Magereza yaeleza maisha ya Lulu jela

MSANII wa fi lamu nchini, Elizabeth Michael ‘Lulu’ jana alianza maisha mapya ya gerezani baada ya kuhukumiwa kifuko cha miaka miwili jela. Makahama Kuu Kanda ya Dar es Salaam ilimhukumu Lulu kifungo hicho baada ya kumtia hatiani kwa kosa la mauaji bila kukusudia ya aliyekuwa mpenzi wake na msanii mwenzake, Steven Kanumba.

Akizungumza na gazeti hili jana, Ofisa habari wa jeshi la Magereza Mrakibu Msaidizi Lucas Mboje alisema Lulu amepokelewa kama wafungwa wengine na adhabu yake alianza kuitumikia jana baada ya kufikishwa gerezani.

“Lulu ni kama mfungwa mwingine yeyote, unapopelekwa gerezani kutumikia kifungo hakuna suala la umaarufu, hatuangalii hilo… anapokelewa kama wafungwa wengine, akifika anakabidhiwa mavazi yake na kusomewa sheria na taratibu za kuishi gerezani lakini pia ana haki zake za msingi kama kutembelewa na ndugu na jamaa na kukata rufaa kama ilivyo kwa wafungwa wengine,” alisema.

Lulu amepata hukumu hiyo akiwa kwenye maandalizi ya kufanya filamu yake baada ya kuwa kimya muda mrefu akisoma Stashahada ya Uongozi wa Rasilimali Watu (HRM) katika Chuo cha Utumishi wa Uma (TPSC), Magogoni, Dar es Salaam. Lakini pia ndiyo kwanza alikuwa amepata mkataba wa kuwa balozi wa tuzo za filamu za SZIFF chini ya Azam kupitia chanel ya Sinema Zetu.

Tuzo hizo zimepangwa kufanyika Aprili mwakani na tayari zilishazinduliwa hivi karibuni. Akisoma hukumu hiyo jana, Jaji Sam Rumanyika alisema ameridhika na ushahidi wa mashahidi wanne wa upande wa mashitaka na maoni ya wa zee watatu wa baraza kuwa kweli Lulu aliua bila ya kukusudia. Alisema kwa mara ya kwanza Lulu alifikishwa katika Mahakama ya Mkoa wa Dar es Salaam ambayo ni Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Aprili 12, 2012 kujibu mashitaka ya mauaji ya Kanumba.

Alieleza kuwa baada ya kusota rumande kwa takribani miezi kumi, Lulu alibadilishiwa mashitaka na kushitakiwa kwa mauaji ya bila kukusudia, mashitaka yaliyomuwezesha kuwa nje kwa dhamana hadi jana aliposomewa hukumu hiyo. Katika kesi hiyo, Lulu anadaiwa Aprili 7, 2012 maeneo ya Sinza Vatican Dar es Salaam, alimuua bila ya kukusudia Kanumba na kwamba upande wa serikali uliwakilishwa na Mawakili, Faraja George, Yusuph Abood na Batilda Mushi huku upande wa utetezi uliwakilishwa na Peter Kibatala na Omary Msemo.

Akisoma hukumu hiyo, Jaji Rumanyika alisema, kesi hiyo imejikita katika ushahidi wa mazingira na kwamba mshitakiwa mwenyewe alikubali kwamba yeye ndiyo alikuwa mtu wa mwisho kuwa na marehemeu Kanumba ambaye alikuwa mpenzi wake kwa miezi minne. Alisema ili kuthibitisha kesi hiyo ni watu wawili pekee ndiyo wenye uwezo huo ambao ni mshtakiwa na marehemu Kanumba.

“Kwa sababu hiyo, mshitakiwa anatakiwa kutoa maelezo ya kina yanayojitosheleza na akishindwa kufanya hivyo ataonekana kwamba yeye ndiye muuaji. Ushahidi wa mazingira unaweza kutumika kama msingi pekee endapo utaendelea kumnyooshea kidole mshtakiwa,” alisema Jaji Rumanyika.

Alisema maelezo aliyoyatoa mshitakiwa yanakidhi viwango na vigezo kwa kuwa alikubali kwamba walikuwa na mzozo uliosababisha kupigwa na kwamba si matakwa ya sheria mshitakiwa athibitishe kosa la hasha, bali anatakiwa kueleza namna kifo kilivyosababishwa. Alisema: “kwa maoni yangu kuanguka au kudondoka kwa mtu mmojawapo katika ugomvi inasababishwa na kusukumwa au kukabwa”.

Alisisitiza kuwa mshitakiwa alikuwa na jukumu la kutoa maelezo ya kutosha kuhusu tukio lililotokea na kwamba alijikanganya wakati akitoa utetezi wake. Alieleza kuwa Lulu aliiambia mahakama kwamba Kanumba alikuwa amelewa na desturi ya mlevi mara nyingine huanguka, lakini yeye alieleza kuwa aliburuzwa na kurudishwa chumbani hivyo kama alikuwa mlevi hakueleza kama wakati wanakimbizana alianguka.

Pia alisema maelezo yaliyotolewa na Josephine Mushumbuzi kama ushahidi wa upande wa utetezi, yanaacha maswali mengi kwa sababu hayana hadhi ya cheti cha daktari kwa kuwa tayari mahakama ilitambulishwa kuwa Daktari Paplas Kagaiga ndiyo daktari wa familia.

Alisema mshitakiwa mwenyewe pamoja na mdogo wa marehemu, Seth Bosco ambaye ni shahidi wa kwanza katika kesi hiyo walieleza kuwa ndiye daktari wa familia hivyo ndiye aliyepaswa kujua historia ya marehemu ikiwemo afya yake na maradhi yanayomsumbua na siyo maelezo ya Mushumbusi. Jaji Rumanyika alisema kwa kuwa mshitakiwa alikuwa na mahusiano ya kimapenzi kwa miezi minne na Kanumba, na kwa kuwa alimfahamu kwa undani alitarajiwa ajue maradhi ya marehemu yanayomsibu lakini kwenye utetezi wake hajaeleza.

“Maelezo yake yanakinzana na hekima ya kawaida kwa sababu hata pale marehemu alipokuwa akimpiga na kumtishia kumuua kwa panga hakuthubutu kufanya chochote, kumsukuma wala kumrudishia bali alichukua taratibu zile za Kibiblia kwamba akupigaye shavu la kulia mgeuzie na la kushoto,” alisema. “Akiwa mtu wa mwisho kuwa na marehemu hakutoa maelezo ya kina na ya kutosheleza ni kitu gani hasa kilitokea hadi kukutwa na mauti,” alisema.

Jaji Rumanyika alisema wakati tukio linatokea mshitakiwa alikuwa mtoto wa umri wa miaka 17, lakini alikubali kuitwa mke na kuthubutu kufanya vitu tofauti na maelekezo ya wazazi wake kwa kuamua kutoka nyumbani kwenda matembezi usiku wa manane.

Alisema mtoto wa umri kama wake ambaye ameweza kuyafanya ya watu wazima siyo mmoja wa wale watoto waliolengwa kulindwa na sheria ya watoto, hivyo kuwa mtoto wa umri na kuweza kufanya kama alichofanya Lulu kwa kujiamini, mahakama zitegemee kuona watu wazima wazee wakifanya mambo ya watoto na kuomba kulindwa kwa haki sawa.

Alifafanua kuwa watunzi wa sheria ya watoto walikuwa na maana ya umri na siyo ukomavu kama amesherehekea sikukuu ngapi za kuzaliwa na kwamba kukua na kuzeeka ni jambo moja na ukomavu ni jambo lingine. “Kama wanasheria na majaji wataendelea kuwa na fikra na mawazo yaliyosimama huku jamii ikiwa inaendelea kwa kasi, basi watashindwa kuonesha kwa vitendo utawala wa sheria kwa kasi hiyo nami sitaki kuwa wa kwanza,” alisema.

Pia alisema mahakama ikiacha kufanya yale ambayo sheria hazijaruhusu, lazima kuwepo na jamii isiyokuwa na maendeleo kisheria hivyo kushindwa kutimiza matakwa ya kikatiba. “Ninajiridhisha kuwa kifo cha marehemu kimetokana na ugomvi ndiyo maana mshitakiwa alishitakiwa kwa kosa la mauaji bila kukusudia na hata katika utetezi wake, mshitakiwa alisema marehemu alikuwa na wivu uliopitiliza ambao haukuwa na maana… lakini hakuna mchezo usiokuwa na kanuni na katika mapenzi wivu ni moja ya kanuni zake,” alisisitiza Jaji Rumanyika. Alisema, kuna wivu wa maendeleo ambao huleta maendeleo lakini wivu wa mapenzi huleta maangamizi.

Alieleza kuwa kama Lulu alishajiingiza katika mapenzi huku akifahamu kwamba marehemu alikuwa na wivu kumbe hata alivyoanza kumshuku kwa simu, alitakiwa aachane nayo ili kuepusha ugomvi lakini yeye alichukua kwa misingi ya liwalo na liwe. Baada ya kutiwa hatiani, Lulu ambaye alikuwa amevalia vazi aina ya dera na kujifunga kilemba kichwani alianza kukunja kunja vidole na mikono yake huku akipandisha na kushusha gauni lake na kuanza kujifuta machozi yaliyokuwa yakimtiririka.

Kabla ya kutolewa adhabu, Wakili wa Serikali, Faraja alidai hawana kumbukumbu za makosa ya nyuma ya Lulu, lakini kwa vile mashitaka hayo yamehusisha uhai wa mtu, mahakama itoe adhabu stahiki dhidi ya mshitakiwa. Wakili wa utetezi, Kibatala alidai mshitakiwa anategemewa na familia yake ambao ni mama na mdogo wake, pia ni balozi wa taasisi mbalimbali ambazo zinamuwezesha kiuchumi.

Pia alisema mshitakiwa huyo ataangaliwa kwa macho ya dhihaka na jamii inayomzunguka na kwamba Lulu amebadilika tangu tukio lilipotokea, hivyo anaamini ataendelea kubadilika kwani tayari alishakaa rumande. Alieleza kuwa amemaliza masomo ya diploma na anategemea kujiunga na chuo kikuu licha ya kwamba wazazi wake hawaishi pamoja bali wamekutana katika tukio hilo.

“Marehemu alipaswa kumpa muongozo kwa wakati ule kwa kuwa alikuwa na umri mdogo pia alipaswa kumsubiri. Hivyo mahakama ione adhabu ya kifungo itamuathiri bali apewe nafasi ya kukaa nje ili aweze kuwa na mawasiliano kati yake, jamii na walio karibu hivyo tunaomba asipewe adhabu kali,” alidai Kibatala.

Kabla ya kutolewa kwa hukumu ya Lulu, washitakiwa wengine watatu ambao walisomewa hukumu jana na Jaji Rumanyika, waliachiwa huru kwa mashitaka ya mauaji na hata baada ya Lulu kuhukumiwa kifungo hicho umati wa watu waliofika mahakamani hapo ulihamaki na baadaye mama yake mzazi, mashabiki, ndugu na jamaa zake waliangua vilio na kusababisha mama yake Lulu kushikiliwa na watu watatu baada ya kukosa nguvu kwa kulia. Kwa upande wa mama Kanumba, ambaye alitoa machozi akiwa nje ya mahakama alishukuru mahakama kwa kutenda haki na kueleza kuwa anakwenda kumzika rasmi mwanaye.

Aidha, Kibatala alidai kuwa upande wa utetezi umekusudia kukata rufaa kupinga kifungo hicho. Lulu alizaliwa na kukulia Dar es Salaam na mama Lucrecia Kalugira na baba Michael Kimemeta. Alianza kuigiza tangu akiwa mdogo kwenye kundi la sanaa la Kaole.

Alipata elimu yake ya msingi katika Shule ya Remnant Academy kabla ya kwenda sekondari za Perfect Vision na St Mary’s, za Dar es Salaam. Baadhi ya mafanikio katika sanaa ni kupata tuzo ya mwigizaji bora wa Tamasha la filamu Tanzania (ZIFF) mwaka 2013 na tuzo ya Afrika Magic ya Filamu Bora Afrika Mashariki mwaka 2016.