Yanga yachoka kuibiwa mapato ya jezi

TIMU ya soka ya Yanga imesema imechoka kuibiwa mapato yatokanayo na nembo za jezi zake na sasa inachukua hatua kali kuyadhibiti.

Msemaji wa Yanga, Dismas Ten alisema jana kuwa uongozi wa Yanga unatarajia kukutana na wafanyabiashara wanaouza jezi zenye nembo yao keshokutwa kujadili na kupeana utaratibu maalumu wa uuzwaji wa jezi ili Klabu inufaike.

Alisema mkutano huo utafanyika Makao Makuu ya klabu hiyo mtaa wa Twiga na Jangwani na lengo ni kuwa na watu maalumu ambao watauza jezi zenye nembo yao ya klabu na si vinginevyo.

“Tumeamua kubadili kutumia fursa iliyopo ili kujiongezea kipato kwa kutumia nembo yetu, kuanzia leo kesho (leo). Tukimkamata mfanyabiashara yeyote anauza jezi yenye nembo ya Yanga, tutachukua hatua za kisheria,” alisema.

Ten alisema kwa muda mrefu walilifumbia macho suala hilo na licha ya kuwaelimisha mara kadhaa, hawajaelewa hivyo sasa watawabana. Alisema watakuwa wakali kwani wamegundua wanapoteza mapato mengi kupitia nembo yao hivyo wafanyabiashara wafahamu hilo ili wasije kujikuta matatani watakapokamatwa.

Hatua hii inamaanisha Yanga inaelekea kuanza kujiendesha kibiashara baada ya muda mrefu wa kushindwa kutumia wingi wa mashabiki wake. Yanga imechukua hatua hiyo wakati tayari wafanyabiashara ndogo, Wamachinga, wakiuza jezi na kalenda zenye picha za wachezaji wa Yanga na Simba zinazocheza leo. Yanga inavaana na Simba leo Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam katika mechi ya Ngao ya Hisani.