Simba, Mtibwa, shughuli yao kubwa

SIMBA leo itakuwa mwenyeji wa Mtibwa Sugar kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara katika Uwanja wa Uhuru Dar es Salaam.

Ni mchezo unaotabiriwa kuwa mgumu hasa ikizingatiwa kuwa wote ni wababe wakiwa na pointi sawa, 11 na kabla ya mechi za jana walikuwa wakifuatana nafasi ya kwanza na pili.

Timu hizo zote hazijapoteza mchezo, zote zina rekodi nzuri kila moja imeshacheza mechi tano. Kilichowatofautisha ni uwiano wa mabao. Simba imefunga mabao 14 ikifungwa matatu na Mtibwa mabao matano ikifungwa mawili tu.

Timu hizi zinafahamiana kwani kuna wachezaji wengi walioko Simba wametoka Mtibwa akiwemo Shiza Kichuya, Salim Mbonde, Mzamiru Yasini na Mohamed ‘Mo’ Ibrahim.

Wekundu hao wanapewa nafasi ya kushinda kwenye uwanja wa nyumbani, kwani hucheza kwa kujiamini ikiwa na washambuliaji hatari, Emmanuel Okwi ambaye kwenye uwanja huo alifunga mabao sita katika michezo miwili.

Simba ina safu bora ya ulinzi inayoongozwa na kipa Aishi Manula, Method Mwanjele, Salim Mbonde na Erasto Nyoni. Mtibwa Sugar inao wachezaji hatari kama Mohamed Issa, Dickson Daud, Salum Kihimbwa, Issa Rashid, Salum Kupela na kipa Benedict Tinoco.

Katika mchezo uliowakutanisha Septemba mwaka jana Simba ilishinda mabao 2-0. Simba mchezo wa mzunguko wa tano wa ligi msimu huu imetoka kushinda 2-1 ugenini dhidi ya Stand United na Mtibwa Sugar ikipata suluhu dhidi ya Yanga.

Kila moja itataka ushindi kuhakikisha inalinda nafasi yake katika harakati za kuliwania taji la ligi. Mchezo mwingine utakaochezwa leo ni Tanzania Prisons dhidi ya Stand United kwenye Uwanja wa Sokoine, jijini Mbeya.