Mambo yamejipa, yatamba Simba SC

KOCHA msaidizi wa kikosi cha Simba, Jackson Mayanja, amesema safu yao ya ushambuliaji imesikia kilio cha mashabiki wao baada ya juzi kufunga idadi kubwa ya mabao katika mchezo wao wa kwanza wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara dhidi ya Ruvu Shooting ya Pwani.

Katika mchezo huo uliopigwa Uwanja wa Uhuru Dar es Salaam, Simba ilitoa kichapo cha mabao 7-0 kwa Maafande hao huku mshambuliaji wake wa kimataifa wa Uganda, Emmanuel Okwi, akifunga mabao manne peke yake.

Akizungumza baada ya mchezo huo kumalizika, Mayanja alisema ushindi huo walioupata haukuwa wa kubahatisha kwani kwa muda mrefu wakiwa kwenye kambi zao za Afrika Kusini na Zanzibar walikuwa wakishughulika na safu ya ushambuliaji na sasa wanafurahi kuona mbinu walizowapa washambuliaji wao zimeanza kutoa majibu.

“Hatukubahatisha haya ni mafunzo ya muda mrefu ambayo tumeyaanza tangu Afrika Kusini na Zanzibar, lakini pia haitakuwa mwisho tutaendelea na ushindi wa aina hii ingawa idadi inaweza kupungua kufikia tano au nne,” alisema Mayanja.

Kocha huyo pia alisema sababu ya kucheza vizuri na kuutawala mchezo huo ni kutokana na kikosi kipana walichokuwa nacho msimu huu ambacho ndani yake kina wachezaji wengi wenye uwezo wa kucheza nafasi zaidi ya moja uwanjani.

“Angali Haruna Niyonzima aliumia na kutolewa lakini alivyoingia Mohamed Ibrahim na kucheza nafasi yake alicheza vizuri na pasipo kuonekana pengo lake, hii inaonesha kwamba msimu huu tumejipanga kuhakikisha tunabeba taji la Ligi Kuu na kumaliza kiu ya muda mrefu waliyokuwa nayo mashabiki wetu,”alisema Mayanja.

Kwa upande wake kocha wa Ruvu Shooting, Abduli Haji ‘Kiduu’ alikiri timu yake kuzidiwa na Simba katika mchezo huo na sababu kubwa iliyochangia wao kupoteza mchezo huo kwa idadi kubwa ya mabao ni kuwakosa wachezaji wake sita wa kikosi cha kwanza ambao wapo nchini Burundi kwenye mashindano ya Majeshi.

“Hatukucheza vizuri na Simba walistahili kushinda kwa sababu tulikuwa na makosa mengi uwanjani hasa kwenye safu yetu ya ulinzi ambayo ilikuwa inakatika kila wakati na kuwapa mwanya wapinzani wetu ambao kutokana na kuwa na wachezaji wenye uzoefu kama Okwi ilikuwa vigumu kupoteza nafasi hizo,”alisema Kid