chembe za dawa za kulevya aina ya bangi. Mulima ni shahidi wa kwanza katika kesi ya Wema kukutwa na dawa za kulevya aina ya bangi Februari 4 mwaka huu Dar es Salaam.

Shahidi huyo alidai hayo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama ya Kisutu, Thomas Simba shauri hilo lilipokuja kwa kusikilizwa. Akiongozwa na Wakili wa Serikali, Costantine Kakula, shahidi huyo alidai kuwa Februari 2 mwaka huu, alikuwa katika ofisi ya Mkemia mkuu Dar es Salaam ambapo alipokea vielelezo kutoka Jeshi la Polisi vilivyowasilishwa na Koplo Robert kwa lengo la kufanyiwa uchunguzi kujua kama ni dawa za kulevya au la.

Alidai Koplo Robert aliwasilisha bahasha yenye fomu maalumu ya dawa za kulevya aliyoisajili na kuipa namba 291/2017 ambayo ndani yake kulikuwa na msokoto mmoja na vipisi viwili vinavyodhaniwa kuwa ni dawa za kulevya.

‘’Nilipima uzito wa majani hayo yanayodhaniwa kuwa ni dawa za kulevya ambayo yalikuwa na uzito wa gramu 1.08 na kuanza uchunguzi wa awali ambapo niligundua kuwa majani hayo ni dawa za kulevya aina ya bangi,’’ alidai Mulima.

Alidai aliandaa taarifa ya uchunguzi aliyoisaini na kuthibitishwa na Kaimu Mkemia Mkuu wa Serikali inayoonesha bangi ina kemikali inayosababisha mtumiaji kuwa na ulevi ambao hautibiki kirahisi na huleta matatizo ya akili.

Pia alidai, Februari 8, mwaka huu, akiwa ofisi kwake alipokea sampuli mbili moja wapo ikiwa ni mkojo wa Wema aliyepelekwa na Inspekta Willy na WP Mary kwa ajili ya kuchunguzwa.

Alidai alifanya usajili wa sampuli hizo namba 321/2017 na kumpatia WP Mary kontena maalumu kuwekea sampuli ya mkojo wa Wema ambapo walienda choo maalumu kilicho katika ofisi hizo na mshitakiwa alitoa sampuli hiyo.

Mulima alizidi kuieleza mahakama baada ya kupokea sampuli hiyo, aliendelea na uchunguzi uliofanywa kwa hatua mbili, kupata chembe chembe za dawa za kulevya na kujiridhisha kama sampuli ilikuwa na dawa za kulevya au la.

‘’Baada ya uchunguzi ilionekana sampuli ya mkojo wa Wema ilikuwa na chembe chembe za dawa za kulevya. Chembe chembe hizo zinaweza kugundulika ndani ya siku 28 kwa mtumiaji wa dawa hizo.

Niliandaa taarifa kuhusu sampuli hiyo na kusaini ikathibitishwa na Kaimu Mkemia Mkuu,’’ alieleza Mulima. Shahidi huyo aliomba mahakama kupokea vielelezo ambavyo ni fomu maalumu za uchunguzi wa sampuli hizo na akasema kuwa anazitambua kutokana na saini yake, muhuri wa moto na namba za usajili wa maabara alizoipa.

Baada ya upande wa mashitaka kuomba mahakama kupokea vielelezo hivyo, upande wa utetezi ukiwakilishwa na Wakili Peter Kibatala uliomba visipokelewe kwa sababu ripoti iliyowasilishwa haijakidhi vigezo vya kisheria.