Kilomoni kumwaga mboga

MWENYEKITI wa Bodi ya Udhamini wa klabu ya Simba, Mzee Hamis Kilomoni kesho atajibu mapigo ya wanachama na viongozi wa klabu hiyo kumsimamisha kwa madai ya kukiuka katiba kwa kupeleka masuala ya klabu kortini.

Kilomoni alisema jana kesho atazungumzia suala hilo kutoa ufafanuzi wa kinachoendelea Simba na hatma ya Klabu kama mdhamini wao. Juzi Kaimu Rais wa Simba, Salim Abdala alitoa pendekezo wanachama wamwondoe Kilomoni kwenye Uenyekiti wa Bodi ya Wadhamini na kumsimamisha uanachama kwa kuwashitaki.

Alisema Simba ni klabu ambayo ameitumikia kwa muda mrefu na ameona kuna haja ya kulizungumzia suala la adhabu yake rasmi na kuwataka waandishi wa habari kuhudhuria. “Mimi ni Mwenyekiti wa baraza la Wadhamini na ningependa ifahamike kuwa ninayo haki na wajibu wa kuzungumzia lolote kuhusiana na mustakabali wa klabu hii.

Kesho nitaweka wazi msimamo wangu kwa kusimamishwa,” alisema. Aliwataja wajumbe wenzake wa Bodi kuwa ni Abduhalab Patel aliyeenda Ulaya kwa matibabu, Ramesh Patel na Ally Sykes (marehemu)”. Juzi Simba walitangaza kumwondoa na kumteua Abdala Mgoyi kuchukua nafasi yake na Juma Kapuya kuchukua nafasi ya Sykes.

Kilomoni anapinga Simba kubadilishwa mfumo wa uendeshaji kutoka wa wanachama wote kwenda wa hisa za wachache usio na uwazi. Wakati Kilomoni akisema hayo, African Lyon imemwekea pingamizi kipa wake, Mcameroon Youthe Rostand ambaye amesajiliwa Yanga msimu huu ikitaka Yanga iwalipe fidia.

Baada ya Lyon kushuka daraja msimu uliopita wachezaji kadhaa walienda klabu nyingine ambapo Rostand alienda Yanga kwa mkataba wa miaka miwili kumrithi Deogratius Munishi ‘Dida’ aliyeenda Afrika Kusini soka la kulipwa.

Mmiliki wa timu hiyo, Rahim Kangezi tayari amewasilisha barua ya pingamizi hiyo kwenye Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ili kumwekea pingamini mchezaji huyo na kuitaka Yanga kufuata utaratibu wa kulipa fidia.

Kangezi anataka walipwe ada ya mazoezi, ada ya uhamisho, ada ya maendeleo ya mchezaji na fidia ya kuvunja mkataba. Alisema wachezaji wengine 20 wanatakiwa kulipiwa fidia hiyo.

Wachezaji hao ni Miraji Adam (Singida United), Vicent Ludovic (Kagera Sugar), Salehe Malande (Majimaji), Hamad Manzi (Lipuli FC), Hamad Tajiri (Ndanda FC), Omary Salum (Coastal Union), Baraka Majogoo (Ndanda FC) na Abdul Hilal (Tusker).

Wengine ni Omary Abdallah (Kagera Sugar), Abdallah Mguhi (Kagera Sugar), Musa Nampaka (Lipuli FC), Raizan Hafidh (Coastal Union), Lambele Jerome (Lipuli FC). Wengine ni Fred Cosmas, Alhaji Zege, Rehan Nkungu (KMC FC) Halfan Twenye (KMC FC) na Baraka Jafary (Coastl Union), Adhi Juma (Njombe Mji) na Yusuf Abdul (KMC FC). Alisema wachezaji hao walisajiliwa na klabu hizo bila kuzingatia sheria na taratibu za usajili.