Okwi mashine

MSHAMBULIAJI wa timu ya soka ya Simba, Emmanuel Okwi jana alithibitisha ni moto wa kuotea mbali katika Ligi Kuu ya soka Tanzania bara baada ya kuifungia mabao mawili kati ya matatu, ambayo Simba iliichapa Mwadui FC ya Shinyanga katika mchezo uliofanyika Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.

Okwi, ambaye wiki iliyopita alitangazwa na Shirikisho la soka Tanzania (TFF) kuwa mchezaji wa mwezi Agosti na kuzawadiwa Sh milioni moja na wadhamini wa Ligi hiyo, Vodacom, alifunga bao moja kila kipindi na la tatu likafungwa na John Bocco.

Alifunga bao la kwanza katika dakika ya saba baada ya kupiga mkwaju mkali uliomgonga beki na kujaa wavuni baada ya kupokea pasi ya Shiza Kichuya aliyegongeana naye vizuri. Mshambuliaji huyo mhenga raia wa Uganda aliongeza bao la pili dakika ya 67 baada ya kuchukua mpira na kutisha kama anapiga kisha akaachia mkwaju mkali na kufunga.

Dakika tano baadaye, dakika ya 72, Bocco alimchambua beki wa Mwadui FC na kufunga bao safi la tatu kwa Simba na la kwanza kwake katika ligi msimu huu. Bocco alifunga bao hilo dakika mbili tu baada ya Okwi kupiga mpira wa adhabu uliotoka sentimeta chache nje.

Kwa ushindi huo, Simba sasa imefikisha pointi saba sawa na Azam FC iliyokuwa ya pili kwenye msimamo nyuma ya Mtibwa Sugar inayoongoza kwa pointi tisa hadi jana. Simba imeiengua Azam FC katika nafasi ya pili kwa kuwa ina magoli 10 ya kufunga na haijafungwa bao katika mechi tatu ilizocheza dhidi ya Azam, Mwadui na Ruvu Shooting ambayo ilifungua nayo dimba na kuishinda 7-0.

Pamoja na kufungwa, Mwadui FC walitoa upinzani kwa Simba na mara kadhaa walifanikiwa kuonesha makali yao. Mwadui FC ndio walikuwa wa kwanza kufika langoni mwa Simba lakini shuti lililopigwa na mchezaji lilipita juu. Timu zote zilishambuliana kwa zamu hadi dakika ya 16, Okwi alipopiga mkwaju wa faulo lakini mpira ukapita juu.

Kipindi cha pili kilianza kwa kasi Simba wakionekana kupania kupata bao la pili kujihakikishia ushindi. Dakika ya 48, Okwi aliambaa vizuri na mpira pembeni na kutoa krosi nzuri lakini Ndeule akaokoa. Okwi alirudi tena dakika tatu baadaye akiwa amebaki na kipa Massawe akapiga juu.

Katika dakika ya 54, Simba waligongeana vizuri lakini Bocco aliyekuwa wa mwisho kumalizia akaachia mkwaju ukatolewa kona iliyochongwa na Kichuya ikaokolewa. Dakika mbili kabla ya hapo, Mwadui walimpima kipa wa Simba, Aishi Manula akaruka juu kudaka krosi ya Ndeule.

Mwadui walijaribu bahati yao tena dakika ya 56 na kupata kona lakini Manula akada kwa ustadi na dakika ya 58, Mbonde aliruka na kuondosha mpira hatarini. Katika kuongeza nguvu, Simba ilifanya mabadiliko dakika ya 60 kwa kumwingiza Mwinyi Kazimoto na kumtoa Gyan