Serikali yatoa bil 1/- uwanja wa 'Morocco'

WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe amesema serikali imetenga zaidi ya Sh bilioni moja kwa ajili ya hatua za awali za maandalizi ya ujenzi wa Uwanja wa Michezo mjini Dodoma.

Akizungumza na watalaamu kutoka Morocco, mjini Dodoma jana, Dk Mwakyembe alisema Serikali imetenga fedha hizo ili kufanya maandalizi ya hatua za awali za kujenga uwanja huo wa kisasa.

“Serikali ilijiandaa kwa ajili ya hatua za awali ya kujenga uwanja huo wa kisasa mtangamani kwa kutenga zaidi ya Sh bilioni moja katika bajeti yake ya mwaka huuu 2017/18,” alisema.

Dk Mwakyembe alisema ujumbe huo kutoka Morocco, umefi ka nchini hasa mjini Dodoma kutokana na ahadi aliyotoa Mfalme wa Sita wa Morocco, Mohamed alipofanya ziara ya kihistoria na akaahidi atajenga uwanja huo.

Alisema ujumbe huo umesheheni watalaamu wa usanifu majengo, ujenzi na upimaji ardhi watakaoenda eneo lililosafi shwa kwa ajili ya ujenzi huo la ekari 120 kati ya ekari 300 za uwanja huo karibu na Viwanja vya Nanenane.

Alimshukuru Rais John Magufuli kwa kuikumbuka sekta ya michezo, akisema ndoto za kuwa na uwanja wa kisasa wenye viwanja mchangamani nchini zitatimia. Alisema uwanja huo utakuwa na maduka, hoteli, hosteli na viwanja vya michezo ya ndani na huduma za wanamichezo na watazamaji.

Alisema awali mkoa ulitoa eneo la ekari 150 katika eneo la Nara umbali wa kilometa 70 kutoka mjini Dodoma lakini Rais Magufuli kwa kutaka wananchi wengi wa mjini wapate fursa ya kutumia viwanja hivyo akaagiza mkoa utafute eneo lingine lililo karibu na mjini. Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Jordan Rugimbana alitafuta eneo lingine karibu na viwanja vya Nanenane pembeni ya barabara ya Dar es Salaam lenye ukubwa wa ekari 300.